Vipimo ni muhimu sana kwa maendeleo ya afya zetu, kwa watu wa jinsia zote na
rika zote. Kupitia vipimo tunaweza kutambua mustakabali wa afya zetu na hivyo
kujiweka kwenye nafasi nzuri katika kupambana na maradhi mbalimbali.
Hivi karibuni, takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) zilionesha kuwa idadi
ya wanaume watu wazima wanaopatiwa vipimo vya afya ni ndogo kuliko idadi ya
jinsia nyingine.
Kama nilivyokuahidi katika toleo lililopita, leo tutaendelea kukumbushana aina ya
vipimo ambayo unapaswa kuvipata na kufahamu majibu yake.
Vipimo vya shinikizo la juu la damu
Hatari ya kupata shinikizo la juu la damu huongezeka kadri umri unavyosogea,
lakini pia shinikizo la juu la damu lina uhusiano mkubwa na uzito wa mwili
kupitiliza na aina ya maisha, kama vile ulaji wa vyakula vyenye mafuta kwa wingi,
na kutofanya mazoezi ya viungo mara kwa mara na sababu za kisaikolojia.
Shinikizo la juu la damu humpata mtu bila dalili zozote, na linaweza kuleta
madhara makubwa mengine ya kiafya kama vile magonjwa ya moyo, kiharusi na
hata kusababisha figo kushindwa kufanya kazi.
Hivyo, ni muhimu kujua vipimo vyako vya shinikizo la damu mara kwa mara na
kama vinaashiria kupanda ni vyema kupata msaada wa daktari mapema.
Vipimo vya kisukari
Kisukari ni ugonjwa unaowapata watu wa jinsia zote lakini takwimu zinaonesha
kuwa wanaume wapo hatarini zaidi kupata kisukari kuliko wanawake. Ni ugonjwa
unaotokana na uwepo wa kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu.
Huenda ikasababishwa na aina fulani ya maisha kama vile ulaji wa aina fulani ya
vyakula vinavyosababisha kisukari, kutofanya mazoezi lakini hata sababu za
kifamilia zinazotokana na kurithi.
Japo kisukari pia kinaweza kuwapata watu wa rika zote lakini inashauriwa pia ni
vyema kwa wenye umri wa kuanzia miaka 45 kupata vipimo vya kisukari mara
kwa mara kwa kuwa kisukari pia kinawapata zaidi watu wenye umri wa utu uzima
na kuendelea.
Vipimo vya glakoma

Glakoma huenda likawa ni neno geni miongoni mwa wengi, jina hili linaunganisha
makundi ya magonjwa ya macho ambayo husababisha kuharibu neva zilizopo
ndani ya macho na hatimaye kusababisha upofu wa kudumu. Glakoma inaweza
kutokea bila kuambatana na dalili yoyote hadi pale mgonjwa anapojikuta
amekuwa mpofu ghafla.
Ni muhimu kupata vipimo vya macho mara kwa mara kubaini madhara yoyote
yanayoashiria kujitokeza kwenye macho. Ni kweli kwamba watu wengi hawana
utamaduni wa kupima macho mara kwa mara.
Ugonjwa huo huwa na dalili mbalimbali kwenye macho kama vile matatizo ya
kuona, macho kuuma na kuwasha na hata kutoa machozi. Ni vyema ikafahamika
kuwa glakoma inashambulia jicho bila kuambatana na dalili zozote.
Hivyo, ni vyema kufanya vipimo mara kwa mara hata kama unahisi huna tatizo
lolote kwenye macho yako. Vipimo vya glakoma vinashauriwa kufanyika kwa
kuzingatia umri na mazingira hatarishi ya kupata ugonjwa huu kwa mtu husika.
Kwa wenye umri wa miaka chini ya 40, wafanye vipimo angalau kila baada ya
kipindi cha miaka miwili hadi minne, kwa wenye umri wa miaka 40-54
wanashauriwa kufanya vipimo angalau kila baada ya mwaka 1-3 na kuanzia umri
wa miaka 55 na kuendelea wanashauriwa angalau kufanya vipimo angalau mara
mbili kwa mwaka mmoja.

By Jamhuri