Mabadiliko hayazuiliki. Kubadilika kwa ajili ya
yaliyo bora ni ajira ya wakati
wote.
Adlai E. Stevenson II
Mabadiliko ni kanuni ya maisha na
uumbaji. Hebu fikiri na uwaze. Ulipokuwa na
umri wa miaka mitatu, ulikuwa wewe? Bila
shaka ulikuwa ni wewe.
Lakini sasa umebadilika, lakini bado ni wewe.
Je, ulipokuwa na umri wa wiki moja,
ulikuwa wewe? Ndiyo, ulikuwa ni wewe. Lakini
sasa umebadilika, lakini bado ni wewe.
Je, ulipokuwa tumboni mwa mama yako,
ulikuwa ni wewe? Ndiyo ulikuwa ni wewe. Sasa
umebadilika, lakini bado ni wewe. Je, miaka
300 iliyopita ulikuwa wapi? Bila shaka mbele ya
Mungu ulikuwa ni ‘wazo’.
Lakini bado ni wewe uliyekuwa wazo mbele ya
Mungu. Tafakari miaka 200 ijayo hautakuwa
hai, lakini bado utakuwa ni wewe.
Mwanafalsafa, Henri Bergson, anasema:

“Kuishi ni kubadilika, kubadilika ni kukamilika,
kukamilika ni kuendelea kujiumba mwenyewe
pasipo mwisho.” Mabadiliko hayazuiliki,
mabadiliko ni ya lazima, hakuna yeyote duniani
anayeweza kuyakwepa.
Kila mtu katika maisha yake anafikiria
kuwabadili watu wengine. Ni watu wachache
wanafikiria kubadilika wao wenyewe. Mafanikio
yaliyo bora kiroho, kimwili, kiuchumi na
kifamilia ni kila mtu kukubali kuwa; ‘Mabadiliko
mazuri anayotaka kuyaona yakitokea duniani’.
Badilika ili uwabadili wengine.
Kubali kuwa mabadiliko. Fanyika kuwa
mabadiliko. Badilika ili mke/mume wako
abadilike kupitia wewe. Badilika ili jirani yako
abadilike kupitia wewe. Badilika ili watoto wako
wabadilike kupitia wewe.
Badilika ili mfanyakazi mwenzako abadilike
kupitia wewe. Badilika ili familia yako ibadilike
kupitia wewe. Badilika ili mtaa wako ubadilike
kupitia wewe. Badilika ili taifa lako libadilike
kupitia wewe.
Badilika ili dunia ibadilike kupitia wewe.
Mabadiliko yanaanza na mimi. Mabadiliko
yanaanza na wewe. Kabla haujafikiri kumbadili
mtu yeyote, fikiri kwanza kujibadili wewe
mwenyewe.
Rinohold Niebuhr, alisali sala hii: “Mungu, nipe

utulivu wa kukubali mambo ambayo siwezi
kuyabadili; na ujasiri wa kubadili mambo
ambayo naweza kuyabadili; na hekima ya
kujua tofauti zake.”
Maisha yetu yamejaa vipindi visivyotarajiwa.
Usipokuwa mpokeaji wa mabadiliko katika
mtazamo chanya, utakuwa mhanga wa
mabadiliko katika mtazamo hasi. Mwandishi,
mnenaji na mshauri wa biashara, Brian Tracy,
anasema: “Azimia kuwa bwana wa mabadiliko
kuliko kuwa muathirika wa mabadiliko.” Kinga
pekee dhidi ya athari hasi ya mabadiliko ni
kuyatarajia na kujiandaa kuyapokea katika
mtazamo chanya. Iko hivi; ukipambana na
mabadiliko, utaishia kuwa muathirika wa
mabadiliko. Ukikubaliana na mabadiliko,
utakuwa mshindi wa mabadiliko.
Njia bora ya kukabiliana na mabadiliko katika
maisha yako ni kuyafanya mabadiliko
yawe rafiki yako na si adui yako. Hatuwezi
kuyazuia mabadiliko. Hatuwezi
kuyachelewesha mabadiliko. Hatuwezi kuyaua
mabadiliko. Mabadiliko daima ni utangulizi wa
yajayo kwa yaliyopo. Mabadiliko ni kesho
inayobadilika leo. Kuyakataa mabadiliko ni
uamuzi wa kuishia jana. Bila kujali chanzo cha
mabadiliko, iwe binafsi, kijamii, kisiasa,
kiuchumi au kiroho hatuwezi kujifanya kuwa

mabadiliko hayatokei.
Yanapotokea tusiyakatae. Badala yake tutafute
namna bora ya kuyaelewa. Unatakiwa kupata
faida kamili kila fursa za mabadiliko
zinapojitokeza katika maisha yako.

Mwisho

By Jamhuri