*Vijiji 20 kugawiwa fedha, chakula, elimu

Wakati bado mjadala wa upendeleo wa wilaya yake ukiendelea kumwandamana Rais Jakaya Kikwete, mradi mwingine wa mabilioni ya shilingi umepelekwa katika vijiji 20 vya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Mradi huo ni wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Zilizo Katika Mazingira Hatarishi, na kwamba baada ya Bagamoyo, utasambazwa katika maeneo yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.


Tayari kuna malalamiko kwamba Serikali ya Rais Kikwete imependelea Bagamoyo, kwa kujenga bandari kubwa kuliko zote katika ukanda wa Afrika Mashariki, kujengwa kwa reli, barabara na fursa nyingine nyingi za kiuchumi.

 

Kwa Bagamoyo ambako mradi huo unaanzia, vijiji 20 vya Halmashauri ya Bagamoyo vyenye kaya 3,056 vimeshatambuliwa. Mpango huo unalenga kuziwezesha kaya maskini kupata chakula na kujiongezea fursa za kipato, kwa kuzipatia fedha ili kumudu mahitaji ya msingi kama vile lishe bora, huduma za afya na elimu.

 

Taarifa hiyo njema kwa wana-Bagamoyo imetangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, katika Hotuba ya Bajeti ya Ofisi yake ya mwaka wa fedha wa 2013/2014.


Hata hivyo, baadhi ya wabunge wamekosoa upendeleo huo, wakisema kuna wilaya maskini zaidi zilizostahili kuanza kufaidi mradi huo. Moja ya wilaya maskini kabisa ni Bunda iliyo mkoani Mara. Wilaya hiyo inatajwa kuwa ndiyo ya kwanza kwa umaskini nchini.


“Zoezi hilo (mpango huo) linaendelea kwenye halmashauri nyingine 13, na ifikapo Juni 2014, halmashauri zote nchini zitafikiwa,” amesema Pinda. Kutekelezwa kwa mradi huo, anasema Pinda, kumetokana na mafanikio yaliyopatikana chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ulio chini ya Ofisi ya Rais (TASAF). Agosti 15, 2012 Rais Kikwete alizindua awamu ya tatu ya TASAF mjini Dodoma.


“Awamu hiyo itagharimu Sh bilioni 440. Mpango huo utatekelezwa kwa awamu katika halmashauri zote Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema Pinda.  Katika hatua nyingine, Pinda amesema Serikali imeratibu na kufanya tathmini ya mifuko mbalimbali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.


Mifuko hiyo ni pamoja na Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi, Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira, Sido, Self, Agriculture Input Trust Fund na Presidential Trust Fund. Mifuko mingine ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Mauzo ya Nje, na Mfuko wa Kudhamini Taasisi za Fedha Kutoa Mikopo kwa Miradi Midogo na ya Kati.

 

Amesema katika makubaliano yaliyofikiwa baina ya Serikali na taasisi za fedha zilizoteuliwa kutoa mikopo kwa wajasiriamali, ni kwamba taasisi hizo zikopeshe mara tatu zaidi ya dhamana iliyotolewa na Serikali.

 

“Katika kutekeleza makubaliano hayo, hadi Desemba 2012 Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira, ulitoa mikopo kwa wajasiriamali 76,546 yenye thamani ya Sh bilioni 50.06.  Urejeshaji wa mikopo hiyo umefikia wastani wa asilimia 82. Katika kipindi hicho, Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi umetoa mikopo ya Sh bilioni 8.6 kwa mikoa 11, wilaya 27, vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOs) 49 na wajasiriamali 8,497.


“Ufuatiliaji wa maendeleo ya mifuko mbalimbali ya uwezeshaji, unaonesha kuwa wananchi waliopata mikopo wameweza kupiga hatua za kimaendeleo, kwa kuongeza tija na uzalishaji katika shughuli zao na hatimaye kuongeza kipato na kuboresha hali zao za maisha.

 

“Utekelezaji wa awamu ya pili ya Tasaf ulikamilika mwaka 2012. Tathmini ya utekelezaji imeonesha kwamba Tasaf imetoa mchango mkubwa katika kuwezesha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo vijijini iliyoibuliwa na wananchi.


Katika utekelezaji wa awamu hiyo, miradi 1,010 yenye thamani ya Sh bilioni 20 iliibuliwa na kuwezeshwa katika wilaya za Tanzania Bara na Zanzibar.


“Aidha, mafunzo ya ujasiriamali yalitolewa kwa vikundi 1,778 vyenye wanachama 22,712 katika halmashauri 44, kwa lengo la kuviimarisha ili kuongeza ufanisi zaidi katika shughuli zao,” amesema Pinda.


 

1082 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!