Wiki iliyopita, Serikali imewasilisha bajeti yake bungeni. Bajeti hii imetangaza maeneo mengi ya kuboresha uchumi wa nchi hii. 

Imetangaza uwekezaji mkubwa katika reli, ununuzi wa ndege, ujenzi wa barabara za kisasa, ununuzi wa meli, kuweka mazingira bora ya uwekezaji, upimaji wa ardhi, uwezeshaji wa wananchi kupitia Sh milioni 50 kwa kila kijiji na mambo mengine mengi mazuri.

Bajeti hii pia imetoa kipaumbele katika elimu. Kimsingi tunaiona bajeti hii kuwa kwa mtazamo wa muda mrefu imeweka msingi imara wa nchi yetu kuzalisha wafanyabiashara wakubwa, na hatimaye kutoa ajira na kulipa kodi nyingi serikalini. Tunaipongeza pia Serikali kuweka utaratibu wa malipo ya kiinua mgogo kwa wabunge kukatwa kodi.

Wakati tukiipongeza Serikali kwa uamuzi huu wa msingi, tunaomba kuainisha hatari tulizoziona katika bajeti iliyowasilishwa. Ipo hatari kuwa Bunge kwa kushirikiana na Serikali wasipofanya marekebisho katika baadhi ya maeneo, basi wajue fika kuwa uchumi wa nchi yetu unaweza kuanguka kifo cha mende.

Eneo la kwanza ni la utalii. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameliambia Bunge kuwa mawaziri wa fedha wa Afrika Mashariki walikaa na kukubaliana maeneo aliyowasilisha bungeni. Wakati Tanzania imetangaza kuanzisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye huduma za utalii, Kenya kupitia bajeti yake imeondoa VAT katika huduma za utalii.

Hii inathibitisha wasiwasi uliopo miaka yote kuwa Wakenya wanatindikiwa uaminifu katika ahadi wanazoipa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sisi tukiweka VAT kwenye utalii, gharama za utalii zitakuwa kubwa na huo ndiyo utakaokuwa mwanzo wa mwisho wa watalii kuja hapa nchini mwetu. Kimsingi tunaiomba Serikali na Bunge VAT hii iondolewe.

Eneo jingine tunalodhani linahitaji marekebisho ni la mikutano yote kufanywa kwenye kumbi za Serikali na kutoruhusu warsha au makongamano kwenye hoteli. Hoteli nyingi tayari zinapunguza wafanyakazi. Tunasema ndiyo, tusiruhusu ufujaji, lakini kwa makusudi Serikali ilegeze kamba kidogo na kuruhusu japo mikutano michache kwenye hoteli.

Huduma ya hoteli ikififia, watalii wataondoka. Mwaka jana nchi imepata dola bilioni 2. Iwapo utalii ungeendelezwa, nchi hii inaweza kupata hadi dola bilioni 15, ambazo ni zaidi ya bajeti ya nchi hii. Eneo jingine, ni ushuru wa karatasi. Kuongeza ushuru kutoka asilimia 10 hadi 25, hii inaweza kuwa kikwazo katika elimu kwa kufanya vitabu, madaftari na magazeti kuuzwa kwa bei ghali, kitu kisichofaidisha Watanzania. Hatuna viwanda vya karatasi kwa sasa.

Mwisho, ni hatua ya Serikali kusema itatoa kipaumbele kwa taasisi zake katika kufanya biashara. Tunakubaliana na dhana ya kubana matumizi, lakini ikiwa hilo litatokea basi tujue fika kuwa hiyo inayoitwa sekta binafsi tunayoijenga itachukua muda au itakuwa vigumu kusimama kwa miguu yake.

Serikali iwawezeshe wawekezaji wa ndani kwa kufanya nao biashara. Vinginevyo, dhamira ya ujenzi wa viwanda tunayoamini ni nguzo ya maendeleo ya kweli kwa Taifa hili, itaingia dosari kwa bidhaa zao kukosa soko.

By Jamhuri