Na Mwandishi Maalum
Makala ya mwisho katika mfufulizo wa makala za Bandari tuliona jinsi Bandari ya
Mwanza ilivyo kiungo muhimu kwa uchumi na biashara katika mikoa ya Kanda ya
Ziwa, nchi za Afrika Mashariki na maeneo mengine. Leo katika makala hii tutaona
umuhimu wa kufanya biashara katika bandari zenye usalama na mazingira rafiki
na yanayovutia wateja.
Katika utekelezaji wa shughuli zake za kupakia na kupakua mizigo melini na
kuhifadhi shehena zinazosubiri ama kupakiwa au kusafirishwa nje ya Tanzania au
kuchukuliwa na wenye shehena au mizigo husika, bandari za Tanzania ikiwamo
Bandari Kuu ya Dar es Salaam zimejipanga vilivyo kukabiliana na majanga
mbalimbali yakiwamo ya moto na uchafuzi wa mazingira.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kupitia idara yake ya
Zimamoto, Usalama, Afya na Mazingira kwa kila bandari, imejipanga kikamilifu
kuhakikisha usalama, afya na mazingira ya nchi kavu na mazingira ya majini,
vinasimamiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyowekwa.
Majukumu ya Zimamato, Usalama, Afya na Mazingira kwenye bandari
yanasimamiwa na kutekelezwa kwa mujibu wa sheria namba 17 ya 2004 ya TPA.
Sheria hii katika kipengele cha 12 (j), kinaitaka TPA kuhakikisha usalama wa
mizigo na wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira salama bandarini.
Pia, kwa mujibu wa kipengele cha 12 (h), TPA ina wajibu wa kuyazuia au
kukabiliana na majanga yoyote endapo yatatokea ndani ya maeneo ya bandari.
Maeneo ambayo bandari inayasimamia ni yale yaliyo ndani ya mipaka ya bandari
ambayo yapo katika nautical mile 12.
Pamoja na kufanya kazi kwa kufuata sheria za bandari, idara ya Zimamoto,
Usalama, Afya na Mazingira inafanya kazi kwa kufuata sheria za nchi. Sheria hizo
ni pamoja na Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, Sheria ya OSHA ya Mwaka
2003, Sheria ya Nguvu za Atomic ya Mwaka 2002 na Sheria ya Merchant
Shipping ya Mwaka 2003.
Sheria nyingine ambazo idara hii inazifuata ni ya Industrial and Consumer
Chemicals and Management Control ya mwaka 2003, pia inafanya kazi kwa
kufuata Sheria za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pamoja Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Kitengo cha Afya kilichopo
bandarini.
Pamoja na sheria hizo za nchi, idara hii inafanya kazi kwa kufuata miongozo ya
ndani ya nchi na za kimataifa. Kwa shughuli za majini inafuata miongozo ya
Shirika la Kimataifa la Bahari (IMO) ambalo ndilo linalotoa maelekezo na
miongozo ya shughuli za majini ambayo bandari inazifuata.
Kwa mfano, MARPOL 73/78 ni sheria inayotoa mwongozo wa kusimamia uchafuzi

wa bahari ambayo TPA kama taasisi ni lazima isimamie na kutekeleza. Sheria
nyingine ni SOLAS 78 ambayo inatoa mwongozo na usimamizi wa vyombo
vinavyofanya kazi baharini.
Kwa kuwa Bandari inahudumia mizigo mbalimbali ikiwamo mizigo hatarishi, kuna
miongozo ya namna ya kushughulikia na kuihudumia mizigo hatarishi. Idara ya
Zimamoto, Usalama, Afya na Mazingira ina wajibu wa kusimamia mizigo
inayobainika kuwa ni hatarishi kwa wafanyakazi, kuhakikisha mazingira ya
Bandari ni salama kwa kusimamia miongozo ya bandari na masharti
inayoandamana na miongozo hiyo.
Mizigo hatarishi imegawanyika katika madaraja tisa. Miongozo inayosimamia
mizigo hatarishi imetoa maelekezo kwa kila daraja namna ya kushughulikia au
kuhudumia mizigo hiyo. Miongozo hiyo imetolewa ili kuhakikisha kuna usalama
kwa wafanyakazi wetu na kulinda afya zao.
Katika utekelezaji wa sheria, miongozo na maelekezo ambayo yameainishwa,
kazi za kila siku za idara ni pamoja na kuzuia majanga ya moto yasitokee katika
maeneo ya Bandari. Kazi hiyo inafanyika kwa kufanya ukaguzi wa kiusalama wa
kuzuia na inapotokea kuna moto bandarini au katika meli zilizopo bandarini, idara
ya Zimamoto, Usalama, Afya na Mazingira ina wajibu wa kuuzima.
Majukumu makubwa ya idara hii ni kuhakikisha wafanyakazi wanaingia salama
kila siku bandarini na kutoka salama. Hilo linafanyika ili waendelee kufanya kazi
wakiwa na afya njema katika mazingira salama kwa lengo la kuhakikisha kazi
zinafanyika kwa ufanisi mkubwa ili kuongeza tija.
Pia idara ina wajibu wa kusimamia mizigo ambayo ni hatarishi kwa wafanyakazi
kwa kuhakikisha mazingira ya Bandari yapo salama kulingana na miongozo na
maelekezo ya sheria zilizopo. Usimamizi huo unafanyika kwa kusimamia
vihatarishi vinavyoweza kuwapo kwenye mizigo inayopita bandarini.
Mizigo hiyo hukaguliwa kwa kutumia vifaa maalumu kugundua kama kuna mzigo
wowote hatarishi au una kemikali hatarishi. Endapo mizigo ya namna hiyo
ikigundulika hutengwa katika sehemu maalumu kushughulikiwa inavyopaswa kwa
kushirikiana na taasisi husika.
Wafanyakazi wa TPA wanapohudumia mizigo mbalimbali kulingana na miongozo,
wanatakiwa kuvaa vifaa vya kinga (PPE) kama vile reflector, helmet, overall,
masks, boots. Umuhimu wa kuvaa vifaa kinga ni kuhakikisha mazingira ya
kufanyia kazi ni salama na rafiki.
Aidha, idara hii husimamia mazingira yote ya Bandari upande wa nchi kavu na
upande wa baharini. Kwa upande wa baharini kunaweza kukatokea uchafuzi
kama vile kumwagika kwa mafuta, na hilo likitokea idara inajipanga ili kusafisha.
Pia, idara inasimamia mazingira ndani ya Bandari kwa kushughulikia takataka
bandarini.
Kwa kuwa TPA inajenga na kuboresha miundombinu katika bandari zake kutoa
huduma bora kwa wateja wake, miradi yote huwa inafanyiwa tathmini ya
kimazingira. Idara ya Zimamoto, Usalama, Afya na Mazingira hushiriki michakato
yote na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Kazi nyingine ya idara hii ni kuzuia ajali bandarini kwani mfano Bandari ya Dar es
Salaam eneo ambalo lina mitambo mikubwa kulingana na shughuli zake, kila siku
kuna watu walau wafanyakazi na wateja zaidi ya 3,000 na vyombo vingi vya moto
vinaingia na kutoka. Katika hali kama hiyo ajali ni rahisi kutokea, kwa hiyo idara ya
Zimamoto, Usalama, Afya na Mazingira ina wajibu wa kutoa elimu, kuzuia ajali
zisitokee na endapo zitatokea kuzishughulikia kwa kushirikiana na taasisi
nyingine.
Kwa kuwa Bandari ni lango kuu la biashara, TPA ina wajibu wa kuhakikisha
bandari zote nchini ni salama kwa wafanyakazi ili waweze kufanya kazi katika
mazingira rafiki na salama kwa lengo la kufanya kazi kwa ufanisi. Pia TPA ina
wajibu kuweka mazingira ya bandari kuwa rafiki na salama kwa wateja wanaokuja
kuchukua mizigo au kusafirisha mizigo yao.
TPA kwa kumjali mteja ina kituo cha huduma kwa mteja ambacho kina simu
ambazo mteja anaweza kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi (SMS) bure kuuliza
swali lolote au kupata ufafanuzi juu ya meli na mizigo ya wateja bandarini kwa
saa 24. Namba hizo ni 0800110032 au 0800110047. Tuwasiliane.

987 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!