Wakati Rais John Magufuli, akijitahidi kubana matumizi, Manispaa ya Morogoro imejenga barabara ya lami yenye urefu wa Kilomita 4, kwa gharama ya Sh bilioni 12.

Gharama hiyo imevunja rekodi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami nchini, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umekuwa ukijenga kilomita moja ya tabaka la lami nzito kwa gharama ya Sh milioni 800-900. Kupaa kwa gharama hizo za ujenzi kumetajwa kuchochewa na baadhi ya watumishi wa halmshauri hiyo.

Maafisa wanaotuhumiwa kufanikisha mpango huo ni pamoja na Afisa Ununuzi na Ugavi Msaidizi wa Manispaa ya Morogoro, Meya wa Manispaa na Mkurugenzi wa Manispaa. Maafisa hao wanatuhumiwa kupokea hongo inayokadiriwa kufikia Sh milioni 240.

Viongozi hao wametuhumiwa na baadhi ya madiwani wa Manispaa ya Morogoro, wajumbe wa Kamati ya Fedha kuwa wamechukua kiasi hicho cha fedha kutoka kwa kampuni ya ujenzi ya Group Six International. Kampuni hiyo ina makao yake makuu jijini Dar es Salaam.

Kumekuwepo na tuhuma kwamba viongozi hao ‘wamelambishwa’ asilimia mbili ya gharama za mradi huo. Mradi wa ujenzi wa barabara za Tubuyu, Nanenane na Maelewano umegharimu Sh bilioni 12.6. Fedha za mradi huo zimetolewa na Benki ya Dunia.

Akizungumza na JAMHURI kwa sharti la kutokutajwa jina, mmoja wa madiwani ambaye pia ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango ya Manispaa hiyo, amesema baadhi viongozi wanatajwa kushawishi Manispaa iingie mkataba huo wa ujenzi bila kupatikana kwa Mshauri wa Mradi.

“Jambo hili limesababisha kazi isianze kwa wakati kama ilivyokuwa imekusudiwa, kutokana na kutokuwepo kwa Mshauri wa Mradi. Imechukua mwezi mmoja na nusu kumpata Mshauri wa Mradi ambaye ni Mhandisi Consultancy Ltd.

“Group Six amepewa kazi hii baada ya kukubaliana na Meya, Afisa Ugavi na Ununuzi na Mkurugenzi kwa makubaliano ya asilimia 2 ya Sh bilioni 12.6 za mradi huu,” amesema Diwani huyo.

JAMHURI limezungumza na Afisa Ununuzi Msaidizi Manispaa ya Morogoro, Albert Ngwada ambaye amekana tuhuma hizo.

“Hilo jambo si kweli. Mimi nafahamu wapo watu wanaojaribu kuharibu mambo. Mimi ninachokifahamu ni kwamba taratibu zote zilizingatiwa hadi Group Six kupewa kazi,” amesema Ngwada.

Alipoulizwa kwanini alishiriki kusaini mkataba wa kazi na kampuni hiyo, kabla ya Mtaalam Mshauri kupatikana, amejibu kuwa mambo hayo yote yalikwisha kamilishwa na Kamati ya Tathimini na Bodi ya Zabuni.

Ngwada anatuhumiwa na baadhi ya madiwani kujihusisha na vitendo vya rushwa kiasi cha kusababisha kandarasi nyingi katika Manispaa hiyo kufanyika chini ya kiwango.

Afisa Ununuzi na Ugavi, Ngwada, anatajwa kuwa na maslahi yake binafsi ya kujipatia fedha na washirika wake akiwemo Mkurugenzi na Meya wa halmashauri hiyo na anadaiwa kuwa amekuwa akiingilia zabuni zinazotangazwa na Manispaa kwa kuwapatia baadhi ya wakandarasi ‘Bills of Quantity’ (BOQ) za kazi zilizotangazwa.

JAMHURI limezungumza na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, John Mgalula, aliyesema hawezi kuzungumzia suala hilo kwani hayuko katika nafasi nzuri kutokana na kusubiri kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU).

“Takukuru wameniita kunihoji juu ya suala hili wiki ijayo (hii). Nitakukaribisha tuzungumze kwa undani juu ya ukweli wa suala hili ila kwa sasa naomba tusubiri kwanza mahojiano hayo.

“Na mimi naomba nikuhakikishie kuwa ukweli utafahamika. Sisi hatuwezi kufanya mambo ya ajabu kiasi hicho kuipa kazi kampuni isiyostahili. Hao (jina limehifadhiwa) waligushi nyaraka na mimi nitakuonesha nyaraka zote baada ya mahojiano na Takukuru,” amesema Mgalula.

JAMHURI limezungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Group Six, Johnson Huang, ambaye amekana kuhusika kwa namna na kutoa rushwa ili kupata zabuni hiyo.

“Taarifa hizo umezipata kutoka wapi? Nakuhakikishia kwamba si taarifa za kweli hata kidogo. Kampuni yangu haijatoa rushwa kupata kandarasi hiyo,” amesema Johnson.

Meya wa Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Pascal Kihanga, ameliambia JAMHURI, tuhuma zinazoelekezwa kwake hazina ukweli wowote.

“Mimi kama Meya sina mamlaka ya kuiondoa kampuni kwa sababu maamuzi yote yanafanyika kwenye Baraza. Sifanyi mimi peke yangu. Kamati husika ndiyo inatoa maamuzi.

“Hayo uliyoambiwa sio ya kweli, ukweli ni kwamba baada ya kuwaambia Siha warudi kurekebisha dosari zilizoonekana, kilichofuata washauri wakasema kuwa wamegundua… taarifa hiyo ilipewa Kamati ya Fedha,” amesema Kihanga.

Alipoulizwa kuhusu kugawa rushwa ya Sh milioni 2, kwa kila mjumbe wa Kamati ya Fedha, Kihanga amekana tuhuma hizo, huku akisisitiza kuwa mchakato huo kupitia kwenye mikono ya watu wengi wakiwemo Mkurugenzi wa Manispaa, Afisa Ununuzi na Mkuu wa Mkoa.

Akizungumza na JAMHURI, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Morogoro, Beutoz Mbwiga, kuhusiana na mradi huo wa barabara kuhusishwa na rushwa, amesema kuwa taarifa hizo ni mpya kwake na kuomba ushirikiano wa kupatiwa nyaraka zinazohusiana na suala hilo ili alifuatilie kwa ukaribu.

“Suala hili ni jipya kwangu. Sina uhakika nalo zaidi kwasababu miradi ipo mingi inayosubiri utekelezaji na mingine ipo katika utekelezaji. Naomba unipatie maelezo uliyopewa na vyanzo vyako ili niweze kusoma na kuelewa suala hilo kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria,” amesema Mbwiga.

JAMHURI limezungumza na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dk. John Ndunguru ambaye amekiri kuwepo kwa suala hilo huku akikataa kutoa ufafanuzi zaidi.

“Siwezi kusema kuhusiana na Timu ya Uchunguzi iliyoundwa kuchunguza hili suala, kwamba ina wajumbe wangapi na majukumu yake hata muda wa kazi niliyoipa ila naomba unitafute muda mwingine tulizungumze,” amesema Dk. Ndunguru.

Kazi hiyo ya ujenzi wa barabara za Tubuyu na Maelewano kwa kiwango cha lami nzito imepewa Kampuni ya Group Six kwa gharama ya Sh bilioni 11.530 bila VAT na ikiwa pamoja na VAT gharama ni Sh bilioni 12.630.

Katika barua ya Novemba 11, 2016 iliyoandikwa na Ngwada kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manipaa ya Morogoro kwenda kwa Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya Fedha, ambayo JAMHURI, limeiona inaeleza kwa urefu wa barabara.

Zabuni ya ujenzi wa barabara ya Tubuyu (2.4Km), Nanenane (1.6Km) na Maelewano (0.6Km) kwa kiwango cha lami iliyotangazwa Septemba 12, 2016 na kurudiwa Octoba 11, 2016 wazabuni wanne tu ndiyo waliwasilisha zabuni zao ndani ya muda uliokubaliwa.

Zabuni hizo ni Hari Singh & Sons Ltd ya Moshi kwa gharama ya Sh bilioni 13.810 bila VAT, Group Six International JV Lukolo Company Ltd ya Dar es Salaam kwa gharama ya Sh bilioni 12. 600 bila VAT, Siha Enterprises Ltd JV Msindavii Investment ya Dar es Salaam kwa gharama ya Sh bilioni 9.461 bila VAT na Jassie and Company Ltd ya Mwanza kwa Sh bilioni 11. 470 bila VAT.

Katika uchambuzi wa awali wazabuni wawili kati ya wanne walienguliwa kuendelea kwa madai ya kuwa na upungufu kadhaa. Wazabuni hao ni Jassie and Company Ltd na Hari Singh &Sons Ltd.

Katika barua hiyo Ngwada alieleza kuwa Jassie and Company Ltd iliondolewa kwa sababu kuu mbili ambazo ni kuwasilisha leseni ya biashara iliyokwisha muda wake na kuonesha utendaji hafifu wa kazi kwa kushindwa kukamilisha kazi aliyopewa awali kwa muda muafaka.

Wakati Mzabuni Hari Singh alienguliwa kwa kigezo cha kubadilisha ‘Bills of Quantity’ ya taa za barabarani.

Kwa vyovyote iwavyo, kiwango cha wastani wa Sh bilioni 3 kwa kilomita moja ya barabara ya lami ni kikubwa kupata kutokea katika historia ya ujenzi wa barabara za lami nchini.

By Jamhuri