BARACK OBAMA:

Rais wa Marekani wa tatu kuzuru Tanzania

Barack Obama anakuwa Rais wa Marekani wa tatu kuzuru Tanzania, ambayo imekuwa nchi ya kwanza kutembelewa na rais huyu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Rais wa Marekani wa kwanza kuzuru Tanzania ni Bill Clinton mwaka 2000, akifuatiwa na George W. Bush mwaka 2008.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, ajenda kuu ya ziara ya Rais Obama hapa nchini imejikita katika kuongeza msukumo wa kuboresha demokrasia, utawala bora, biashara, huduma za afya na uwekezaji.

 

JANA

Mara baada ya ndege aina ya Air Force One anayosafiria kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana saa 8:20 mchana, Rais Obama aliongozwa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete kuelekea Ikulu na kufungua barabara mpya upande wa mashariki mwa lango kuu.

 

Baadaye marais hao walisaini mikataba ya misaada, ushirikiano, uwekezaji na biashara baina ya nchi hizi mbili. Tukio lililofuata baada ya hapo lilikuwa la marais hao kukutana na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam.

 

Ratiba iliyofuata ilikuwa ya Rais Obama kukutana na maofisa watendaji wakuu wa kampuni mbalimbali na wafanyabiashara kutoka nchi za Afrika na Marekani katika Hoteli ya Hyatt Regency kabla ya kuzungumza na wafanyabiashara wa Tanzania pekee hotelini hapo.

 

Baadaye jana usiku Rais Kikwete alimkaribisha Rais Obama katika dhifa ya taifa kwa heshima yake iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

 

LEO

Ratiba inaonesha kuwa leo kuanzia saa 3:30 asubuhi, Rais Obama atatembelea ubalozi wa Marekani na kuzungumza na wafanyakazi wa ubalozi huo kabla ya Rais huyo na mke wake, Michelle, kuweka mashada ya maua katika jengo la zamani la ubalozi wa Marekani lililokumbwa na shambulio la kigaidi mwaka 1998 na kugharimu maisha ya watu 11 na wengine 80 kujeruhiwa.

 

Rais Obama atazuru pia eneo la Ubungo ilipo mitambo ya kufua umeme inayoendeshwa na Kampuni ya Symbion ya Marekani. Kisha saa 5:30 asubuhi atapanda ndege yake kuelekea Washington, Marekani, kupitia Dakar, Senegal ambako ndege hiyo itaongezewa mafuta.

 

Ziara ya Rais Obama, mke wake, Michelle na binti zao, Malia na Sasha katika Bara la Afrika ilianza Alhamisi iliyopita nchini Senegal, kisha Afrika Kusini na baadaye hapa Tanzania.