Ndugu akina mama na akina dada, nawasalimu kwa salamu za fedha ziletwazo na uchumi na ujasiriamali. Naamini barua hii itawafikia salama mkiwa mmesherehekea Pasaka kwa amani na mkiwa mmeanza robo ya pili ya mwaka kwa mafanikio.


 Si mara yangu ya kwanza kusema na wanawake kuhusu ujasiriamali, lakini ni mara yangu ya kwanza kuwaandikia barua maalumu. Nimeamua kuwaandikia kwa sababu ninawaamini sana wanawake linapokuja suala la ujasiriamali na biashara. Utaniuliza, ""Sanga umepata wapi imani hii?"


 Ohoo! Imani ya kuwakubali wanawake nimeipata kutoka kwa mama yangu mzazi ambae alikuwa ni mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa katika majira yake. Ndiyo maana kila niwaonapo wanawake, huwa naamini wanaweza zaidi ya wanavyojidhani. Licha ya kwamba nimewaandikia wanawake lakini natamani na kukusudia kuwa barua hii isomwe na watu wote, yaani wakiwamo kina kaka na akina baba wote. Hivyo nitazungumza katika mtindo wa ujumla.


 Ndugu zangu, katika zama hizi za ujasiriamali tunazoishi sasa kwa hakika hatuwezi kabisa kukuweka kando wewe mwanamke kutokana na nafasi yako katika jamii. Hili linatokana na vuguvugu la ukombozi wa mwanamke linaloendelea duniani pote, ambapo mwanamke unahitaji kuwa huru katika nyanja zote ikiwemo, kiuchumi, kijamii na kisiasa. Katika kuelekea ukombozi kamili wa kiuchumi, mazingira na hali zinamlazimisha mwanamke kuwajibika kikamilifu katika harakati za ujasiriamali.


 Ninapoongelea ujasiriamali kwa wanawake ninafahamu kuwa kutakuwa na ukinzani mkubwa kama sitatengenisha wanawake kwa makundi. Kwa uthubutu, kundi la kwanza ninawaweka wanawake ambao hawajaolewa na lile la pili ninaweka kundi la wanawake walioolewa.
 Mwingine ataniambia, wanawake wako sawa kwa nini uwatenganishe? Ninasukumwa kufanya hivi kwa sababu ninafahamu kuwa kundi la wanawake walioolewa uamuzi wao unafungwa na matakwa ya waume zao wakati kundi la wanawake ambao hawajaolewa lenyewe lipo huru zaidi.


 Nimesema wanawake wenye ndoa maamuzi yao yanadhibitiwa sana na wanaume, kwa kuwa kuna wanaume ambao wanawaunga mkono wake zao kufanya ujasiriamali lakini wapo wanaume ambao hawapo tayari kuruhusu wake zao kujishughulisha na ujasiriamali. Kwa hawa mbali na changamoto nyingi za kijasiriamali pia wanakumbana na dubwasha jingine, liitwalo ‘kunyanyaswa na waume zao’.


 Kiukweli asilimia kubwa ya wanaume wengi wana matatizo katika fikra zao, kutokana na namna wanavyouchukulia uwezo wa wanawake katika ujasiriamali. Wengi wanaona mwanamke kuwa mjasiriamali, atakuwa na kiburi, wanahisi atachukua nafasi yao katika familia na kubwa linalowaogopesha ni kudhani kuwa mwanamke mjasiriamali ni muhuni.


 Ujinga wa baadhi ya wanaume ni kudhani kuwa hulka hasi wanazokuwa nazo wao katika ujasiriamali, zipo pia kwa wanawake wajasiriamali. Upo ukweli kuwa baadhi ya wanaume wanapofanikiwa kiujasiriamali (na hata katika maeneo mengine) huwa na mtindo wa kuanza kiburi kwa wake zao, kusaliti ndoa zao na kusahau michango ya wake zao kwa hatua wanayokuwa wamefikia. Kutokana na hili, wanaume ni kama wanaogopa vivuli vyao wenyewe, katika kuwapa uhuru wake zao kujishughulisha kikamilifu na ujasiriamali.


 Dhana hii imepelekea wanaume wengi kuwanyanyasa wake zao wanaojishughulisha na ujasiriamali na hata kuwakatisha tamaa. Na hili linatokea sana pale ambapo, eidha mwanaume siyo mjasiriamali ama ikiwa wote ni wajasiriamali lakini wanafanya biashara tofauti. Inamhitaji mwanamke kujifunga kibwebwe ili kuendelea mbele.
 Mara nyingi sana inapofika hapo (manyanyaso kuzidi) wanawake wengi husalimu amri na kuuacha ujasiriamali. Ni wachache tu ambao huamua kujitoa katika ndoa na kujikita katika ujasiriamali. Ndio maana takwimu na uzoefu unaonesha kuwa idadi kubwa ya wanawake waliofanikiwa kiujasiriamali ama hawakuolewa kabisa au walitalikiana na waume zao ama wanavumilia kuishi katika ndoa zenye migogoro mikubwa sana.


 Kwa wale wanaume ambao wameoa na wanafanya ujasiriamali pamoja na wake zao nao bado wameendelea kuwa wagumu sana katika kuwashirikisha wake zao kikamilifu. Kama ni duka, mwanamke anabaki kuwa muuzaji tu, hajui ni wapi mali zinanunuliwa, hajui mfumo kamili wa mapato na matumizi tena hajui hata mipango na mikakati ya biashara.


 Wapo wanaume ambao huwa wanadiriki hata kuchukua mikopo katika mabenki kwa kutumia rasilimali za familia bila kuwashirikisha kabisa wake zao. Hili ni tatizo kubwa! Ndio maana idadi kubwa ya wajane wa wajasiriamali huwa hawafiki mbali kibiashara mara baada ya waume zao kufariki.
 Kwa wale ambao wanaendesha biashara katika mifumo rasmi, (kwa mfano makampuni) ni vema na tena ni njia rahisi ya kutoa kiwango unachodhani kinafaa cha ushiriki wa mke wako katika biashara zako. Kwa mfano, mke anaweza kuwa na asilimia fulani ya hisa katika kampuni. Hili litamuwezesha kuingia katika vikao vya bodi ya wakurugenzi pamoja na kushiriki katika mipango na maendeleo ya kampuni, hata kama anaendelea na kazi yake nyingine.


 Siku zote ninasukumwa kuamini kuwa suala la ukombozi wa mwanamke linahitaji sana kuhusisha ukombozi wa fikra za mwanaume, ili aweze (mwanamume) kuachia haki na uhuru wa mwanamke; alioushikilia kwa karne nenda rudi kupitia hiki kinachoitwa mfumo dume.
 Hata hivyo naomba niweke sawa msimamao wangu katika hili ya kuwa sikubaliani na “baadhi ya wanaharakati” wanaotaka mwanamke abebe majukumu ya mwanaume. Tumkomboe mwanamke lakini tusithubutu kubadilisha uumbaji wa Mungu.


 Ipo haja ya kuwekana sawa katika hili kwa sababu si busara kuona wanawake mkizikacha ndoa ama wakikataa kuingia katika ndoa, kwa sababu ya ujasiriamali. Ujasiriamali haupaswi kuwa kiwanda cha talaka, haupaswi kutengeneza waseja (wanawake wasiotaka kuolewa) na katu hutakiwi kuwa kapu linalotunza migogoro ya ndoa.
 Lakini tunapoongelea ujasiriamali kwa wanawake ni lazima ninyi wanawake na jamii kwa ujumla, kuachana na mtindo wa kuwa na mitizamo hafifu. Kuna fikra zimemea za kudhani kuwa wanawake wanatakiwa kufanya biashara ndogo ndogo, kama kuuza maandazi, kuuza mboga, kushona vitambaa na vibiashara vingine uchwara.


 Hayumkini hili ni tatizo lililopo hata katika fikra na mipango ya taasisi mbalimbali za fedha zinazotoa kile kiitwacho mikopo midogo midogo kwa wanawake. Taasisi hizi zimejizoesha kukopesha ‘vimikopo’ vya elfu hamsini, laki moja ikizidi sana laki tano! Ni vigumu wanawake kupiga hatua kiujasiriamali kama hawataaminiwa na kupewa mikopo zaidi ya hapo (mikubwa). Tukitaka mabadiliko hatuna budi kuwaamini wanawake.
 Wanawake wenyewe mnatakiwa kuachana na mawazo hayo ya kujikunyata na unyonge, bali waanze kufikiria kiupana (thinking in big picture). Ni wasaa wa wanawake kuibuka na mawazo makubwa ya kibiashara, kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa, kuanzisha makampuni pamoja na kucheza na fursa za biashara za kitaifa na kimataifa.


 Wanawake sasa muwatazame wanawake wenzenu wachache waliofanikiwa kiujasiriamali duniani na katika mazingira ya Tanzania, halafu muinuke na kuanza kutenda. Hakuna maana ya kuwa na visingizio, hakuna maana ya kukata tamaa tena haina maana ya kudhani kuwa mwanaume ana asilimia mia moja za uhuru wa mwanamke kiuchumi.


 Kama si kusimama peke yake kiujasiriamali basi mwanamke unatakiwa kushikana bega kwa bega na mume wako, ili thamani na mafanikio ya familia kupitia ujasiriamali yawe ni mchango wa nguvu, bidii na maarifa ya wanandoa wote kwa pamoja.
 Faida iliyopo kwa wanawake ni kuwa wana hulka ya uvumilivu na kujituma ambazo ni hulka muhimu sana katika ujasiriamali. Kwa ‘added advantage’ hii kwa nini wanawake wabaki nyuma?


 Haina ubishi kuwa wanawake mpo katika kipindi cha mpito katika kutokomeza mfumo wa kutoaminiwa. Kipindi hiki ni kigumu na kinahitaji kukilipia gharama ili kupata mafanikio likiwemo eneo hili la ujasiriamali. Ni kipindi cha mapambano, kutoka utumwa wa mwanamke kuwa, ‘mama wa nyumbani’, kuwa, ‘golikipa’ ‘kuwa tegemezi’ na kuwa ‘wa kuamuliwa hata kama ana kazi yake’ kuelekea katika uhuru wa kiuchumi.


 Wanawake msione taabu kukataliwa na jamii zao, msirudi nyuma kwa kuachwa ama kunyanyaswa na waume zenu na mvumilie kutukanwa na kusemwa vibaya na wanajamii ambao wanawaona wanawake wanaouendea mstari wa mafanikio kupitia ujasiriamali, kana kwamba ni wahuni.
 Ni lazima wanawake mjitahidi kushinda changamoto za kuhudumia familia, kukabiliana na vishawishi, kubaki wasafi kinidhamu, kimaadili na katika imani. Kwa kufanya hivyo, jamii itaendelea kushuhudia na kuyaheshimu mafanikio ya wanawake katika ujasiriamali nchini Tanzania na duniani kwa ujumla.
 Wanawake wajasiriamali wanastahili ushindi.
stepwiseexpert@gmail.com

2374 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!