Barua ya wazi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro

Ndugu Mhariri,

Naleta hoja hii ambayo inatuhusu sisi wananchi wa Wilaya ya Kilosa kupitia Umoja wa Wakulima wa Umwagiliaji Mvumi (UWAUMVU) kuhusu uharibifu wa Skimu ya Mvumi.

Skimu ya Mvumi iko katika Kijiji cha Mvumi, Kata ya Magole, Wilaya ya Kilosa, ilianzishwa mwaka 2002 na ina wanachama 298 huku eneo hilo likiwa na ukubwa wa ekari 720 zilizomo ndani ya mradi na nje kuna ekari zaidi ya 1,000 na kila mwananchi anamiliki eneo lake, umoja wetu ni kwenye miundombinu ya umwagiliaji tu.

Uwekezaji uliofanywa na serikali pamoja na wadau wake wa maendeleo kama JICA, Food Aid, Benki ya Dunia n.k ni zaidi ya Sh bilioni 2. Eneo letu la mradi liko katikati ya Mto Kisangata kwa upande wa kaskazini na Mto Wami kwa upande wa mashariki. Maji tunayotumia ni ya Mto Kisangata.

Tatizo letu kubwa tangu tuanze mradi huu ni wafugaji kuchungia mifugo yao na kuharibu miundombinu ya umwagiliaji. Wafugaji wanaotusumbua zaidi ni wale wanaotoka Parakuyo, Kata ya Kimamba na Mambegwa, Kata ya Msowero, Tarafa ya Magole, ambao wako ng’ambo ya mito hii miwili.

Hali ya skimu hii kwa miundombinu ni mbaya kutokana na wafugaji kuchungia mifugo yao ndani ya skimu kutoka nje ya kijiji kiasi kwamba wanabomoa matuta yanayokinga maji kwenye mashamba na mifereji ambayo serikali imefanya uwekezaji mkubwa sana.

Malalamiko yetu tumeyafikisha sehemu mbalimbali za mamlaka ya serikali wakiwemo viongozi wa kuteuliwa na kuchaguliwa kwa ngazi ya kitongoji, kijiji, kata, tarafa hadi wilayani lakini hakuna msaada wowote tulioupata zaidi ya kero hii kuendelea na hata Desemba 21, mwaka jana wafugaji wameingiza makundi ya ng’ombe katika eneo hilo.

Hivyo tumeona tuombe msaada kutoka kwako Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kuwa wilayani hakuna wa kutusaidia tangu Oktoba mwaka 2017 ambapo nilifika kwa OCD wa Kilosa kupeleka kilio changu kwa niaba ya wanachama wenzangu akanieleza niende kwa Katibu Tawala wa Wilaya kwani wao ndio wanahusika na operesheni ya kuwaondoa wafugaji wavamizi.

Nikafika kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilosa na kumweleza kuhusu hilo tatizo na kumpa ushauri kuwa kwa sababu hao wanatoka nje ya Kata ya Mvumi ni vema viongozi wa maeneo yao wazuie wafugaji kuingiza mifugo yao ndani ya skimu.

Pamoja na ushauri huo, akanijibu kwamba Kijiji cha Mvumi hakuna zizi la kuhifadhia mifugo inayokamatwa kama kijiji kitajenga yuko tayari kukamata mifugo hiyo.

Nikafuata ushauri huo na umoja kwa kushirikiana na Kijiji cha Mvumi tukajenga zizi hilo Novemba mwaka jana na taarifa tulimpa Katibu Tawala wa Wilaya kuwa zizi tayari tumelijenga, lakini hadi naandika barua hii hakuna chochote kilichofanyika huku fedha za umoja zimetumika bila faida yoyote.

Hivyo, kutokana na hatua tulizozichukua na hakuna msaada wowote ule na kinachoendelea ni mgogoro mkubwa kati ya wakulima na wafugaji, lakini sisi wakulima tumekuwa wavumilivu sana tukisubiri msaada wako mkuu wa mkoa, kwani ukimya wa viongozi wa wilaya umetusikitisha sana.

Pia kama eneo hilo limetengwa kwa ajili ya kuchungia mifugo watueleze, kwani hata ile kauli mbiu yetu ya “Umwagiliaji Kilimo cha Uhakika” kwa Skimu ya Mvumi haina maana tena.

Wako katika kilimo cha umwagiliaji,

Hamza D. Mbalale,

Mwenyekiti UWAUMVU.

1395 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons