Ndugu Rais, kama Mwenyezi Mungu alinijalia sauti inayosikika na wengi walio karibu na walio mbali ili niwasemee waja wake, basi namwomba Muumba wetu huyo huyo awajalie baraka viongozi wetu ili wasizifanye ngumu shingo zao, bali wabarikiwe na wautegee sikio ukulele huu niupigao kama mtu aliaye kutoka jangwani:  Watoweni katika hofu watu wa Mungu ili wapate kuishi kwa amani, furaha na ustawi katika nchi yao hii njema waliojaliwa na Mola wao!

Baba tutengenezee jukwaa la maridhiano kwa kuwa busara ni kupatana na kamwe siyo kupambana.

Imeandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu kuwa vita yoyote ni mbaya. Ni mbaya kwa aliyeshindwa na ni mbaya kwa aliyeshinda pia. Ni mbaya kwa aliyeshindwa kwa sababu huumizwa sana na kula hasara kubwa.

Lakini ni mbaya pia kwa aliyeshinda kwa sababu huandamwa na laana na visasi vya milele kwa maisha yake yote. Baba tutengenezee jukwaa la maridhiano kwa kuwa busara ni kupatana na kamwe siyo kupambana.

Ndugu Rais, majuzi asubuhi niliamua kuendesha mkweche wangu baada ya kuona umekaa muda mrefu kwa kukosa mafuta. Kuingia tu katika barabara kubwa ghafla mkweche ukazima bila kutoa taarifa. Nikamkumbuka rafiki yangu Kazadi. Aliniambia ukiwa na gari mbovu utakuwa fundi gari. Bila kujua niguse wapi, nilipouchokonoa mkweche wangu ukawaka. Jirani kuna kijana fundi gari wa siku nyingi anaitwa Kibiwi. Amejiajiri kama mjasiriamali kwa kufungua kigereji kisicho rasmi chini ya muarobaini.

Nikamkuta na vijana wenzake hawana gari hata moja la kutengeneza. Zamani magari yalikuwa yanajaa mpaka anakosa nafasi pa kuyaegesha. Baada ya matengenezo akaniambia ile sehemu ya mkweche wangu imeoza inahitaji kuchomewa. Kwa kuwa wao wameishiwa gesi, niende gereji nyingine. Nina kijana mwingine naye amejiajiri. Ana kigereji chake kisicho rasmi chini ya mzambarau. Hali niliyoikuta ilinitisha. Ilikuwa yapata saa tano asubuhi. Mwenyewe pamoja na vijana wenzake wametandika malapulapu wamelala usingizi. Hakuna hata gari moja la kutengeneza.

Nikakumbuka nilipotaka kupiga rangi ilinibidi ningoje kwa siku mbili ili magari yapungue nipate nafasi.

Hata hivyo, niliambiwa kuwa sehemu inayotakiwa kuchomewa haiwezi kuchomwa na moto wa gesi, bali kwa umeme. Kwa kuwa hawana umeme pale ikabidi nimwendee kijana wangu mwingine ana kigereji chake chini ya mwembe. Nikamkuta anachomea nondo za madirisha. Hana hata gari moja la kutengeneza. Akanichomea.

Baba, siyo kwamba magari mabovu ya kutengenezwa hayapo. Yapo mengi, lakini watu wameyaegesha uani. Maisha yamekaza. Matokeo yake maisha ya vijana wetu waliojiajiri katika fani mbalimbali kwao maisha yamekaza zaidi. Kwa macho ya nyama ukiniangalia baba, utaona kuwa nimepigika. Nimechoka! Lakini mimi niache. Baba wahurumie vijana wako. Vijana wa nchi hii wamepigika!  Mbaya zaidi hawajui msaada wao utatoka wapi.

Vijana shime, haya yana mwisho. Mmoja kaniambia, “Tunangoja ndege nyingine.” Sikumuelewa! Zogo lililoanzishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuitwa akahojiwe na kamati ya Bunge ni kwa faida ya nani? Baba huwezi na hili ukalikokotoa? Kusema haoni shilingi trilioni moja na nusu zimetumika wapi ndiyo kulitumbukie nyongo taifa?

Hakupaona, sasa angesemaje? Anayepaona zilipotumika si amuonyeshe yaishe?

Baba, Watanzania wanauliza huu mtifuano unaoendelea usio na faida yoyote kwa taifa wala kwa wananchi ni kati ya Spika na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali au ni kati ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Job Ndugai? Wanaumia kwa matumizi ya mabaya ya kodi zao. Mwingine kachomekea, “Huyu anafanya kazi ya mtu’’.

Wananchi wana haki ya kuambiwa kama kweli huu mjadala ulikuwa ni wa lazima. Mpaka sasa umeishatumia fedha kiasi gani? Tunakoelekea kubaya. Tutengenezee jukwaa la maridhiano kwa kuwa busara ni kupatana na kamwe siyo kupambana.

Hali hii ndiyo inayoamsha simanzi katika vifua vyetu na kuashiria kuwa tunaelekea katika majuto ya dhiki kuu! Furaha yetu inaanza kutupotea. Tukisha kuipoteza kabisa hatutaipata tena. Simanzi nzito itakapokuwa imeielemea mioyo yetu inaweza kutusukuma kumkufuru Muumba wetu kwa kutupatia fursa ya kuwa hivi tulivyo. Tufike mahali Watanzania wote katika ujumla wetu tukubaliane katika mambo makuu mawili. Kwanza, kuwa nchi hii ni ya Watanzania wote. Hakuna mwenye haki zaidi ya wengine.

Pili, kuwa wewe ndiye Rais wa nchi hii. Kwa utaratibu tuliojiwekea wenyewe kwa wadhifa ulionao wewe ndiye baba yetu wote hata tulioona jua miaka mingi kabla yako. Anayetaka ni hivi hivi. Asiyetaka ni hivi hivi. Wewe ndiye baba yetu. Tutengenezee jukwaa la maridhiano kwa kuwa busara ni kupatana na kamwe siyo kupambana.

Ndugu Rais, kuyakataa yote eti kwa kuwa tu yamesemwa na wazungu haiwezi kuwa sawasawa. Nchi yetu siyo kisiwa. Viongozi waliotangulia na wazee wa nchi hii waliomfahamu na kumheshimu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere bado wanaamini kuwa Nyerere hakuwa fisadi. Wanafanya utaratibu atangazwe kuwa mtakatifu. Makubaliano yake na dunia kuwa Stiegler’s Gorge uwe urithi wa walimwengu wote, ulitokana na uchaji wake kwa Mungu na hulka yake ya kuwatanguliza wengine katika mema.

Nyerere hakuwa mbinafsi. Nyerere hakuwa mroho wa fedha! Wanaoamini kuwa anaweza akatokea kiongozi mtakatifu kama Nyerere, mawazo yao yaheshimiwe. Lakini utakatifu wa mtu huonekana mwishoni, siyo anapoanza.

Dunia hivi sasa imefunikwa na wavu wa mitandao. Kila kitu kinaanikwa. Mema yetu na makubwa yote tuliyoifanyia nchi yetu sasa yanaanza kutambuliwa na ulimwengu. Kama kwa ubinadamu wetu kuna ovu tulilifanya nalo litatambuliwa pamoja na mema yetu. Dunia itatutukuza kwa mema yetu, lakini kama kuna ovu tulilitenda dunia itaugua juu yetu. Itaomboleza na kulaani. Nani anaweza kuihimili laana ya dunia?

Baba, hatuijui siku ya kufa kwetu, lakini wote tunajua tutakufa. Ni kifo cha namna gani kila mmoja wetu atakipitia – anajua Mungu peke yake.

Laiti tungejua ni kwa namna gani kifo chetu kitakavyokuwa yako mengi ambayo huenda tusingethubutu kuyatenda. Basi, tumwombe Mwenyezi Mungu atujalie mwisho mkamilifu! Baba tutengenezee jukwaa la maridhiano kwa kuwa busara ni kupatana na kamwe siyo kupambana.

Please follow and like us:
Pin Share