Tanzania imetenga maeneo kwa ajili ya kuhifadhi maliasili na urithi wa taifa kwa kuwa na maeneo yaliyohifadhiwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Wizara ya Maliasili na Utalii ndiyo iliyopewa mamlaka ya kusimamia maeneo yote yaliyohifadhiwa nchini yakiwa na sifa na hadhi tofauti tofauti. Kuna mapori ya akiba, misitu ya hifadhi, mapori tengefu, hifadhi za taifa, Mamlaka ya Ngorongoro na hifadhi za kihistoria.

Licha ya maeneo haya kuhifadhiwa kisheria, katika siku za hivi karibuni kumeibuka tatizo kubwa la baadhi ya wananchi kuyavamia na kuendesha shughuli za kibinadamu zikiwamo za ujenzi wa makazi ya kudumu, kukata miti, kilimo na ulishaji mifugo.

Hali hiyo imesababisha kuwapo kwa msukumo kutoka kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wa ardhi kutaka kuhaulishwa kwa maeneo yaliyohifadhiwa wakitaka kuyapunguza kwa ajili ya matumizi mengine yasiyo ya kiuhifadhi.

Uvamizi huu umesababisha uharibifu mkubwa kwenye maeneo hayo, hivyo kuongeza athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile kupungua kwa maji, ongezeko la mafuriko, ukame na mmomonyoko wa udongo.

Athari nyingine za uvamizi huo ni kupungua kwa malisho ya wanyamapori kulikosababisha wanyamapori wengi kuhama katika baadhi ya maeneo ya hifadhi, hivyo kuathiri shughuli za utalii.

Mabadiliko ya tabianchi yameathiri nchi kiikolojia, kiuchumi na kijamii kwa ujumla wake kwa kukausha maji ya kunywa na kilimo cha umwagiliaji, kuathiri uzalishaji umeme na kuongezeka kwa maradhi yanayoambukiza mifugo na binadamu.

Maeneo yaliyohifahiwa ni muhimu kiikolojia na manufaa makubwa ya maeneo hayo ni vyanzo vikuu vya maji kutokana na maji yanayozalishwa katika maeneo hayo kutumika nyumbani, kwenye kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji umeme, viwandani, ustawi wa wanyamapori, samaki na viumbe hai wengine kwa ujumla wao.

Kupitia vyanzo hivyo vya maji, maeneo yaliyohifadhiwa hujaza maji katika bahari na maziwa. Kwa mfano Mto Pangani maji yake huingia moja kwa moja Ziwa Jipe na Bwawa la Nyumba ya Mungu ambayo hutumiwa na maelfu ya wananchi kwa kilimo cha umwagiliaji na uvuvi.

Pamoja na faida zitokanazo na upatikanaji wa maji, hifadhi za misitu zina faida katika kunyonya hewa ukaa, hivyo kuchangia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Makadirio ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa misitu nchini inanyonya takriban tani milioni 17 za hewa ukaa.

Umuhimu wa maeneo yaliyohifadhiwa kiuchumi

Maeneo yaliyohifadhiwa huchangia katika uchumi wa nchi kutokana na shughuli za uzalishaji zinazofanyika katika maeneo hayo zikiwamo za utalii wa picha na uwindaji wa kitalii.

Sekta hii ndogo ya utalii imekuwa ikikua kwa kasi ya wastani wa asilimia 12 kati ya mwaka 2000 hadi 2012. Takwimu zinaonyesha kuwa katika mwaka 2013 jumla ya watalii 1,095,884 waliingia nchini na kutembelea vivutio mbalimbali ukiwamo Mlima Kilimanjaro. Matarajio ni kuona Tanzania inapokea watalii 2,000,000 ifikapo mwakani, yaani mwaka 2020.

Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 utalii pekee ulichangia takriban asilimia 17.2 ya pato la taifa na kwa miaka miwili – yaani 2014 na 2015 sekta hii ndogo ya utalii iliongoza kwa mapato ya fedha za kigeni ikilinganishwa na vyanzo vingine vikuu vilivyozoeleka kama vile madini, kilimo na mauzo ya bidhaa za viwandani.

Mbali na utalii, faida nyingine za uhifadhi zinatokana na uuzaji wa mazao ya misitu na nyuki nje ya nchi ambayo pia yanachangia moja kwa moja pato la taifa kwa asilimia 3.5.

Katika miaka hiyo miwili, mapato hayo yalifikia takriban asilimia 25 ya mapato yote ya fedha zote za kigeni zilizopatikana nchini; hivyo inaonyesha ni kwa jinsi gani sekta hiyo ilivyo muhimu na inavyotakiwa kulindwa kama mboni ya jicho.

Kutokana na juhudi makini za uhifadhi nchini, Tanzania imepata sifa kadhaa kutoka katika jumuiya ya kimataifa na hivi karibuni tumetajwa kuwa ni moja kati ya nchi tano katika Bara la Afrika zenye uwezekano wa juu kabisa wa kukua kwa sekta hii ya utalii.

Hata hivyo, kuna dalili katika miaka ya karibuni kuwa sifa hiyo inaanza kushuka kutokana na uharibifu wa kutisha wa maeneo ya hifadhi unaotokana na uvamizi wa maeneo ya hifadhi ambao umechangia kushuka kwa ubora wa vivutio vya asili nchini, hivyo kuathiri utalii kwa ujumla.

Maeneo yaliyohifadhiwa yanakabiliwa na ongezeko la uvamizi wa watu kukaa ndani ya maeneo hayo au kuingiza makundi makubwa ya mifugo. Mwenendo huo unaashiria kuwapo kwa hali ya juu kwa  migongano ya uhifadhi na sekta nyingine hususan makazi ya watu na mifugo.

Swali la kujiuliza ni je, hakuna ardhi ya kutosha au hakuna mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi au vyote ili kuchukua hatua muafaka za kushughulikia tatizo hilo kabla halijawa sugu? Ni vema kuangalia matumizi ya ardhi yetu kwa mapana yake, hasa shughuli za ufugaji kwa vile ndiyo yenye mgongano mkubwa na sekta ya uhifadhi.

Mlinganisho wa ng’ombe na eneo la malisho unahitajika kama sehemu ya kutathmini kwa kina chanzo cha mifugo hasa ng’ombe kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa.

Uharibifu unaosababishwa na uingizaji wa makundi ya mifugo ndani ya hifadhi ni mkubwa. Kuna mmomonyoko wa udongo, uharibifu wa vyanzo vya maji, uharibifu wa mimea na hata kuenea kwa magonjwa kati ya mifugo na wanyamapori.

Kwa mchanganuo huo wa faida za maeneo yaliyohifadhiwa na zile za ufugaji inaonyesha wazi kuwa hifadhi za maliasili ni sekta muhimu, pana na mtambuka na ndiyo msingi wa kuwapo kwa maendeleo ya sekta nyingine za kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, viwanda na ustawi wa binadamu na viumbe hai wengine.

Kwa maana nyingine, maliasili si sekta tegemezi, bali inahitaji kuimarishwa ili kuendelea kuwa mhimili wa kusaidia maendeleo ya sekta nyingine na uwepo wa uhai wa viumbe hai. Misitu ni roho ya uchumi wa nchi kwa sababu hakuna kitu cha maendeleo kinachoweza kufanyika bila kuhitaji malighafi zinazotokana na uhifadhi.

Hauwezi kuwa na viwanda bila kuhitaji umeme, malighafi na maji. Hauwezi kupata maji kama hauna misitu. Hauwezi kupata umeme kama hauna maji. Hauwezi kupata fedha za kigeni kama hauna wanyamapori. Hauwezi kuwa na wanyamapori kama hauna misitu.

Huruma ya Rais John Magufuli ya kumega maeneo ya hifadhi itazamwe kwa umakini mkubwa ili kutoathiri urithi huu tuliopewa na Mwenyezi Mungu. Dhambi ya kuua uhifadhi ni mbaya na athari zake ni kubwa mno.

0783847877

Please follow and like us:
Pin Share