Mheshimiwa Waziri Dk. Harrison Mwakyembe, tunayo heshima kuchukua nafasi hii kukujulisha kuwa matrekta haya unayoyaona yamekwishalima sana na sasa hayawezi kazi hiyo tena. Ukiyafukuza mjini ni wazi hayatakwenda kulima, maana mengi hayana uwezo tena wa kufanya kazi hiyo.

Nyingi kati ya haya hayana hydraulic system. Kila mmiliki ana historia ya kulima na trekta lake kabla hajalileta hapa kwa miaka kadhaa. Yale ambayo bado yana uwezo huo yanaondoka kila msimu ufikapo kwenda kulima na baada ya msimu kwisha yanarejea, maana ni hasara kubwa isiyo kifani kuweka trekta isubiri msimu mwingine bila kuipa kazi nyingine.

 

Mheshimiwa, watu wengi hawatapenda kununua trekta kama likimaliza linalazimika kupaki bila kufanya kazi mbadala.

 

Tunawaombeni sana viongozi mliopo madarakani mtuongoze na kutuhurumia. Ombi letu kwako uturuhusu kufanya kazi hiyo maana hatuendi maeneo mengi ya jiji, vile vile tupo tayari kulipa Road Licence, Mapato, SUMATRA na Bima.

 

Bima hii tulikuwa tunalipa kitambo. Bila huruma kutoka kwako tutaathirika sisi na wategemezi wetu mpaka wazazi kijijini ambao ni wapigakura, tusisahau hilo.

 

Mheshimiwa, wengine wakila mkate na chai ya maziwa wengine basi waachwe wapate muhogo na chai. Mtu akila hata huo muhogo atakata tamaa ya maisha na kuingia katika mambo yasiyofaa.

 

Tunakuomba utupende sisi tunaojihangaisha, maana Serikali haina kazi za kutupa sote, hivyo wengine tumetawanyika katika kazi nyingine. Tunaomba utuhurumie, tunafanya kazi zetu kwa usalama wala hatuharibu uchumi wa nchi.

 

Tungeshukuru sana kama wenzetu mliopo ofisini mtazingatia shida tunazopata wajasiriamali maana ni vikwazo kila kukicha, ndiyo maana uchumi wa nchi unakua, lakini kwa wananchi wa kawaida ufukara unaongezeka.

 

Mheshimiwa, matrekta mengi yenye uwezo huondoka Oktoba kwenda kulima na kurudi Januari na Februari kuendelea na kazi hizi mbadala. Bila hivyo trekta ni mzigo na ni kitu kisichofaa kununua. Kulima ni jambo la muda mfupi sana. Tumelima sana mheshimiwa na matrekta hayo unayoyaona.

 

Sisi tunamalizia hapa mheshimiwa. Tunaweza kusema sana wala isisaidie kitu na tunaweza kusema kidogo ikasaidia, na wala kusema sana  siyo kufundisha.

 

Tunaandika tukiwa na matumaini.

Tunatanguliza shukrani.

 

Ni sisi,

matrekta@gmail.com

 

1163 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!