BARUA ZA WASOMAJi

 

Barua ya wazi kwa Waziri wa Maji

Mheshimiwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, hongera kwa kazi, siwezi kukupa pole kwani kazi ni wajibu na kipimo cha mtu.

Mheshimiwa Waziri, mimi ni mkazi wa kata ya Kyanyari, Wilaya ya Butiama mkoani Mara na ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Butiama kutoka Kata ya Kyanyari.

 

Naandika barua hii kwako kwa uchungu mkubwa, wakazi wa kata ya Kyanyari hulazimika kutembea umbali wa kilomita zaidi ya 20 kutafuta maji katika kata ya Kukirango, hasa katika kijiji cha Kiabakari, kitongoji cha Busaraga.

 

Mheshimiwa Waziri, kata ya Kyanyari iko umbali wa kilomita 20 kutoka Kiabakari lakini maji yanatoka Mugango mpaka Kiabakari, Butiama umbali wa kilomita zaidi ya 100. Tunauliza sisi Kyanyari tumekosa nini wakati tuko karibu au umbali wa kilomita 20 kutoka JWTZ Kiabakari ambao wao wana maji ya bomba. Kata ya Kyanyari inaundwa na vijiji vitatu: Nyamikoma, Mwibagi na Nyakiswa.

 

Mheshimiwa Waziri, tunakuomba hata hizo fedha ulizotiliana saini na Benki ya Kiarabu tarehe 19/06/2013 (BADEA) kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya maji Kiabakari, Mugango na Butiama ungeangalia pia hata hata ya Kyanyari katika vijiji vya Nyamikoma, Mwibagi na Nyakiswa kwani haviko mbali na Kukirango (Kiabakari).

 

Mheshimiwa Waziri wa Maji nakutakia kazi njema, ila nikiwa kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), naumia ninapoona mama zetu wakitembea umbali mrefu kutafuta maji wakati tumepewa dhamana ya kusimamia ni aibu tuchukue hatua.

 

Ahsante.


Mgingi Mhochi

S.L.P. 1384

Musoma

0759 278 509/0782 245 429