Baada ya Gazeti la JAMHURI kuchapisha habari ya kwanza kwenye toleo Na. 371 ikionyesha jinsi Benki ya BOA inavyoibia wateja nchini kwa maofisa wake kughushi nyaraka za wateja na kujipatia mikopo, sasa yameibuka mambo ya kutisha, JAMHURI linaripoti.

Wamejitokeza wateja zaidi ya 50 wanaolalamika kuibiwa na maofisa wa BOA kwa nyakati tofauti, kwa utaratibu ule ule wa nyaraka zao kughushiwa na kuonekana wamechukua mkopo wakati hawajachukua.

“Mungu ndiye atawalipa ninyi watu wa JAMHURI. Mimi kwa umri wangu huu unavyoniona (anasema mama mwenye umri wa miaka 58), najuta kuchukua mkopo kutoka BOA. Nimelipa nimemaliza, lakini kila nikienda wanirejeshee hati yangu, naambiwa njoo kesho, njoo keshokutwa, ni miezi tisa sasa.

“Lakini kilichoniuma zaidi, ameniambia mtu mmoja anayefanya kazi ndani ya benki hiyo kuwa hati yangu imetumiwa kukopa fedha nyingine, kwa jina la mtu mwingine anayeonekana nimemdhamini mimi wakati sijawahi kumdhamini mtu yeyote wa aina hii. Naomba Benki Kuu iwachunguze hawa BOA, ni lazima wanirejeshee hati yangu. Sitaki kufanya nao biashara tena,” amesema mama huyo.

Ukiacha watu wanaojitokeza kudai kuwa wametapeliwa na BOA, kuna taarifa za kutisha juu ya malipo yaliyodaiwa kufanywa kutokana na uuzaji wa nyumba tano za Jimmy Mwalugelo eneo la Ukonga, Stakishari kwa jinsi yalivyofanyika.

“Kwa kawaida sisi kama mteja anakuwa ameshindwa kulipa deni lake, inapofika wakati wa kuuza mali iliyowekwa kama dhamana ya mkopo, basi tunaamini tayari kunakuwapo mgogoro kati ya mteja na benki, hivyo fedha zote zinazouzwa kama ni kwenye mnada au vinginevyo zinapelekwa moja kwa moja kwenye akaunti maalumu ya benki ya kukusanya madeni, na si vinginevyo. Ndivyo utaratibu ulivyo kwa benki zote, lakini hapa BOA, lohooo! Nisiseme mengi,” ofisa mmoja wa BOA ameliambia JAMHURI.

Kuonyesha kwamba kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika uuzaji wa nyumba hizo zilizokuwa katika kiwanja chenye hati Na. 55709, Benki ya BOA haikuwasilisha fedha za mauzo mahakamani kama kielelezo kwa kuwa walikuwa wanaendesha shughuli hiyo kinyume cha sheria. Walimtaka mnunuzi kuweka fedha hizo katika akaunti Na. 01509670009, ambayo ni ya mtu anayedaiwa kushindwa kulipa mikopo hiyo, Rose Asea.

Cha kushangaza Februari 15, mwaka jana Benki ya BOA ilidai kuwa imemuuzia Yusufu Omary nyumba hizo, ila aliponunua hizo nyumba kwa mara ya kwanza alilipa Sh milioni 25 katika akaunti ya Asea aliyekuwa amekopeshwa na BOA Sh milioni 500 akashindwa kulipa, ikiwa ni asilimia 25 ya malipo ya awali.

Februari 28, mwaka jana alilipa tena Sh milioni 75 kwenye akaunti hiyo hiyo ya Rose Asea iliyoko katika Benki ya BOA, ikiwa ni asilimia 75 ya awamu ya pili ya malipo ya nyumba hizo.

Novemba 6, mwaka huu JAMHURI lilitaka kuthibitishiwa na BOA kama inazitambua nakala hizo za malipo yaliyolipwa kupitia akaunti ya Asea iliyoko katika benki hiyo badala ya kulipwa kupitia akaunti maalumu ya kukusanyia madeni.

Pamoja na BOA kupokea barua ya JAMHURI yenye kumbukumbu namba JML/ADM/PRM/2018/013 iliyotaka kuthibitishiwa uhalali wa nakala za malipo kutoka kwa mnunuzi wa nyumba hizo, hadi tunakwenda mitamboni hawakuleta majibu.

Mnunuzi wa nyumba hizo, Omary, amelithibitishia JAMHURI kuwa nakala hizo za malipo ni halisi, kwani  alielekezwa na BOA kulipa kupitia akaunti hiyo ya Asea na kwamba yeye alikuwa mshindi wa pili wa mnada wa kuuza nyumba za Mwalugelo.

Omary amesema hamkumbuki mshindi wa kwanza wa mnada huo, wala kampuni iliyokuwa imeendesha mnada. Mwalugelo ameeleza kuwa hajawahi kusikia tangazo lolote la kupiga mnada nyumba zake.

Tatizo lilivyoanza

Aprili, 2011 Mwalugelo akiwa mteja wa muda mrefu wa BOA alikwenda kuomba mkopo wa Sh milioni 100 katika benki hiyo, Tawi la Kariakoo, lakini akaelezwa kuwa lazima ufanyike utaratibu wa kukagua nyumba anayotaka kuweka kama dhamana ya mkopo huo.

Amesema Meneja wa Mikopo wa benki hiyo Tawi la Kariakoo alimwelekeza kuwa anapaswa kuleta nakala ya hati ya nyumba wamtume mthamini wao kwa ajili ya kujiridhisha kama inakidhi masharti ya mkopo au la. Naye aliwakabidhi vivuli vya hati.

Amesema baada ya wiki tatu walimweleza kuwa eneo lake linatosha kupewa mkopo unaoanzia Sh milioni 100 hadi 180, lakini aliwajibu kuwa hitaji lake ni Sh milioni 100 tu.

“Wakaniambia maombi yangu ya mkopo wanayapeleka makao makuu ya benki hiyo na baada ya mwezi mmoja wakasema mkopo umepita, hivyo nipeleke akaunti yangu, kikonyo cha kitabu cha hundi (check reference book) na hati ya nyumba.

“Niliwapelekea vielelezo hivyo nao wakanipa jibu kuwa tayari wameniingizia fedha hizo, lakini wakataka kwanza niwaandikie wao hundi ya Sh milioni 24. Nikawauliza hiyo hela ya nini? Wakanieleza kuwa Sh milioni 20 ni mgawo wa maofisa wa benki hiyo makao makuu walioidhinisha mkopo huo, Sh milioni 2 atapewa mthamini na Sh milioni 2 nyingine zitakuwa ni bima ya mkopo.

“Nikawaeleza kuwa siwezi kutoa fedha hizo kwa kuwa nitakuwa nalipa Sh milioni 40 ambazo sijazifanyia kazi yoyote, nikawataka wanirudishie hati yangu (kivuli) na kikonyo cha kitabu cha hundi. Sikuchukua mkopo wao, hakuna wanachonidai, lakini kilichonishangaza Novemba, 2016 nikapata taarifa kutoka kwa mjumbe kuwa nyumba yangu inapigwa mnada na BOA kwa kuwa ilitumika kama dhamana kwa mkopo wa mtu (Asea).

“Simfahamu mtu huyo, wala sijawahi kumdhamini kwa kutumia hati yangu. Nikaelezwa na madalali wa benki hiyo kutoka Kampuni ya Mabunda Auctioneers Mart Ltd kwamba nionane na Mkurugenzi wa Mikopo wa BOA, Joseph Bakari kwa ajili ya ufafanuzi,” amesema.

Mazingira ya mkopo

Mazingira hayo yalimfanya Unosye Mwalugelo (mke wa Mwalugelo) afungue kesi Na. 441 ya mwaka 2016 dhidi ya Rose Miago Asea, Bank Of Africa (T) LTD na Mabunda Auctioneer Mart Co. LTD. Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, C. A. Kiyoja, alitoa zuio la muda (Interim Order) kwa wadaiwa kushikilia na kuuza nyumba katika kiwanja Na. 671/1, 682/1, 698/1, Block ‘C’ Ukonga, eneo la Stakishari Desemba 16, 2016.

Hata hivyo, wakati kuna zuio la Mahakama, Machi 22, mwaka jana Benki ya BOA waliuza viwanja hivyo kwa Yusuf Omary na kubadilisha umiliki. Mei 22, mwaka jana kesi aliyofungua Unosye ilitupwa kwa madai kuwa mlalamikaji alichelewa kufika mahakamani.

Baada ya kutupwa kwa kesi hiyo, Jimmy Mwalugelo alifungua kesi Na. 152 ya 2017 katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala dhidi ya Rose Asea, Bank Of Africa (T) LTD na Mabunda Auctioneers Mart Co. Ltd akiiomba mahakama itoe amri ya upande mmoja (Ex-Parte Drawn Order) baada amri ya kwanza iliyowazuia mdaiwa wa 2 na 3 kushikilia na kuuza nyumba za mlalamikaji zilizopo katika viwanja namba 660/1, 662/1, 696/1 na 698/1, Block ‘C’ eneo la Ukonga Stakishari hadi shauri la msingi litakaposikilizwa.

Juni 2, 2017, mahakama ilitoa amri nyingine ya kuwazui mdaiwa wa 2 na 3 kushikilia na kuuza nyumba hizo ambayo ilikuwa inafikia kikomo Septemba 3, mwaka jana, lakini walalamikiwa tayari walikuwa wameuza nyumba za Mwalugelo. Julai 28, mwaka jana hati ya Mwalugelo ilibadilikishwa na kuwa mali ya Yusuf Omary.

Mwalugelo amelieleza JAMHURI kuwa kutokana na nguvu asiyojua BOA wanaipata wapi, hakuna kesi yoyote aliyoifungua yeye au mkewe iliyowahi kusikilizwa na mahakama zaidi ya mahakama kutoa amri dhidi ya walalamikiwa na kupuuzwa. Kesi ya msingi iliyokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala iliondolewa na mlalamikaji baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa mahakimu akaihamishia Mahakama Kuu na kusajiliwa kwa Na. 701 ya 2017.

Katika kesi hiyo BOA walibanwa mahakamani. Walimweleza Jaji Moses Mzuna wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa walikwishauza nyumba hizo kwa Yusuf Omary, hivyo mlalamikaji alitakiwa kufungua kesi upya akimwongeza mnunuzi wa nyumba hizo kama miongoni mwa wadaiwa.

Mlalamikaji alifungua kesi upya Mahakama Kuu liliyopewa Na. 802 ya 2017 iliyomuunganisha mnunuzi wa nyumba hizo kama mdaiwa wa nne. Hata hivyo, wakati shauri bado halijasikilizwa Benki ya BOA walibomoa nyumba zote tano likiwemo Kanisa la Moravian zilizokuwepo katika viwanja vyenye nakala ya hati ililiyokuwa benki na Jaji Mzuna alieleza kuudhiwa na kitendo hicho.

Akitoa uamuzi Oktoba 18, mwaka jana, Jaji Mzuna alisema mahakama haikutoa baraka zozote kwa walalamikiwa kujichukulia uamuzi na kupoteza hadhi ya utendaji wa mahakama. Alisema nyumba hizo ndizo zlikuwa zinalalamikiwa hivyo BOA walipaswa kusubiri uamuzi wa mahakama kabla ya kufanya jambo lolote hata kama hakukuwapo amri ya zuio kwa kuwa kesi ilikuwa inaendelea mahakamani.

Nyumba zavunjwa

Wakati kwa kawaida mkopaji akishindwa kulipa deni nyumba huwa zinauzwa, kwa Mwalugelo imekuwa tofauti. Nyumba tano likiwemo Kanisa la Moravian zilizokuwa katika kiwanja kinachodaiwa kuwa hati yake ilitumika kama dhamana zimebomolewa na mabaunsa wa Kampuni ya Udalali ya Mabunda kwa kushirikiana na BOA, Oktoba 17, mwaka jana, majira ya saa 10 alfajiri. Nyumba hizo zilikuwa na wapangaji 12 wakiwemo watoto wa Mwalugelo na vitu vyote vilivyokuwemo katika nyumba hizo viliibwa na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni 3.

Baada ya ubomoaji wa nyumba hizo, alifungua tena shauri Na. 940 ya 2017 akijumuisha gharama za mali na wapangaji 12, lakini shauri hilo pia lilitupiliwa mbali na Jaji Mzuna kwa kutaka kesi ya msingi iendelee na gharama zote za mali zilizoharibiwa zitafuata baadaye. Hadi sasa hakuna kesi iliyosikilizwa.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI unaonyesha kuwa maofisa wa benki hiyo walitumia vivuli vya hati hiyo kumkopesha Assea mkopo wa Sh milioni 100 mwaka 2011, Sh milioni 200 mwaka 2014 na Sh milioni 200 mwaka 2015 wakati mmiliki wa hati hiyo akiwa hafahamu kinachoendelea. Hii ilikuwa baada ya kuwakatalia baadhi ya maofsia wa BOA rushwa ya Sh milioni 24.

BOA watishia kufungua kesi

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Brela kupitia Kampuni ya B & E AKO Law, imeliandikia barua Gazeti la JAMHURI ikilitaka liache kuchapisha habari zinazohusiana na BOA na kwamba gazeti lijitathmini na kupeleka mapendekezo linataka kuilipa BOA shilingi ngapi kama fidia kwa hasara na usumbufu walioupata kutoka kwa wateja wao kutokana na kuchapishwa kwa habari za BOA kuibia wateja wake.

Pamoja na kwamba kwa miezi miwili BOA waliandikiwa maswali na gazeti hili wakawa hawajibu, kupitia kwa kampuni hii ya kisheria wamekiri kupata barua ya Nov. 6, 2018. Taarifa ambazo JAMHURI limezipata zinaonyesha kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tayari imeanza kuichunguza BOA katika mgogoro huu wa aina yake unaotishia usalama wa fedha za wateja. Je, wewe ni mmoja wa watu au ndugu yako amepata kuumizwa na BOA? Tuma ujumbe wako au piga simu Na. 0784 404827 usaidiwe.

3148 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!