Rais John Magufuli katika kipindi chake cha uongozi cha miaka mitatu amefanya mengi ambayo hata wakosoaji wake wanakiri kuwa ni ya kupigiwa mfano.

Kwenye toleo hili maalumu, tumeorodhesha baadhi ya mambo hayo yakilenga kuonyesha mafanikio makubwa katika kuimarisha nidhamu, uadilifu na uwajibikaji ndani ya utumishi wa umma na kukemea uzembe na kujenga ari ya kufanya kazi.

Amefanikisha ununuzi wa meli katika maziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria; amefufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuimarisha usafiri wa anga na kukuza sekta za utalii, afya, kilimo na kujenga reli ya kiwango cha kimataifa (SGR).

Kwenye utalii, kuna ongezeko kubwa la watalii na mapato. Kwa mfano, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa mwaka huu ulioishia Juni 30, 2018 imeongeza mapato kutoka Sh bilioni 60 hadi Sh bilioni 127.

Rais Magufuli, amehakikisha taasisi nyeti kama Bandari zinafanya kazi kwa saa 24. Amehakikisha wizi na ufisadi vilivyokuwa vimeshamiri Bandari sasa vinatoweka.

Ujenzi wa barabara na madaraja unaendelea nchini kote, ukilenga kuiunganisha nchi na kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi. Pia ajali za barabarani, hasa kwa mabasi ya abiria zimepungua, hivyo kupunguza vilio na ulemavu kwa wasafiri.

Mafanikio mengine ni kuendesha vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwenye taasisi za umma, sambamba na kuanzisha mahakama ya mafisadi na kuimarisha ulinzi wa rasilimali za nchi, ikiwamo madini na maliasili.

Mengine ni kujenga vyanzo vipya vya umeme, kikiwamo chanzo cha kuzalisha umeme wa maji megawati 2,100 katika bonde la Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge); kusambaza umeme hadi vijijini na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya awamu ya tatu ya mpango wa REA, na ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania).

Rais Magufuli pia ameimarisha huduma za afya, hasa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya na ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za wilaya na utoaji wa elimu msingi (shule za msingi na sekondari) bila malipo.

Vilevile amehakikisha miradi yote ya maji inayotekelezwa inakuwa bora, yenye uwiano na thamani halisi ya fedha na kukamilishwa kwa wakati na kuimarisha kilimo, ushirika na bei za mazao ya biashara. Mfano wa karibuni kabisa ni wa kuhakikisha wakulima wa korosho wanafaidi jasho lao kwa haki.

Mpango alionao Rais Magufuli sasa ni kuiwezesha nchi kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya kuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.

Soma zaidi taarifa za mafanikio ya Rais Magufuli kwa miaka mitatu ndani ya toleo hili.

Please follow and like us:
Pin Share