Home Kitaifa Benki Kuu yaja na kanuni mpya Dawati la Malalamiko

Benki Kuu yaja na kanuni mpya Dawati la Malalamiko

by Jamhuri

ARUSHA

NA ZULFA MFINANGA

Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  imesema imo katika mchakato mahususi wa kupanua Dawati la Malalamiko na kuongeza wigo wa kutoa huduma kwa watoa huduma wote za kifedha, tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo linapokea malalamiko ya kibenki pekee.

Akizungumza katika semina ya waandishi wa habari za Fedha na Uchumi jijini Arusha, Meneja Msaidizi wa dawati hilo, Ganga Mlipano, amesema licha ya kuwa dawati hilo limesaidia kutatua kero mbalimbali za wateja nchini, lakini kanuni zilizopo zinawalenga wateja wa benki pekee wenye amana isiyozidi Sh milioni 15, huku pia ikichukua muda mrefu (zaidi ya siku mia moja) mtu kuhudumiwa.

Amesema Sheria mpya zilizopitishwa hivi karibuni (The Microfinance Act 2018, The Microfinance Regulations, 2019, The Bank of Tanzania Financial Customer Regulations, 2019) zitawajumuisha watoa huduma za kifedha wote kama vile maduka ya fedha za kigeni, benki, kampuni, SACCOS na VICOBA pamoja na mwananchi mmoja mmoja bila kujali viwango vya fedha walivyo navyo.

“Kanuni za sasa zinamlenga mteja wa benki pekee na zinasema iwapo mteja hajaridhika na huduma, kwanza anatakiwa atoe malalamiko yake katika benki husika, iwapo hajatatuliwa kero yake ndani ya siku 21 ndipo anaruhusiwa kuja kwetu, ambapo kabla ya yote tutaangalia kama madai yake yamo ndani ya muda, kwa maana kwamba hayana zaidi ya miaka miwili, pia hayapo na wala hayajawahi kwenda mahakamani,” anasema na kuongeza:

“Ndani ya siku mbili tutamjibu mteja kwa barua kuwa tumepokea malalamiko yake na ndani ya muda wa siku nne tutakuwa tumeshamtumia mlalamikiwa notisi na tutamtaka kujibu ndani ya siku kumi, ambapo tutawaita wote wawili kuwasikiliza na baada ya siku 90 tutatoa hukumu, hapo mmeona ni jinsi gani mteja anatumia muda mrefu kusubiri majibu.”

Amesema kanuni mpya imeainisha aina ya malalamiko na muda utakaotumika kuyatatua baada ya kuona kuna baadhi ya malalamiko yanahitaji utatuzi wa haraka, lengo ni kuendelea kujenga imani kwa wananchi pamoja na taasisi za kifedha.

Amesema tangu dawati hilo lianzishwe mwezi Aprili, 2015, jumla ya malalamiko 496 yamepokewa ambapo mengi yanahusiana na huduma za kutolea fedha kwa njia ya mashine (ATM), mikopo na mikataba pamoja na kuchelewa au kutokurudishwa kwa hati au kadi za magari ambapo asilimia 40 yalitatuliwa kwa maelewano.

Amesema licha ya mafanikio hayo bado watu wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu dawati hilo na kwamba malalamiko kutoka mikoani ni machache ikilinganishwa na Mkoa wa Dar es Salaam ambao unaongoza kwa kutoa malalamiko kwa asilimia 90.

Awali, akifungua semina hiyo, Gavana Mkazi wa Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Arusha, Charles Yamo, amewataka waandishi wa habari kujiendeleza kielimu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuhakikisha wanakuwa wabobezi kwenye eneo moja ili kufanya kazi kwa ufanisi.

“Huwezi kuwa mwandishi mzuri kama hautakuwa umebobea kwenye eneo moja maalumu, msiwe waandishi wa kuandika kila kitu, leo unaandika hiki, kesho kile, mtondogoo kingine, ni vema mkajiendeleza kielimu, kwani dunia inakwenda kasi sana kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano,” anasema Gavana Yamo.

You may also like