Benki yahukumiwa kwa kumwibia mteja

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara imeiamuru EcobankTanzania Limited kumlipa mteja wake zaidi ya Sh milioni 100 baada ya kukutwa na hatia ya ‘kukwapua’ takriban Sh milioni 66 kutoka kwenye akaunti yake.

Hukumu iliyosomwa Agosti 13, mwaka huu na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Zepharine Galeba, imetupilia mbali hoja tano zilizofunguliwa na wakili wa mrufani, Mpaya Kamara.

Ecobank inadaiwa kuiibia zaidi ya Sh milioni 66.2 Kampuni ya Future Trading Limited, zilizokuwa kwenye akaunti yake kupitia huduma ya ‘internet banking’ na kuziingiza katika akaunti ya Bashir K. General Dealers CC ya Afrika Kusini.

Jaji Galeba amesoma hukumu hiyo kwa niaba ya majaji wenzake wa Mahakama ya Rufaa; Rehema Mkuye na Ferdinand Wambali.

Awali, katika hukumu ya kesi ya msingi namba 68 ya mwaka 2014 iliyoripotiwa na Gazeti la JAMHURI katika toleo la Aprili, 2019, Jaji Barke Sehel, aliipa ushindi Kampuni ya Future Trading Limited kabla ya Ecobank kukata rufaa.

Wizi huo ulifanyika Ecobank, Tawi la Uhuru jijini Dar es Salaam, katika akaunti Na. 0010135400019801 ya Future Trading Limited.

Jaji Galeba amesema: “Mrufani alileta hoja nne kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kabla ya baadaye kuongeza hoja nyingine.”

Hoja ya kwanza iliyowasilishwa na Wakili wa Ecobank, Kamara, ni kwamba jaji wa Mahakama Kuu alikosea kisheria na katika ukweli kwamba mjibu rufaa hakuwahi kuomba huduma ya benki mtandao.

Pili, jaji huyo hakujali ukweli kwamba Mkurugenzi Mtendaji wa Future Trading Limited, Abubakar Suwed, alipokea ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kupitia simu yake ya kiganjani ukimtaarifu kuhamishwa kwa fedha kutoka kwenye akaunti yake kwenda Afrika Kusini.

Tatu, ni kwamba jaji alikosea kukubali kwamba miamala ilifanywa bila idhini (kuwa na taarifa) ya mjibu rufani na nne pamoja na ushahidi mzito uliotolewa, bado jaji alitoa hukumu dhidi ya Ecobank.

Kisha baadaye Kamara akaongeza hoja kwamba Jaji Sehel hakufuata mchakato stahiki wa kisheria na kuweka rekodi ya sababu za kuchukua kesi hiyo kutoka kwa mtangulizi wake, Jaji Mwambegele.

Hoja zote hizo zilipingwa na mawakili wa mjibu rufaa; Joseph Rutabingwa akisaidiana na Idda Rugakingira.

Katika hukumu hiyo, Jaji Galeba amekubaliana na hoja za mawakili wa mjibu rufaa akisema ushahidi unaonyesha kuwa hakukuwa na makosa kisheria kwa Jaji Sehel kuendelea na kesi kutoka kwa Jaji Mwambegele.

“Kuhusu hoja kuwa mjibu rufaa alipokea SMS zikimtaarifu kuwapo kwa miamala kutoka kwenye akaunti yake kwenda Afrika Kusini, tunakubaliana na mawakili wa mjibu rufani kwamba SMS hizo, hata kama angekuwa ametumiwa, hazikuwa na maana.

“Hii ni kwa sababu, SMS hizo zilitumwa Machi 10, 2014 wakati fedha tayari zilikwisha kuhamishwa. Pia mrufani hakupeleka mahakamani ushahidi kutoka Vodacom kuonyesha ukweli kwamba SMS zilitumwa kwa mtu husika,” anasema Jaji.

Anasema pia kuwa shahidi muhimu anayedaiwa kuanzisha mawasiliano kwa njia ya internet kwa idhidi ya Future Trading Limited, Anita Moshi, hakuitwa mahakamani kutoa ushahidi, hivyo kukosekana ushahidi muhimu kwamba Mkurugenzi wa Future Trading Limited aliufahamu uhamishaji huo wa fedha.

“Kwa kuzingatia hayo, hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu iendelee kama ilivyo pamoja na gharama zote,” anahitimisha Jaji Galeba kwa niaba ya jopo la majaji waliosikiliza rufani hiyo.

Kwa hukumu hiyo, sasa Ecobank Tanzania Limited imetakiwa kumlipa mlalamikaji Sh milioni 66.24 ambazo zilihamishwa kinyemela kutoka kwenye akaunti yake kwenda kwa mtu asiyeidhinishwa.

Pili, Ecobank Tanzania Limited imlipe mlalamikaji Sh milioni 25 ikiwa ni malipo ya fidia kwa madhara yaliyotokana na benki husika kufanya malipo bila idhini ya mteja.

Tatu, Ecobank imlipe mlalamikaji riba ya kiwango cha asilimia saba kuanzia siku ya hukumu hadi itakapokuwa imemaliza kulipa deni hilo.

Nne, mteja arejeshewe gharama za uendeshaji wa kesi hiyo.

Taarifa ya JAMHURI Aprili 2019

Katika taarifa iliyochapwa Aprili, JAMHURI linamnukuru Mkurugenzi wa Future Trading Company Limited, Suwed, amesema licha ya hukumu (ya mwaka 2019), Ecobank imegoma kumlipa.

“Januari 3, mwaka huu [2018] nimeiandikia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) malalamiko yangu, lakini sijafanikiwa. Sijapata msaada wowote,” amesema.

Fedha hizo ziliibwa na wafanyakazi wa Ecobank Machi 10, 2014 kupitia mfumo wa internet banking.

Jaji Sehel, amejiridhisha pasi na shaka kuwa Kampuni ya Future Trading Limited iliingizwa kwenye huduma ya Internet banking bila ridhaa yake; na kwamba hata fomu za kufunguliwa kwa akaunti ya kampuni hiyo kwenye sehemu ya huduma hiyo kuliwekwa alama ya “X” kuonyesha kuwa hakuihitaji huduma hiyo.

Walalamikaji waliripoti polisi na kufunguliwa jalada Na. IR/CD/1060/2014 na baadaye kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania (Divisheni ya Biashara).

Mahakama Kuu imethibitisha kuwa sahihi ya mkurugenzi wa Future Trading Company Limited ilighushiwa. Fomu zilizotumika kuingiza kwenye huduma ya kibenki kwa njia ya mtandao (internet banking) haikuwa na mihuri ya benki wala sahihi ya ofisa aliyeidhinisha kuingia kwenye huduma hiyo.

Fomu hazikuwa na mhuri wa kampuni, sahihi inayodaiwa kuwa ni ya mkurugenzi haifanani na sahihi zilizopo katika fomu ya kufungulia akaunti Ecobank.

Namba za simu zilizowekwa kwenye fomu mahususi za kujiunga (set up form) hazijulikani na haziko kwenye fomu iliyojazwa na Future Trading Company Limited wakati wa kufungua akaunti.

Mahakama imejiridhisha kuwa fomu hizo (set up form) pia zilikuwa na anuani ya ofisi (physical address) ambayo si sahihi.

Imebainika kuwa mwandiko uliotumika kujaza fomu hiyo si wa viongozi wa Future Trading Company Limited; na wala hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa wenye kampuni hiyo walipewa nywila (password) ya huduma ya internet banking; hapakuwapo mafunzo au maelekezo yoyote ya huduma ya internet banking, hapakuwa na maazimio ya bodi ya kuruhusu benki kuwapatia Future Trading Company Limited huduma hiyo.

Mahakama imesema uhakiki wa mtumaji wa fedha na mpokeaji kama inavyoelekezwa na BoT haukufanyika kama inavyoelekeza kwenye miongozo ya BoT ya huduma za benki za kielektroniki ya mwaka 2007.

Hatua nyingine

Kampuni ya Future Trading Ltd inasema kuwa ilibaini hali isiyo ya kawaida kwenye akaunti yao Machi 13, 2014 kwa fedha kuondolewa katika akaunti bila idhini yake.

Kiasi cha fedha kilichochotwa kwenye akaunti hiyo ni Sh milioni 66.24 na baada ya benki kuulizwa walielezwa kuwa fedha hizo zimehamishwa kwenda kwa mpokeaji aliyeko nchini Afrika Kusini kwa njia ya ‘telegraphic transfer’, ikidaiwa kuwa ni maagizo ya Kampuni ya Future Trading Company Limited.

Kampuni hiyo ilikana madai hayo ya kuagiza fedha hizo kuhamishwa na kuitaka benki izirejeshe.

Kati ya mambo ambayo mlalamikaji aliomba mahakama iamue ni kulipwa Sh milioni 66.24; kulipwa faini ya Sh milioni 50 kutokana na kushindwa kutunziwa akiba yao katika benki hiyo, sambamba na usumbufu waliosababishiwa kutokana na tukio hilo la wizi wa fedha zao.

Mlalamikaji aliomba alipwe Sh milioni 50 za fidia kutokana na kukiukwa kwa mkataba wa kibenki kati yake na benki; alipwe malipo ya usumbufu wa jumla kadiri itakavyoamuliwa na mahakama; na alipwe gharama za uendeshaji wa kesi.

Mchezo ulivyokuwa
 

Katika kesi hiyo, shahidi kwa upande wa mlalamikaji, Abubakar Suwed, aliieleza mahakama kuwa alibaini wizi huo Machi 13, 2014.

Alisema alipigwa butwaa baada ya kubaini Sh milioni 66.24 zimehamishwa na alipoutaarifu uongozi wa benki alielezwa kuwa fedha hizo zimehamishwa na kupokewa nchini Afrika Kusini kwa njia ya ‘telegraph transfer’ kupitia maelekezo ya kielektroniki yaliyokuwa yakitolewa na barua pepe ya mlalamikaji iliyosajiliwa katika benki hiyo.

Suwed amesema hakuna popote ambako alisaini kuidhinisha uhamishaji huo wa fedha na wala hakutumia mfumo wa kielektroniki kufanya mawasiliano.

Amesema pamoja na malalamiko yake, benki hiyo iligoma kurejesha fedha hizo.

Akaiambia mahakama kuwa kampuni imeshindwa kuendesha shughuli zake na kupoteza fursa nyingi za kibiashara na muda.

Katika mahojiano na wakili mahakamani (cross examination), shahidi namba moja upande wa mlalamikaji alikiri kwamba wakati akifungua akaunti katika benki hiyo alitoa anuani ya barua pepe rasmi kwa ajili ya mawasiliano.

Alisema hakutoa nywila kwa benki hiyo kuweza kuingia kwenye akaunti yake, bali aliwapa namba yake ya simu kwa ajili ya mawasiliano.