Gwajima, Polepole, Silaa wazidi kubanwa mbavu

DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Mienendo ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Askofu Josephat Gwajima (Kawe), Jerry Silaa (Ukonga) na

Humphery Polepole (kuteuliwa) inazidi kumulikwa.

Kumulikwa kwa mienendo hiyo hasa kwa Gwajima na Silaa kunatokana na kuadhibiwa Jumanne wiki iliyopita kutoshiriki mikutano miwili na kulipwa nusu mshahara baada ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kupendekeza watiwe hatiani kwa makosa ya kusema uongo, kushusha hadhi na heshima ya Bunge, kisha kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Wabunge wa CCM.

Baada ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka, kusoma hukumu kwa wabunge hao na kutoa mapendekezo mengine ya kuchukuliwa, ikiwamo ya Silaa kuvuliwa nafasi ya uwakilishi katika Bunge la Afrika (PAP) na kufikishwa mbele ya CCM ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa maadili ya chama hicho, naye Spika wa Bunge, Job Ndugai, ameviagiza vyombo vingine viwachunguze ili kujiridhisha kuhusu mienendo yao.

“Ukifanya mambo ya hovyo lazima ujisahihishe, suala la Askofu Gwajima, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mpo, sisi tumenawa na mkikaa kimya msishangae mkiitwa katika Kamati ya Maadili,” anasema Ndugai.

Maagizo ya Ndugai na kamati hiyo kwa ujumla yakazidi kutekelezwa dhidi ya wabunge hao akiwamo Polepole baada

ya kuanza ‘kubanwa kikaoni’ pale walipoitwa Ijumaa ya wiki iliyopita kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Wabunge wa

CCM ikiwa ni siku mbili baada ya kuadhibiwa na Bunge.

Katibu wa Wabunge wa CCM, Rashid Shangazi, anasema wabunge hao wawili wameitwa ikiwa ni utekelezaji wa mapendekezo ya Bunge ya kutaka wahojiwe pia wamemuita Polepole ambaye naye amehojiwa masuala mbalimbali

ikiwamo kushabikia mambo katika mitandao ya kijamii.

Shangazi anasema hatua ya kuwaita wabunge hao ni ya kwanza inayohusisha mazungumzo na majadiliano na watakapoona kuna haja zaidi watakwenda hatua ya pili.

Kama alivyosema Shangazi ndivyo inavyotokea baada ya hatima ya sakata la wabunge hao kupelekwa katika Kamati

ya Uongozi ya Wabunge wa CCM inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Kassim Majaliwa, ambaye pia ni Waziri Mkuu kwa ajili ya kushughulikiwa zaidi.

Jana Septemba 6, mwaka huu majina ya wabunge hao yalitarajiwa kuwasilishwa mbele ya kamati hiyo ya uongozi kwa ajili ya kupitia tuhuma zinazowakabili.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Wabunge wa CCM, Hassan Mtenga, anasema wao wamemaliza kazi na mapendekezo wameyapeleka katika Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM na itajulikana nini kitakachofuata.

Pia Mtenga ametaja sababu za Polepole kuitwa katika kamati hiyo kuwa ni kushabikia mambo yaliyosemwa na Gwajima

katika mitandao ya kijamii.

Katika hatua nyingine, Shangazi, anasema ziko adhabu za aina tofauti kwa wabunge kama hao pindi watakapobainika

wamekiuka maadili na amesisitiza kuwa mienendo ya wabunge hao, hasa Gwajima na Polepole haileti picha nzuri

ya kibunge na chama hicho.

Agosti 25 na 28, mwaka huu Gwajima na Silaa walihojiwa kwa mara ya pili, tofauti na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya

Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge huku Mwakasaka na wajumbe wa kamati hiyo wakisema bungeni kuwa wabunge

hao ni wajeuri na waongo na walishindwa kujutia kauli zao na mmoja wao alisisitiza ataendelea kuzitoa.

Silaa alitiwa hatiani na kamati hiyo baada ya kukiri kusema kuwa mishahara ya wabunge inakatwa kodi lakini alisisitiza

kuwa posho na marupurupu mengine ndiyo hayakatwi kodi.

Pia licha ya kupewa nafasi ya kujitetea hakuonyesha dalili ya kujutia, jambo linalotajwa kuwa alikusudia kufanya hicho

alichokisema ambacho ni uongo na uchonganishi kati ya Bunge na wananchi, huku Ndugai akikazia hoja hiyo kuwa

suala la kodi ni kitu kikubwa na katika nchi nyingine watu wakisikia wamekwepa kodi wanajinyonga.

Kwa upande wa Gwajima, kamati hiyo ilimtia hatiani kutokana na matamshi yake kwamba walioruhusu chanjo ya

ugonjwa wa corona (Covid-19) ianze kuchanjwa hapa nchini walipokea rushwa kutoka kwa nchi wahisani, kwa nini

chanjo itoke nchi moja na si nyingine kama China, na kauli nyingine kwamba watakaochanja hawatazaa.

Pia alipotakiwa athibitishe kauli zake kwamba kuna waliopokea rushwa na hakuna chanjo nyingine za corona zaidi ya Johnson & Johnson, alishindwa, kwa kuwa kuna chanjo nyingine kutoka China ziko Zanzibar.