ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali imefanya uamuzi

mgumu wa kuziuza meli zote za Shirika la Meli la Zanzibar (Shipco).

Akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara yake katika mikoa miwili ya Pemba, Dk. Mwinyi amesema uamuzi huo umekuja kutokana na gharama kubwa za uendeshaji wa meli hizo.

Amesema meli hizo zitauzwa kwa lengo la kununua meli ambazo hazitakuwa na gharama kubwa za uendeshaji.

“Shirika letu la meli sasa hivi ni kama limekufa. Hakuna meli hata moja inayofanya kazi. Tunachukua uamuzi wa makusudi. Wakati mwingine ni lazima tuchukue uamuzi mgumu. Sasa meli zote zile ziuzwe,” amesema.

Rais amesema baada ya kuziuza meli hizo zitanunuliwa meli nyingine za kisasa zinazoendana na mazingira ya sasa.

Anazitaji meli za kisasa za Bakhresa kama mfano wa meli zinazopaswa kununuliwa na serikali zitakazobeba mizigo na abiria.

“Meli kubwa kama Mapinduzi II ni gharama kuiendesha. Hata kama ingekuwa inafanya kazi, ikitiwa mafuta na kusafiri

mpaka hapa, fedha zote zinakwenda kwenye mafuta. Hatuwezi kuendelea nayo.

“Sasa hatuwezi kufanya kazi namna hii. Tutachukua uamuzi huo na tutaliunda tena shirika letu la meli ili lilete meli kama hizi na kuondokana na adha ya usafirishaji wa abiria na mizigo,” anasema Dk. Mwinyi.

Aidha, anasema SMZ itachukua juhudi za makusudi kuimarisha uchumi na kulipa hadhi zao la karafuu. Akizungumzia suala la udhalilishaji, Rais Dk. Mwinyi amesema wote wanaotenda vitendo hivyo wasipewe dhamana, hata mahabusu ikijaa, wapelekwe katika vyuo vya mafunzo kusubiri kesi.

Amewataka viongozi wa mikoa na wilaya kusikiliza kesi za wananchi waliodhulumiwa haki zao, akisisitiza kwamba watumishi wote ambao hawawajibiki wataendelea kuchukuliwa hatua, wabadhirifu na wezi wa mali za umma wataendelea kufukuzwa kazi.

Awali, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mkoani baada ya hafla ya kukabidhi boti kwa ajili ya wananchi wa Kisiwa cha Makongwe na Kisiwapanza, Dk. Mwinyi amesema serikali itafanya juu chini kupeleka maendeleo kwa wananchi kama ilivyowaahidi wakati wakipita kuomba ridhaa ya kuchaguliwa na kuwa tena madarakani.

Rais Dk. Mwinyi amesema anatambua kikwazo kikubwa cha maendeleo katika kipindi kilichopita ni kukosekana umoja wa wananchi na mshikamano na ndiyo Serikali ya Awamu ya Nane imetengeneza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa lengo la kuleta amani na umoja utakaokuza maendeleo ya haraka.

Alifahamisha kuwa ni jambo la kushukuru kuwa nchi kwa sasa imetulia, ina amani na hakuna sababu kusipatikane maendeleo na aliwapongeza wananchi kwa kuunga mkono juhudi hizo zilizochukuliwa na viongozi wao.

By Jamhuri