Maofisa wa Bank of Africa (BOA) jijini Dar es Salaam wanadaiwa kughushi hati ya ardhi Na. 55709, Kitalu ‘C’, Ukonga Stakishari ya Jimmy Mwalugelo (68), mkazi wa eneo hilo na kuitumia kumkopesha mtu mwingine Sh milioni 500.

Hati hiyo iliyoghushiwa na maofisa wa BOA inajumuisha viwanja namba 660/1, 662/1, 696/1 na 698/1 na viwanja namba 665 na 666 ambavyo havipo katika hati hiyo.

Maofisa wa BOA walitumia vivuli vya hati ya Mwalugelo kama dhamana ya mkopo kwa Rose Assea, mfanyabiashara wa Soko la Kariakoo, duka namba 32, lililoko katika makutano ya Mtaa wa Kongo na Narung’ombe, Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI unaonyesha kuwa maofisa wa benki hiyo walitumia vivuli vya hati hiyo kumkopesha Assea mkopo wa Sh milioni 100 mwaka 2011, Sh milioni 200 mwaka 2014 na Sh milioni 200 mwaka 2015 wakati mmiliki wa hati hiyo akiwa hafahamu kinachoendelea.

Katika mkataba kati ya BOA na Assea walikubaliana kwamba mkopaji atarejesha Sh milioni 5 kila mwezi bila kukosa kwa dhamana ya viwanja namba 660/1, 662/1 na 698/1, Kitalu ‘C’, Ukonga Stakishari.

Katika awamu tatu, Assea alikuwa amefanikiwa kurudisha mikopo yote aliyokuwa amekopeshwa na benki hiyo, lakini mkopo wa mwisho alishindwa kuurejesha kama walivyokuwa wamekubaliana.

Chanzo chetu cha habari kinaeleza kuwa maofisa wa BOA walikuwa wakimfuata mara kwa mara mdaiwa wao katika duka lake, lakini akawaeleza kuwa hawezi kulipa mkopo wake hadi atakapopatiwa nusu ya mkopo uliobaki.

Kwa mujibu wa vielelezo tulivyonavyo, baada ya kuona anasumbuliwa na maofisa hao, Assea aliamua kwenda katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kufungua kesi iliyopewa Na. 103 ya mwaka 2016, akiomba BOA wazuiwe kumbughudhi au kujaribu kushikilia na kuliuza duka lake kwa njia ya mnada.

Juni 17, 2016, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Sachore, alitoa zuio la muda (Interim Order) hivyo BOA waliacha kumbughudhi mfanyabiashara huyo waliyempa mkopo kwa hati iliyokuwa ikitumika isivyo halali kuidhinisha mikopo hiyo. Badala yake, waliamua kwenda kubomoa nyumba za mtu asiyehusika kwa maelezo kuwa ameshindwa kulipa mkopo aliouchukua.

Mwalugelo amelieleza JAMHURI kuwa Aprili, 2011 akiwa mteja wa muda mrefu wa BOA alikwenda kuomba mkopo wa Sh milioni 100 katika tawi la benki hiyo, Tawi la Kariakoo, lakini akaelezwa kuwa lazima ufanyike utaratibu wa kukagua nyumba anayotaka kuweka kama dhamana ya mkopo huo.

“Meneja wa Mikopo wa benki hiyo, Tawi la Kariakoo alinieleza kuwa nilete nakala ya hati ya nyumba ili wamtume mthamini wao kwa ajili ya kujiridhisha kama inakidhi masharti ya mkopo au la.

“Baada ya wiki tatu waliniita na kunieleza kuwa eneo langu linatosha kupewa mkopo unaoanzia Sh milioni 100 hadi 180. Niliwaeleza kuwa hitaji langu ni Sh milioni 100 tu.

“Wakaniambia maombi yangu ya mkopo wanayapeleka makao makuu ya benki hiyo na baada ya mwezi mmoja wakasema mkopo umepita, hivyo nipeleke akaunti yangu, kikonyo cha kitabu cha hundi (check reference book) na hati ya nyumba.

“Niliwapelekea vielelezo hivyo nao wakanieleza kuwa tayari wameniingizia fedha hizo, lakini wakataka kwanza niwaandikie wao hundi ya Sh milioni 24. Nikawauliza hiyo hela ya nini?

“Wakanieleza kuwa Sh milioni 20 ni mgawo wa maofisa wa benki hiyo makao makuu walioidhinisha mkopo huo, Sh milioni 2 atapewa mthamini na Sh milioni 2 nyingine zitakuwa ni bima ya mkopo.

“Nikawaeleza kuwa siwezi kutoa fedha hizo kwa kuwa nitakuwa ninalipa Sh milioni 40 ambazo sijazifanyia kazi yoyote, nikawataka wanirudishie hati yangu na kikonyo cha kitabu cha hundi.

“Sikuchukua mkopo wao, hakuna wanachonidai, lakini kilichonishangaza Novemba, 2016 nikapata taarifa kutoka kwa mjumbe kuwa nyumba yangu inapigwa mnada na BOA kwa kuwa ilitumika kama dhamana kwa mkopo wa mtu (Assea).

 “Simfahamu mtu huyo, wala sijawahi kumdhamini kwa kutumia hati yangu, nikaelezwa na madalali wa benki hiyo kutoka Kampuni ya Mabunda Auctioneers Mart Ltd kwamba nionane na Mkurugenzi wa Mikopo wa BOA kwa ajili ya ufafanuzi,” amesema.

Mwalugelo amesema aliamua kwenda katika tawi la benki hiyo, Sinza Kijiweni kuonana na mkurugenzi huyo, lakini akaelezwa kuwa atoe Sh milioni 5 wasimamishe taratibu za kupiga mnada nyumba zake na kuwarudisha madali hao mkoani Arusha.

Amesema hakutoa fedha hizo kwa kuwa ni mwendelezo wa vitendo vya uonevu na utapeli anaofanyiwa na maofisa wa BOA.

Hata hivyo, amesema mke wake, Unosye Mwalugelo, alikimbilia katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kufungua kesi akidai kuwa mumewe (Mwalugelo) amemdhamini mtu ambaye hawamfahamu bila ya kuishirikisha familia yake.

Katika kesi hiyo Na. 49 ya 2017, Unosye (mkewe Mwalugelo) alikuwa anawalalamikia Rose Assea, Bank Of Africa (T) LTD na Mabunda Auctioneers Mart Co. LTD kutaka kuuza mali za familia hiyo wakati hawahusiki kumdhamini Assea.

Pamoja na hayo, mahakama ilitoa zuio (stop order) na kuwakusanya wahusika wote asiwepo atakayeleta shida hadi shauri la msingi litakapopatiwa ufumbuzi.

Mwalugelo amesema kilichomshangaza ni kuona BOA wakipuuza maagizo ya mahakama na kwenda kubomoa nyumba zake tano wakati hata shauri halijaanza kusikilizwa.

Nyumba hizo tano, likiwemo Kanisa la Moravian zilibomolewa na mabaunsa wa Kampuni ya Udalali ya Mabunda kwa kushirikiana na BOA Oktoba 17, mwaka jana, majira ya saa 10 alfajiri.

Amesema vitu vyote vilivyokuwemo katika nyumba hizo viliibwa na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni 3.

JAMHURI limefika Makao Makuu ya BOA, Barabara ya Sokoine jijini Dar es Salaam, Ijumaa, Septemba 28, mwaka huu majira ya saa 6 mchana kupata ukweli kuhusu benki hiyo kutumia hati ya Mwalugelo kumkopesha mtu mwingine na kubomoa nyumba zake tano, lakini likaelezwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji yuko safarini.

Hata hivyo, baadhi ya watumishi wa benki hiyo walimwelekeza mwandishi wa JAMHURI kwenda katika kitengo cha ‘recovery’ na kuonana na ofisa mmoja aliyetambulika kwa jina la Victor na alipoulizwa kuhusu suala hilo akasema kuwa yeye si msemaji, hivyo atafutwe Kaimu Mkurugenzi Mtendaji aliyefahamika kwa jina la Maria.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji (Maria) alipotafutwa ofisini kwake hakupatikana kutokana na kuwa kwenye kikao na aliwapowasiliana na Katibu Muhtasi wake kwa njia ya simu akataka aandikiwe maswali na yawasilishwe ofisini kwake Jumatatu ya Oktoba 1, mwaka huu.

JAMHURI liliwasilisha maswali hayo katika benki hiyo kama walivyotaka, lakini tangu Jumatano hadi Ijumaa wiki iliyopita limekuwa likifuatilia majibu ya maswali hayo bila mafanikio huku wahusika wakitaka watafutwe tena kwa njia ya simu ya kiganjani na ya mezani ambazo haziko hewani.

Ijumaa iliyopita majira ya saa tano asubuhi, JAMHURI lilifuatilia tena majibu ya maswali yake katika benki hiyo na kujibiwa na ofisa mmoja wa benki hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja na Joyce kuwa hawawezi kujibu maswali hayo kwa kuwa suala hilo liko polisi na mahakamani.

Mwalugelo amesema nakala zote mbili na halisi (original) za hati yake anazo hadi sasa na moja iko katika taasisi moja ya serikali, kinachoonekana alipokataa kuchukua mkopo walibaki na vivuli ambavyo walivitumia kumpa mtu mwingine mkopo.

BOA walihamisha umiliki wa hati Na. 55709 mali ya Mwalugelo kwenda kwa Yusuf Omary, mkazi wa Dar es Salaam, Januari 2018, ambaye anadaiwa kuuziwa eneo hilo.

Uchunguzi uliofanywa katika Ofisi ya Msajili wa Hati, Julai 28, mwaka jana, unaonyesha kuwa hati hiyo ya kiwanja chenye ukubwa wa mita za mraba 2,406 imebadilishwa umiliki wake na kupewa Omary bila kumshirikisha mmiliki wa eneo hilo.

Mwalugelo amesema wakati taratibu za kudhulumu eneo lake zilipokuwa zikiendelea, maofisa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na BOA hawakumtaka aisalimishe hati hiyo kwa kuwa walikuwa wanafanya utapeli.

Oktoba 31, mwaka jana aliandika barua Benki Kuu ya Tanzania (BoT) akiilalamikia BOA kuvamia nyumba zake na kuzibomoa kwa mkopo ambao hausiki nao kwa namna yoyote na kuwanyanyasa bila sababu za msingi watu waliokuwa wakiishi katika nyumba hizo.

BoT pamoja na kuipokea barua hiyo Novemba 2, mwaka jana, hakuna jibu lolote walilolitoa kwa mlalamikaji hadi leo hii wala hatua zozote dhidi ya benki hiyo.

Majibu ya BoT

Hata hivyo, Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Benki (BoT), imekana kupokea barua hiyo ya malalamiko ya Mwalugelo, licha ya nakala hiyo kugongwa muhuri wa kupokelewa na Benki Kuu, JAMHURI limeiona barua hiyo.

Kaimu Ofisa Habari wa BoT, Victoria Msina, amesema: “Kwa upande wetu sisi hatujapokea barua hiyo. Hata hivyo, malalamiko ya wateja wanaohudumiwa na benki zinazosimamiwa na Benki Kuu huwa yanapelekwa kwenye kitengo cha dawati la kutatua malalamiko ya wateja.”

Pamoja na Benki Kuu kukana kuwa hawakupokea barua ya malalamiko kutoka kwa Mwalugelo anayeilalamikia Benki ya BOA kubomoa nyumba zake na kubadilisha umiliki wa hati yake ya kiwanja wakati hahusiki na mkopo wala kumdhamini mtu yeyote, Oktoba 17, mwaka huu wameibuka wakijibu barua hiyo ya Oktoba 31, mwaka jana.

Barua hiyo ya Benki Kuu yenye kumbukumbu namba FA.56/433/42/21 ambayo imesainiwa na watu wawili; Thomas Mongella na Mary Lukoo inamweleza mlalamikaji kwamba waliwahi kumwandikia majibu ya barua yake Novemba 10, mwaka jana kwa barua yenye kumbukumbu namba FA.56/293/108/VOL.III/78.

Sehemu ya barua hiyo inaeleza kuwa mlalamikaji amefungua shauri Na. 303 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, kitengo cha ardhi, hivyo benki haina mamlaka ya kuingilia mahakama.

 Hata hivyo, Mwalugelo amelieleza JAMHURI kuwa hajawahi kupata majibu yoyote kutoka BoT tangu walipohojiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na wala barua hiyo hajawahi kuipata.

Mahakama yatupa maombi ya BOA

Mahakama ya Biashara kupitia hukumu iliyoitoa imetupa kesi iliyofunguliwa na BOA ikitaka kumshinikiza Mwalugelo afahamike kuwa alitoa nyumba zake kama dhamana.

 Benki ya BOA ilifungua kesi Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara dhidi ya Rose Assea iliyopewa Na. 138 ya mwaka 2017, ikimdai Sh milioni 101.6561 kwa kuisababishia benki hasara na kulipa gharama za kesi husika.

Benki ya BOA ambayo katika shauri hilo ilikuwa ndiye mlalamikaji, iliiambia mahakama kwamba kwa nyakati tofauti mwaka 2011, 2014 na 2015 Assea alipewa mkopo wa Sh milioni 100, Sh milioni 200, na mkopo mwingine wa Sh milioni 200 ikiwa ni mtaji wa kufanyia biashara za jumla za kuuza nguo na mikoba kutoka nje.

Wakiwa katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, BOA walidai kwamba dhamana ya mikopo hiyo kwa mteja wao huyo ni hati ya viwanja namba 662/1, 662/1 na 698/1, Kitalu ‘C’, Ukonga Stakishari, Ilala jijini Dar es Salaam, ambavyo vinamilikiwa na Jimmy Mwalugelo.

BOA walidai kuwa mteja wao huyo alitakiwa kulipa mkopo wake wa mwisho na riba kufikia Aprili 2016 kulingana na makubaliano waliyoafikiana naye.

Katika shauri hilo BOA inasema Aprili 4, mwaka juzi ilimpa notisi ya siku 60 mdaiwa wao, notisi hiyo ilimtaka mdaiwa kulipa mkopo lakini hakuweza kufanya hivyo na baadaye wakatoa notisi nyingine ya siku 14 kwamba watauza dhamana iliyowekwa kwa ajili ya mkopo, hata hivyo bado hakulipa.

Pamoja na ushahidi uliotolewa kwa upande wa mlalamikaji na hukumu kutolewa kwa upande mmoja (Judgment Ex-Parte) Jaji wa Mahakama Kuu, A. R. Mruma, aliyekuwa anasikiliza shauri hilo alilitupilia mbali.

“Ni wakati mwafaka kwa mabenki kufahamu kwamba wanapoamua kutumia mamlaka yao ya kuuza mali zilizowekwa dhamana kwa mujibu wa mkataba, na uuzwaji wa dhamana kushindwa kufikia gharama halisi aliyokopeshwa mteja, hawawezi kuja mahakamani kudai kwamba hawakupata kiwango cha fedha walichotakiwa kulipwa na kuomba kuuza kwa mnada mali nyingine za mdeni.

“Mali pekee zilizowekwa kama dhamana ndizo zitumike kurejesha fedha kwa mujibu wa mkataba wa mkopeshwaji. Hivyo shauri hili la kibiashara Namba 138 la mwaka 2017 limetupwa,” anaandika Jaji Mruma katika hukumu hiyo.

Tuhuma nyingine za BOA

Kati ya mwaka 2016 na mwaka jana barua pepe ya Padri Paschal Luhengo wa Jimbo la Mahenge, Mkoa wa Morogoro luhengop4@gmail.com ilivamiwa na wezi wa mtandao na kutapeli mamilioni ya fedha kutoka kwa rafiki zake waishio nje ya nchi.

Baada ya kuteka anuani yake ya barua pepe wakabadili namba zake za simu kutoka +255784429628 na kuweka namba ya Uganda, pia wakabadilisha anuani yake ya barua pepe kutoka Luhengop4@hotmail.com kuwa sgs.africa@yahoo.com.

Watuhumiwa hao walifungua akaunti Na. 01646030005 katika Benki ya BOA Tawi la Kariakoo, Dar es Salaam na kufanya jaribio la kujipatia kiasi cha dola 200,000 kutoka kwa St Stewart wa Australia, walizodai ni kwa ajili ya ujenzi wa kanisa, Parish ya Lupilo – Mahenge.

Jaribio hilo la uhalifu liliwahusisha baadhi ya maofisa wa BOA kutoka katika tawi hilo. Hata hivyo wizi huo ulizuiwa baada ya Padri Luhengo kutoa taarifa mapema Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kipolisi Kariakoo kwa kufuatilia nyaraka mbalimbali.

2868 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!