Mwezi uliopita nilizindua kitabu changu kipya kiitwacho ‘MAFANIKIO NI HAKI YAKO’ ambacho kinauzwa kwa njia ya mtandao.

Jambo kubwa nililolifanya kutokana na kitabu hiki ni kuandaa mfumo unaoendelea kumsaidia mtu anayenunua kitabu hiki kuyaweka katika vitendo yale atakayoyasoma na kujifunza kutoka katika kitabu hiki.

Mtu akinunua kitabu hiki anapata wasaa wa kuunganishwa na kundi maalumu kwenye mtandao wa Whatsapp liitwalo, “SmartMind For SmartSuccess”.

Kundi hili tumelibatiza jina la ‘Bunge la kiuchumi Tanzania-BKT’, kutokana na kwamba tumeweka mipango mikakati ya kuhakikisha kwamba wanakundi wote wanafikia uwezo wa kivipato sawa ama zaidi ya yale mamilioni ambayo hulipwa wabunge kama kiinua mgongo. 

Lengo hili limepangwa kufikiwa kwa namna tatu. Kwanza ni kulifanya kundi hili kuwa kituo cha mafunzo, semina na warsha za biashara, uchumi na uwekezaji.

Walimu, wataalamu na wazoefu wa maeneo hayo wameunganisha nguvu zao kuhakikisha wanatupiga msasa wanakundi wote ili tuive kiuchumi na kibiashara tayari kwa kuingia ‘mzigoni’.

Njia ya pili ambayo kundi hili litafanikisha visheni hii ni kwa kujenga mtandao (network) miongoni mwa wanakundi ambako watu watasaidia kujulishana na kuziendea fursa huku wakipokea ushauri na usaidizi wa kitaalamu. 

Njia ya tatu ambayo kundi hili limepanga kuifikia visheni hii ya kuwatengeneza wabunge wa kiuchumi ni kupitia uanzishaji wa kampuni ya pamoja ya kiuwekezaji itakayojulikana kwa jina la ‘SmartSuccess Community Company’. 

Kampuni hii inakusudia kuwekeza kisasa katika maeneo ya kilimo cha kisasa cha matunda na ufugaji na wanahisa wake watakuwa ni wale tu waliomo kwenye kundi hili la ‘SmartMind For SmartSuccess’.

Kwa sababu kuna mpango maalumu wa kimafunzo utakaoendeshwa kwa muda fulani kabla ya uwekezaji wa kama kundi na hata wa kama mtu mmoja mmoja.

Kampuni hii kwanza tunategemea itawasaidia wanakundi kupata faida za kuelekea ubunge kiuchumi na pili itatengeneza ajira. Tayari kuna utafiti wa kina unaendelea kuhusu miradi ambayo kampuni hii tarajali inafikiria kuiendea.

Kwa kuwa ninayo timu makini yenye weledi, uzoefu na maono thabiti naamini tutafanya kitu cha mfano kwa uchumi wa nchi

Mwingine atauliza, ni kwa sababu zipi, Sanga umeamua kufanya programu hii? Jibu ni rahisi. Mimi Sanga nimekuwa nikiandika sana kuhusu uchumi, ujasiriamali na biashara kwa takribani mwaka wa sita sasa.

Nilipofikia ninatamani nishuhudie wafanyabiashara na wajasiriamali wengi zaidi wakizaliwa na kukua kupitia uwezo huu wa kuandika niliopewa na Mungu. 

Ndio maana nimeamua kuchukua hatua kwa vitendo kwenda na wale wanaofuatilia maarifa yangu kwa ukaribu. Ndio maana tena utaona kwamba wanaoingia katika mpango huu ni wale watakaonunua na kusoma kitabu hiki kipya cha ‘MAFANIKIO NI HAKI YAKO’.

Mwingine ataniuliza inakuwaje kwa sisi ambao hatuna kompyuta wala simu za kisasa zinazoweza kupokea hicho kitabu na hiyo whatsapp? Ukweli ni kwamba dunia inahamia kwenye digitali.

Mlango wa kufaidika na dijitali umefunguliwa; hatuwezi kuacha kuingia kwa sababu kuna wenzetu bado hawajafika karibu na mlango. Niseme kwamba kwa ‘programu’ hii, sisi tutatangulia, ninyi ambao bado hampo kidijitali kwa sasa, mtatukuta huko mbeleni.

Wanaofuatilia makala zangu tangu zamani bila shaka wangali wanakumbuka kwamba nimewahi kuandika makala kuhusu uchumi wa taarifa. Nilieleza kwa sehemu kwamba mafanikio ya kibiashara kwa sasa yamo katika uharaka, uwezo na ujuzi wa mtu kuweza kumiliki taarifa na kuzitumia itakiwavyo au twaweza sema mafanikio ya sasa yapo kidijitali zaidi.

Uchumi wa taarifa ambao ndio unaoishika dunia kwa kasi sasa; unaweza kufanya biashara bila ardhi, unaweza kuzalisha fedha pasipo kutumia mtaji na unaweza kuwa milionea pasipo hata kuhitaji rundo la watu.

Vigezo vya uzalishaji (factors of production) kwa sasa ni wazo, taarifa, uwezo wa kuwasiliana na ujasiriamali. 

Kwenye uchumi wa taarifa ni kwamba mawazo (ideas) yana bei kubwa kuliko bidhaa. Kwa hiyo; katika uchumi wa taarifa ni suala la kawaida kuona kwamba mtu mwenye wazo (asiyekuwa na mtaji wa fedha hata senti moja) akawa na fedha nyingi, mali ama utajiri mkubwa kuliko mmiliki wa kiwanda!

Kufanikiwa kiuchumi na kibiashara katika uchumi wa taarifa unahitaji uwe ni mtu unaetafuta taarifa kwa bidii, unaezichakata kwa ufanisi na kuibuka na mambo ya kukusaidia. Kwa hii kuna kazi kubwa mbili zinazoweza kukuzalishia utajiri katika uchumi wa taarifa; nazo ni kutafuta taarifa na kufikiria. Kazi zote mbili zinahitaji ubongo na wala sio fedha! 

Mtu yeyote katika uchumi wa sasa akisema ameshindwa kuanzisha biashara kwa sababu yeyote ile; ukweli ni kwamba anakuwa akituambia kuwa hajauweka ubongo wake kazini.

Mfanyabiashara yeyote akilalamika kuwa biashara zinamuendea kombo basi lazima akague namna anavyoushughulisha ubongo wake. Hakuna namna ya kufanikiwa katika uchumi wa taarifa zaidi ya kuwa mtu unaenufaika na taarifa.

Ipo mifano kadhaa tunayoweza kuitazama yenye kuonesha namna mifumo ya biashara katika uchumi wa taarifa ilivyoleta mageuzi makubwa sekta mbalimbali. Bila shaka wengi wetu tunafahamu na pengine tunatumia benki za simu (mobile banking). Kuna jambo la kujifunza katika hizi benki za simu.

Benki za simu, ni kwamba kuna wajasiriamali ambao walikaa chini kuchangamkia fursa baada ya kuliona tatizo la uhaba wa huduma za kibenki. Hawa waliandika program ya kompyuta (software) inayotumika kufanyia miamala.

Katika nchi tofauti tofauti; kuna mahali wanayauzia kabisa makampuni ya simu program hii na kuna mahali wanaiendesha wao moja kwa moja kwa mikataba maalumu ya kibiashara.

Walichofanya ni kuwakutanisha wadau watatu: Makampuni ya simu ambayo yanamiliki mitambo ya mawasiliano, wafanyabiashara ambao watatoa fedha za kuanzia katika benki hizi na wateja ambao ndio wahitaji wa huduma hizi.

Ndio maana mfanyabiashara unapoomba uwakala wa M-PESA, tiGO Pesa, Airtel Money nakadhalika sharti mojawapo unaambiwa uwe na mtaji kiasi fulani wa kuanzia. 

Mteja anapotumia huduma hii, kuna makato ambayo yanagawanywa kwa wakala, kwa kampuni ya simu na kwa wenye program ya kompyuta.

Kwa hiyo; alieandika programu ya benki za simu anazalisha fedha kwa kutumia mtaji wa kampuni ya simu na mtaji wa wakala wa hizi benki. Hadi sasa benki za simu zinafanya miala ya jumla ya thamani kubwa kuliko hata mabenki! Nini ninataka ukione hapa? 

Ni kwamba aliyebuni wazo la benki za simu, hakuwa na mitambo ya mabilioni, hakuwa na mtaji wa mabilioni wa kuanzia, hakuwa na ardhi kubwa na wala hakuwa na maofisi; lakini alikuwa na wazo akatumia manufaa yaliyopo katika zama mpya za mawasiliano akazalisha fedha na anaendelea kuzalisha mabilioni.

Ipo kampuni nyingine inaitwa Uber.  Kampuni hii inashughulika na biashara ya teksi. Haimiliki magari, isipokuwa inafanya kazi ya kuunganisha wenye magari (wajasiriamali) na wateja (abiria).

Hawa nao wamebuni mfumo wa kompyuta ambao unafanya kazi kwenye simu na vifaa vingine kama kompyuta.  Kampuni hii ilianzishwa nchini Marekani mwaka 2009 na mabwana wawili Travis Kalanick na Garrett Camp. 

Ipo katika nchi 53 duniani kote na katika miji zaidi ya 200. Unachofanya ni kuiweka programu waliyobuni kwenye kifaa chako; kisha unapohitaji huduma ya usafiri unabofya na taarifa inatumwa kwa Uber, hao Uber wanaituma taarifa hiyo kwa texi yeyote iliyounganishwa na iliyokaribu nawe.

Ni ndani ya muda mfupi texi inafika mahali ulipo inakuhudumia. Hawa Uber wanapata kamisheni kwa “uunganishaji” huu. 

Kampuni ya Uber hadi mwishoni mwa mwaka jana ilikuwa imekadiriwa kuwa ina thamani ya ukuaji mkubwa kuliko thamani ya kampuni ya AngloGold Ashanti.

AngloGold Ashanti ni kampuni kubwa kuliko zote za dhahabu barani Afrika na ikiwa na maelfu ya vitaru vya dhahabu kila kona duniani. AngloGold Ashanti ni matokeo ya kuungana kwa kampuni mbili za miongo mingi katia biashara ya dhahabu za AngloGold na Ashanti Goldfields Corporation mwaka 2004.

Fikiria, kampuni yenye maelfu ya vitaru tena kwa miongo mingi inazidiwa na kampuni inayofanya kazi ya teksi, tena kwa kutumia magari yasiyo yake! Kimsingi, zamani utajiri ulikuwa ni matokeo ya kumiliki ardhi na vilivyomo ndani yake lakini katika zama mpya utajiri ni matokeo ya kumiliki taarifa sahihi na kuwa na uwezo wa kuzifikisha zinakohitajika kwa wakati sahihi.

Wanachoouza Uber ni taarifa peke yake! Uber wanalipwa kwa kukujulisha ni wapi utapata usafiri na wanaenda mbali kukuitia usafiri ulipo. Hii ndio dunia mpya, huu ndio ulimwengu mpya wa biashara uliopo na unaokuja kwa kasi.

 

>>ITAENDELEA>>>

Whatsapp +255 688 726 442

1739 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!