MeruTupumzike siasa kwa leo. Nazungumzia utalii. Kwa mara ya kwanza hivi karibuni nilipata fursa ya kusindikiza mgeni kutoka Scotland aliyetembelea Tanzania na kuamua kukwea Mlima Meru mkoani Arusha.

Kilele cha Mlima Meru kina urefu wa mita 4,566 juu ya usawa wa bahari ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha yenye ukubwa wa kilometa za mraba 322. Inachukua chini ya mwendo wa saa moja kwa gari kutoka Arusha kufikia hifadhi hii ambayo pia iko umbali wa kilomita 60 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Mlima Meru ni wa tano kwa urefu katika Bara la Afrika. Kulinganisha na kukwea Mlima Kilimanjaro, ambao nimeshaukwea mara kadhaa na ambao ndiyo mrefu kuliko yote barani Afrika, inachukua muda mfupi zaidi – siku tatu hadi nne – kufikia kilele cha Mlima Meru na kurudi chini. Inachukua kuanzia siku tano hadi nane kukwea Mlima Kilimanjaro.

Pamoja na siku chache zinazohitajika kukabiliana na Mlima Meru na pamoja na kuzidiwa urefu kwa zaidi ya mita 1,300 na Mlima Kilimanjaro, taarifa nilizopata ni kuwa kukwea Mlima Meru ni changamoto kubwa zaidi kuliko Kilimanjaro. Muongozaji mashuhuri anayeongoza wageni kukwea Mlima Kilimanjaro, Pius Francis, au maarufu zaidi kama Yahoo, alinisimulia kuwa ukweaji wa Mlima Meru unahusisha miinuko mikali kuanzia siku ya kwanza mpaka kufika kileleni na kuwa mara kwa mara huwa kuna upepo wenye baridi kali unaoambatana na mchanga.

Kuongeza changamoto hiyo ya kusimuliwa nilikabiliwa na nyingine. Pamoja na kuwa hufanya mazoezi ya nguvu kwa maandalizi ya kukwea Kilimanjaro, maandalizi kwa ajili ya Mlima Meru hayakuwa mazuri. Kwa sababu hizi mbili, nilianza safari yangu na hofu kidogo kuwa ningepambana na hali ngumu.

Kundi letu lilikuwa na wageni sita likijumuisha Watanzania wawili, Waingereza watatu, na raia mmoja wa Uholanzi. Siku ya kwanza inaanza kwenye lango la Momella na wageni wanatembea mwendo wa kilomita 14 unaodumu zaidi ya saa nne mpaka kambi ya Miriakamba iliyopo meta 2,514 juu ya usawa wa bahari. Hifadhi ya Arusha ina wanyama wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na tembo, twiga, nyani wa aina mbalimbali; pamoja na nyati, mnyama ambaye ana sifa ya kushambulia binadamu. Kwa sababu ya uwepo wa wanyama wakali, wageni wote wanaokwea Mlima Meru husindikizwa na askari wanyamapori wenye silaha. Uthibitisho kuwa nyati hawako mbali ni kutapakaa kwa kinyesi chao kwenye njia za miguu zinazotumika.

Tofauti na Kilimanjaro ambako kwenye njia zote- isipokuwa ya Marangu- wageni hulala kwenye mahema, wageni wa Meru hulala kwenye nyumba zilizojengwa kwa mbao zenye vyumba vya watu wanne kwa kila chumba. Ndani ya vyumba hivyo nilipima ubaridi kati ya nyuzijoto 12 hadi 15. Kwa hali ya mlimani ni baridi ya kawaida. Kwangu ilikuwa kama vile nimelala kwenye hoteli ya kifahari. Kwa mtu ambaye hazajoea baridi hapo inakuwa fursa ya kuanza kujiuliza kilichompeleka huko mlimani.

Tofauti na nilivyoonywa na Yahoo, siku ya kwanza sikuona kama ina miinuko ya kutisha ingawa sikupenda kasi ya kutembea haraka ya askari wanyamapori aliyetuongoza. Kwangu ilizidi kasi ndogo ambayo nimezoea. Wataalamu hushauri kuwa ukweaji mlima siyo mashindano, ni jitihada za mmoja mmoja kufikia kwenye kilele kwa kasi ambayo anaimudu.

Siku ya pili mnaanza kutembea kuanzia saa 3 asubuhi kwa takribani kilomita 7 za miinuko mikubwa mpaka kambi iitwayo Saddle Hut ambayo iko kwenye urefu wa mita 3,566 juu ya usawa wa bahari.

Muongozaji wetu, John, alituarifu kuwa baada ya chakula cha mchana tungepumzika kwa muda halafu tupande kilele kimojawapo cha Mlima Meru kinachoitwa Meru Ndogo, kilichopo urefu unaozidi meta 360 juu ya kambi.

Madhumuni ya kufika kambini halafu kutoka tena kwa muda kupanda kilele kidogo cha jirani na baadaye kurudi kambini ni mchakato unaokusudia kuandaa mwili kuzoea hali ya mazingira ya kuwa maeneo ya mlimani yenye upungufu wa hewa ya oksijeni, upungufu ambao unaleta athari mbalimbali kwa wale wasio wazoefu, ikiwa ni pamoja na kudhoofisha mwili, kichefuchefu, kuvurugika kwa tumbo, na wakati mwingine hata kukosa hamu ya kula chakula. Athari hizi ni kubwa zaidi kwa wale wanaoishi kwenye maeneo tambarare yaliyo karibu na usawa wa bahari na hasa wale wanaokuwa wanakwea mlima kwa mara ya kwanza.

Wenzangu walivyoelekea Meru Ndogo mimi nilibaki kambini nikapumzika kwa sababu mbili. Kwanza, kutokana na uzoefu wangu kwenye Mlima Kilimanjaro niliamini sikuhitaji kujizoesha kuwapo mlimani. Pili, sikuwa nimefanya mazoezi ya kutosha ya maandalizi na sikuona sababu ya kupoteza nguvu zilizohitajika usiku za kunifikisha kileleni.

Safari ya kwenda kileleni inaanza saa 7 usiku na kutokana na kasi ya mwendo na kupishana kwa uwezo wa kila mmoja unaweza kufika kileleni kuanzia saa 12 alfajiri na kuendelea.

Baada ya mwendo wa saa mbili kundi letu liligawanyika kwenye makundi mawili. Mimi nilibaki kwenye kundi la nyuma pamoja na Mama Helen kutoka Scotland, daktari aliyekuwa nchini kwa ziara ya kazi na utalii. Hakuweza kutembea kwa kasi ya wale waliotangulia, lakini kasi yake ilikuwa ndogo kuliko hata ile niliyoizoea na baada ya muda mimi na mwongozaji wangu tulitangulia na kumwacha nyuma akija polepole na waongozaji wake.

Ulikuwa ni usiku wa mbalamwezi na kwa upande wa Mashariki tulikuwa tunaona Mlima Kilimanjaro. Kulipambazuka kabla ya kufika kileleni na tulipokaribia kilele tulipishana na waliotangulia wakiteremka. Wao walifika kileleni saa 12, sisi tukafika saa 1:30.

Mtanzania mwenzangu Alfred Nyoni aliyekuwa kwenye kundi lililotangulia na ambaye pamoja naye tulikwea Mlima Kilimanjaro mwaka 2014 aliniambia amewahi kuulizwa: “Ukishafika kule kileleni unapata nini?”

Hata mimi nimeshawahi kuulizwa hilo swali. Mbali na cheti kinachotolewa na Hifadhi ya Arusha kuthibitisha kuwa umefanikiwa kufika kileleni, hupati kitu. Kuna watu wengi wanaweza kuona kuwa kukwea milima siyo tu mateso, bali pia ni mateso ambayo yanagharimu pesa.

Sababu nzuri kwangu kuliko zote za kukwea mlima kama Meru au Kilimanjaro ni afya ya mwili. Maandalizi ya kukwea mlima yanahitaji programu ya mazoezi ya muda wa kati ya miezi miwili hadi mitatu ambayo yanamweka mtu yeyote kwenye hali nzuri kiafya. Unapomaliza kukwea mlima unakuwa na uchovu wa kama juma zima, lakini baada ya hapo mwili unakuwa na nguvu zaidi kuliko kawaida.

Sababu nyingine ya msingi ni umuhimu wa raia Watanzania wenye fursa na uwezo kuweka mazoea ya kutembelea vivutio ili kufahamu vyema nchi yao. Kuna raia wa nje wanaofahamu maeneo ya Tanzania vyema kuliko Watanzania.

Ni kweli vipo vikwazo vya fedha ambavyo vinazuia Watanzania wengi kutembelea vivutio mbalimbali vya nchi yao, lakini upo ukweli pia kwamba Watanzania wengi hawana desturi ya kutembelea vivutio hata vile ambavyo vipo jirani na maeneo wanayoishi. Kutembelea vivutio vilivyo jirani na maeneo tunayoishi kunapunguza gharama zinazojitokeza za usafiri na malazi.

Mamlaka mbalimbali kama Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) huhimiza utalii wa ndani ili kutoa fursa kwa Watanzania kutembelea vivutio mbalimbali. Kwa wale wenye uwezo ni fursa muhimu zinazoleta faida kwa wanaozitumia na hata kuwa kichocheo cha kukuza mapato kwa wadau mbalimbali wa sekta ya utalii na Watanzania wanaoishi katika maeneo yenye vivutio.

By Jamhuri