Lowassa pembaMwaka mmoja nyuma  kabla ya vuguvugu hili la Uchaguzi Mkuu kupamba moto,  niliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Ninachompendea Lowassa ni hiki’.

Kusema ukweli makala hiyo ilinipa nafasi kubwa ya kuzielewa vizuri siasa za nchi yetu na hasa Afrika kwa ujumla.

Nilielewa kwamba hata baada ya bara letu kujikomboa, bado tunayo safari ndefu ya kukufikia kule tunakokusema kuwa ni mahali pa demokrasia ya kweli na utawala wa sheria.

Si nia yangu kuwarudisha nyuma wasomaji wangu, ila kuanzia hapa tulipo nataka twende mbele, hasa tunapokaribia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Najaribu kuyatazama yanayohusu uchaguzi wa mwaka huu. Ninachokishuhudia kwa sasa ndicho nilichokuwa nikikiamini tangu siku zote, kwamba Lowassa ni mtu anayefaa kuwa kiongozi mkuu wa nchi yetu.

Mara nyingi wakati nikisema hivyo baadhi ya watu walikuwa hawanielewi, kuna waliokuwa wakiniona kama mtu ambaye nimeshapokea chochote kutoka kwa mtu huyo!

Lakini, watu haohao kwa sasa wananipongeza kwa kuuona ukweli ambao kwao ni kama ulikuwa bado umejificha, kila pahala kwa wakati huu wananchi wanamuimba Lowassa!

Nilichokiona kwa Lowassa tangu mwanzo ni utendaji wake wa kazi, akiwa kazini urafiki anauweka pembeni kwanza na kuujali umaridadi na ukamilifu (perfection) wa kazi inayofanyika.

Chini ya Lowassa, hakuna mtu anayeweza kufanya kazi ovyo ovyo, hasa ya umma, akitarajia kuwa kwa vile ni rafiki wa Lowassa mambo yataachiwa yaende hivyo hivyo. Hicho ni kitu ambacho hakimo katika uongozi wa Lowassa.

Kusema ukweli nchi yetu imelemazwa na mtindo huo wa kazi kuvurugikavurugika bila hatua yoyote kuchukuliwa na walio juu, kwa vile wahusika ni ndugu au marafiki wa wanaopaswa kuwasimamia.

Mfano, mtu anavuruga kazi sehemu fulani, lakini badala ya kukemewa au kuondolewa kwenye utumishi kutokana na kutokidhi viwango vya kazi husika, anahamishiwa kwingine au kupandishwa cheo!

Hali hiyo ndiyo iliyoifanya nchi yetu kudumaa kiasi hiki wakati hata baada ya muda wa nusu karne bado inaitwa Taifa changa! Hata mitume wa Mungu, ambao kiimani ni wakubwa kuliko nchi yetu, hawakuhitaji muda kama huo kutoka uchangani!

Kusema ukweli hilo ni jambo ambalo ni kama limelilemaza Taifa letu. Uzembe wa kiutendaji na uvivu wa kusimamia kazi kwa umakini kinageuka kigezo cha mtu kupandishwa cheo! Kwa Lowassa hayo ni mambo ambayo naamini yatasahaulika kabisa, yeye ni mtu anayefaa sana katika hilo.

Mifano tumeiona mingi tangu akiwa waziri wa kawaida mpaka alipofanywa waziri mkuu. Tunakumbuka alivyounusuru ufukwe wa bahari ilikotazama Hoteli ya Kilimanjaro, wakati huo akiwa waziri wa ardhi.

Kuna mtu alishaamua kujibinafsishia eneo hilo eti akajenge hoteli ya kitalii! Bila juhudi za Lowassa za kutomwangalia mtu usoni linapokuja suala linalogusa maslahi ya nchi, sasa hivi tungekuwa tunapaangalia vingine mahali hapo.

Vilevile akiwa waziri wa ardhi alitoa amri ya kuondoa mara moja uzio wa mabati uliokuwa umezungushwa kwenye viwanja vya wazi vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

 Kuna mtu aliyekuwa ameingia kwa njama za kifisadi katika eneo lile na kudai kuwa ni mwekezaji aliyetaka kuliboresha eneo hilo. Ni lazima kuna waliokuwa wamekula njama za kufanya hivyo katika mamlaka husika, lakini Lowassa bila kumwangalia mtu usoni,  akasema uzio huo uondolewe haraka iwezekanavyo.

Bila kufanya hivyo, sehemu hiyo ya viwanja vya Mnazi Mmoja ingekuwa inahesabika kama mali ya mtu binafsi kwa wakati huu. Lakini uwepo wa Lowassa ukavifanya viwanja hivyo viendelee kuwa mali ya umma.

Kwa upande huo tutaona kwamba vita ya ardhi inayoendelea kwa sasa katika maeneo mbalimbali ya nchi na kusababisha wananchi kupoteza maisha yao mara kwa mara, inatokana na ukosefu wa usimamizi wa ardhi ulio imara.

Nasema usimamizi ulio imara katika masuala ya ardhi lakini kiukweli ni ukosefu wa uwajibikaji kiujumla, au ukosefu wa watu walio makini katika utendaji kiutumishi.

Kwa upande mwingine, tulimuona Lowassa aliyoyafanya akiwa waziri wa maji. Tofauti na ilivyozoeleka hapa nchini, aliweza kuufuta mkataba wa kampuni ya kusambaza maji katika jiji la Dar es Salaam iliyokuwa ikiitwa City Water.

Kwa namna ilivyozoeleka, kwa watu wengine kampuni hiyo ingeonewa aibu ya kufutiwa mkataba wake, sana sana ingehamishwa na kupewa mkataba mwingine sehemu nyingine kama vile Mwanza, Arusha, Mbeya au kwingineko ambako yenyewe ingekutamani!

Yaani uzembe wa City Water iliouonesha hapa Dar es Salaam ndicho kingekuwa kigezo cha kuifanya kampuni hiyo ijiamulie ni wapi pengine inakutaka ikaendeleze uzembe ule ule iliouonesha jijini! Hayo ni mambo ambayo yamezoeleka hapa nchini lakini utendaji wa Lowassa ukionesha tofauti na uzoefu huo.

Vilevile Lowassa aliweza kutegua kitendawili cha kimataifa kuhusu utumiaji wa maji ya Ziwa Victoria. Hayo maji tuna mamlaka nayo kwa vile ziwa hilo kwa upande wa Tanzania ni mali yetu.

Lilipokuja suala la kuvuta maji ya ziwa hilo ili yakainufaishe mikoa iliyokuwa na uhaba wa maji kikajitokeza kikwazo cha kwamba hatukupaswa kuyavuta maji hayo kwa vile yangeathiri utiririkaji wa Mto Nile kuelekea Sudan na Misri!

Lakini Lowassa,  kwa kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu, alijibwaga uwanjani na kuhakikisha anawanyamazisha wote waliokuwa wanaleta sababu hizo ambazo hazikuwa na macho wala masikio!

Mpaka sasa watu wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga, walio mbali kidogo na Ziwa Victoria, wananufaika na maji ya ziwa hilo. Bila ya Lowassa kitu hicho kingebaki kwenye masimulizi tu.

Kawaida mchapakazi huonekana mbaya kwa walio wavivu na wazembe. Si kwamba ninayoyasema hapa yanafurahiwa na wote. Wapo wanaofanya kila njia ili Lowassa asipate kile ambacho umma wa Tanzania ungependa akipate –  uongozi mkuu wa nchi hii.

Zimefanyika mbinu za kumkwamisha kuanzia kwenye chama chake cha awali, CCM, na zikafanikiwa kwa upande huo. Lakini kwa vile alichokihifadhi Mwenyezi Mungu hakiozi, harakati za Lowassa kuwa kiongozi mkuu wa nchi hii zikahamia upande wa Upinzani. Lowassa kwa sasa ni mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Kutokana na hilo,  majungu bado yanafanyika ili kumkwamisha. Nashindwa kuelewa, hizo ni juhudi za kumkwamisha Lowassa au kuikwamisha Tanzania? Sababu Lowassa anaipenda nchi yake Tanzania kama mwananchi mwingine yeyote, ila Tanzania inamhitaji zaidi Lowassa kuliko inavyomhitaji kila mwananchi.

Katika kujaribu kumkwamisha ndipo zinatajwa hata kashfa ambazo zimeshazikwa, zinafufuliwa! Mfano ni Kashfa ya Richmond ambayo ilishasafishwa kwa njia mbalimbali.

Kwanza kabisa Lowassa alijisafisha mwenyewe, si kwa kuikubali kuwa kashfa hiyo inamhusu, ila kwa kuonesha uwajibikaji. Kawaida ya kashfa ya aina ile ni kwamba mtu akishaachia cheo anachokishikilia mambo yote yanakuwa yameisha.

La pili ni kwamba mkuu wake wa kazi, Rais Kikwete,  alilitangazia Taifa kuwa Lowassa alipata ajali ya kisiasa. Kwa hiyo naye rais aliona kuwa kashfa hiyo ilimgusa Lowassa kwa bahati mbaya tu, ndiyo maana akatumia msamiati wa ‘ajali ya kisiasa’.

Baada ya hapo katika Uchaguzi Mkuu wa 2010,  Kikwete alikwenda Monduli kumfanyia kampeni Lowassa kwa kuwaambia wananchi wa Monduli kuwa Lowassa ni jembe.

Mpaka hapo mjadala wa kumhusisha Lowassa na kashfa ya Richmond ulikuwa umefungwa. Yeyote anayetaka kuuendeleza ni lazima kwanza amuite Rais Kikwete na kumhoji kuhusu kauli zake hizo alizozitoa kuhusu sakata hilo. Kinyume cha hapo sioni kama sakata hilo lina nafasi tena katika mustakabali wa nchi yetu.

Hiyo inaleta uthibitisho wa kwamba yeyote anayemnyooshea kidole Lowassa kwa wakati huu amechelewa sana. Huu si wakati tena wa mizengwe, ni wakati wa kukiangalia kilicho bora kwa ajili ya nchi yetu.

Kwa hiyo, ingebidi tumuangalie kwa makini kasisi mmoja, Dk. Willibrod Slaa, kwa kauli zake za kutaka kuwafanya Watanzania ni ‘mazumbukuku ulimwengu uko huku’, akilitajataja neno la Richmond kwa kulihusisha na Lowassa bila ya kutaja ni kwa nini yeye aliamua kuuachia ukasisi wa Kanisa Katoliki. 

Kwa maana nyingine maneno ya Slaa ndiyo yanayoitwa ‘siasa uchwara’ ambazo aliwahi kuziona aliyekuwa Mbunge wa Igunga na kada mkubwa wa CCM, Rostam Aziz.

Kilichopo kwa sasa ni kwamba Watanzania kwa umoja wetu tujiunge pamoja na kukiangalia kile kinachotufaa sisi pamoja na nchi yetu, nacho si kingine bali ni Edward Ngoyai Lowassa.

 

0717 599 579

1588 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!