Bibi mjane Dar amlilia Makonda

Serikali ya Mtaa wa Nzasa Somelo, Kata ya Zingiziwa, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam imetumia hila kumnyang’anya shamba la ekari tatu bibi mjane mwenye umri wa miaka zaidi ya 70.

Shamba hilo ambalo limetenganishwa na Mto Nzasa, kipande kimoja kikiwa Wilaya ya Kisarawe na kingine Wilaya ya Ilala ni miliki ya Theresia Vingambudi ambaye anaishi Halmashauri ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani.

Kabla ya Serikali ya Mtaa kumnyang’anya kipande cha shamba hilo kilichopo Wilaya ya Ilala na kukigawa kwa mwingine, amelilima tangu mwaka 1984 akiwa na marehemu mume wake, Mathias Miteda, aliyefariki dunia Februari 5, 1988.

Shamba hilo walipewa kulima na Mwenyekiti wa Kijiji cha Homboza miaka ya mwishoni mwa 1970 na mwanzoni mwa 1980 likiwa msitu na kwamba mwenyekiti huyo anayemtaja kwa jina moja la Machachari aliwapa shamba hilo kama walivyokuwa wakipewa mashamba watu wengine miaka hiyo.

Bibi huyo amesema kwa miaka 35 amekuwa akilima shamba hilo akipanda mazao ya msimu na kudumu kama minazi na katika miaka yote hiyo hajawahi kutokea mtu yeyote kudai kuwa hilo ni shamba lake isipokuwa kwa miaka ya hivi karibuni, mara kadhaa walitokea watu wakitaka kulinunua.

“Lakini katika hali ya kushangaza, Mei 11, mwaka huu 2019 nilipokea wito kutoka Serikali ya Mtaa wa Nzasa Somelo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, kwamba ninashitakiwa kwa kuvamia shamba na mwanamke mmoja, Amina Mohammed Shomari, hivyo nifike katika ofisi hiyo bila kukosa,” ameeleza kwa masikitiko.

Amesema siku ya shauri mlalamikaji aliwasilisha kielelezo cha karatasi ya mauziano inayodaiwa kuandikwa wakati wa kuuziana ikionyesha kuwa alilinunua shamba hilo Novemba 11, 1984 likiwa na mazao ya kudumu kama mifenesi, michungwa na mikorosho.

Katika karatasi hiyo iliyosomwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Daniel Singo, ilionyesha kuwa mlalamikaji alinunua shamba la ukubwa wa ekari sita kwa bei ya Sh 180,000 kwa Saidi Ngemba (marehemu) lakini tangu wakati huo hakuwahi kuliendeleza ingawa alidai alifika shambani hapo miaka mitatu baada ya kulinunua na aliyemuuzia akamwambia angelikodisha kwa watu walime na akaja tena baada ya miaka minane, wakati huo aliyemuuzia alikuwa amefariki dunia hivyo hakurudi hadi mwaka huu, miaka 24 baadaye.

Wakati wa kusikiliza shitaka hilo mashahidi waliokuwepo kwa upande wa bibi Theresia ni Simon Bento, Modesta Tagasi na Binti Navalomba, ambao walieleza kuwa shamba hilo walipewa na Serikali ya Kijiji cha Homboza iliyokuwa ikigawa maeneo katika eneo la Majumba Sita, Chanika ili kufukuza wanyama wakali na lilikuwa msitu mkubwa uliokuwa na miti mikubwa na si shamba, hivyo hakukuwa na mifenesi wala mikorosho.

Bibi huyo amesema shahidi wa mlalamikaji siku hiyo aliugua ghafla hivyo hakuweza kutoa ushahidi lakini hata siku alipokuja kutoa ushahidi wake, ulitofautiana na kilichoandikwa kwenye kielelezo cha mauziano kilichowasilishwa barazani.

Amesema shahidi huyo mzee Kipalamba alidai kuwa wakati wa mauziano yeye alikuwa kijana, hivyo aliitwa kushuhudia na kwamba mlalamikaji aliuziwa shamba hilo na mzee Tenga kinyume cha maelezo ya mlalamikaji kwamba aliuziwa na mzee Ngemba.

Amesema hata baraza lilipokwenda kwenye shamba linalolalamikiwa, mlalamikaji hakuonyesha mipaka ya eneo analodai isipokuwa alimwachia kijana wake na katika eneo hilo hapakukutwa mti wowote wa kudumu kama anavyodai mlalamikaji na eneo la shamba analodai ni la ekari sita ni kubwa kuliko eneo la shamba lake ambalo ni ekari tatu.

Pamoja na tofauti hizo za maelezo na ushahidi wa mazingira na baraza kushindwa kumuuliza mlalamikaji kwa nini kwa miaka 35 yote hakufika kwenye shamba analodai ni lake, bibi Theresia amesema Serikali ya Mtaa waliamua kumnyang’anya kipande hicho cha shamba na kumpa mwenzake.

“Nasikitika sana kwamba mimi bibi mjane ninayeishi kwa kutegemea kulima mbogamboga, mihogo na mpunga katika shamba hili ninanyang’anywa wakati mashahidi wangu wanathibitisha tuligawiwa bure,” amesema Theresia kwa huzuni.

Ameongeza kuwa hata kama ingekuwa yeye na marehemu mume wake wangeuziwa isingefika hata Sh 5,000 kwa sababu kwa mwaka huo fedha hizo zilikuwa nyingi mno, hivyo inashangaza mwenzake kudai alinunua shamba mwaka 1984 kwa Sh 180,000, isingewezekana kwa wakati huo wa Mwalimu Julius Nyerere, kwani zilikuwa ni fedha nyingi.

Anamwomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amsaidie kwa kipande cha shamba lake la upande wa Ilala kwani kwa upande wa Wilaya ya Kisarawe mpaka sasa hakuna shida.

Akielezea kuhusu mgogoro huo, mtoto wa bibi huyo mjane, Stanislaus Miteda, amesema ulianza wakati yeye na mama yake walipokwenda ofisi ya Mtaa wa Nzasa Sonelo kuchukua barua ya utambulisho akiambatana na mjumbe wa eneo lilipo shamba hilo, Juma Juma.

“Tulipofika siku hiyo nakumbuka ilikuwa Mei 8, mwaka huu tukaeleza kilichotupeleka ofisini kwa mwenyekiti na mjumbe Juma akamtambulisha mama kuwa ndiye mwenye shamba, kwamba alikwenda pale kumtambulisha ili apate barua ya utambulisho wa umiliki wa shamba, akatueleza tunatakiwa kwenda Mei 13 tukiwa na Sh 40,000 za kuandikiwa barua hiyo.

“Hata hivyo baada ya kutoa maelekezo hayo kwetu, mwenyekiti akatuambia eneo lile lilikuwa na mgogoro ingawa ulikuwa haujawasilishwa rasmi, tukashangaa tukamwambia sisi tuendelee na barua ya utambulisho na kama kukiwa na malalamiko itajulikana baadaye,” ameeleza Stanslaus.

Amesema kuwa cha kushangaza kabla ya siku waliyoahidiwa, waliletewa barua ya kuitwa ofisi ya mtaa, barua anayodaiwa kuandikwa kwa haraka baada ya kufika ofisini hapo, tena iliandikwa Mei 11, 2019 kwa kusainiwa na Daniel S. Singo.

“Lakini hata hivyo, wakati tulipokwenda kuomba barua ya utambulisho, mwenyekiti aliniuliza iwapo hatukuwa na mpango wa kuliuza shamba letu, jambo linaloonyesha kulikuwa na jambo alilofahamu kuhusu shamba letu kuwa katika mpango wa kuuzwa,” ameeleza Stanslaus.

Amesema hukumu ya kesi hiyo ilitolewa Juni 19, 2019 na mwenyekiti kutoa siku 21 za kuwasilisha pingamizi ingawa barua ya hukumu waliambiwa wangeipata baada ya juma moja, yaani Jumatano Juni 26, 2019.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nzasa Somelo, Daniel Singo, amesema suala hilo limekatiwa rufaa Baraza la Ardhi la Kata ya Zingiziwa, hivyo hawezi kulizungumzia kwa undani.