Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwapo mjadala mkali kuhusu uhalali wa baadhi ya majaji na sifa zao za kuifanya kazi hiyo. Kumekuwapo madai kwamba baadhi ya majaji wameteuliwa ilhali wakiwa na rekodi mbaya za uombaji rushwa, uonevu, upendeleo na kukosa uadilifu.

Kwa upande mwingine, kuna majaji ambao muda wao wa utumishi kwa mujibu wa Katiba ulimalizika, lakini wameongezwa muda. Shaka inayojitokeza kwenye suala la kuongezewa muda, kwa mujibu wa wataalamu wa sheria, ni kwamba hatua hiyo inakwenda kinyuma cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

 

Shaka ni kwamba majaji wengi wamekuwa wakiongezewa muda bila kula kiapo, jambo linalowafanya wapoteze sifa za kuifanya kazi ya ujaji kwa mujibu wa Katiba.

 

Jambo hilo limetazamwa kwa mapana na Kikundi Kazi kilichoundwa kuchunguza suala hilo; na pia limebainishwa vema na baadhi ya majaji waliobobea na wanaoheshimika katika taaluma ya sheria. Kilichoonekana wazi katika suala hili ni kwamba kuna uvunjifu mkubwa wa Katiba.

 

Tofauti na baadhi ya watu wanavyotaka kuamini, suala hili si mtazamo wa Gazeti la JAMHURI, bali ni wa wataalamu na wanasheria waliobobea. Shaka yetu ni kwamba mamlaka inayohusika na uteuzi na nyongeza ya muda wa kazi kwa majaji, haijaonyesha kuguswa na jambo hili. Ukimya huu si mzuri hasa kwa jambo linalohusu sheria mama – yaani Katiba ya nchi.

 

Kama jambo hili lingekuwa haligusi Katiba, kwa hakika kusingekuwapo shauku kubwa ya wananchi kutaka kujua hatma yake. Kwa kuwa dhima yetu tangu awali tuliiweka wazi, yaani kusimamia ukweli na maadili katika Taifa letu, tunatoa wito kwa mamlaka ya uteuzi wa majaji kulitafakari jambo hili kwa urefu na upana wake ili hatimaye kuondoa wingu hili la uvunjifu wa Katiba.

 

Matarajio yetu ni kuona kuwa vyama vya wanasheria, wanazuoni na wadau wote wanaanza kulijadili jambo hili ili hatimaye liweze kupatiwa jibu sahihi. Litakuwa jambo la ajabu kwa mamlaka husika na vyama vya kitaaluma (sheria) kukaa kimya, ilhali jambo hili likiendelea kusumbua vichwa vya watu wengi.

 

Katiba ndiyo msingi mkuu sheria zote katika nchi. Kunapokuwa na shaka kwenye utekelezaji Katiba, ni wazi kwamba sheria nyingine zitakuwa matatani.  Aidha, tunatambua athari na changamoto zinazotukabili kwa kulivalia njuga suala hili. Yote tunayatambua, lakini kama sehemu ya Watanzania, tumeona hatuna budi kuibua suala hili kupitia njia hii sahihi ya maandishi ili wanaosoma na kulielewa waweze kupata hamasa ya kupata suluhisho lake.

 

Kuendelea kunyamazia mambo mazito kama haya, si dalili nzuri kwa ustawi wa Mhimili wa Mahakama ambao kwa kweli ndiyo injini ya haki na amani nchini mwetu. Tunaamini kwamba kuandikwa kwa habari hizi za Mahakama ni changamoto njema katika kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya kupigiwa mfano mzuri wa kuheshimu Katiba ya nchi.

Kwa pamoja tutaijenga nchi yetu.

 

By Jamhuri