Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linatuhumiwa kumuua kwa kipigo dereva wa bodaboda, Josephat Jerome Hans, baada ya kumtuhumu kwa wizi wa kompyuta mpakato (Laptop) katika nyumba ya kulala wageni ya Blue Sky jijini humo.

Tuhuma hizo zimo kwenye barua ya mama mzazi wa kijana huyo, Lusina Joseph Kiria, aliyomwandikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mwezi Machi, mwaka huu.

Kijana huyo alikamatwa Machi 4, mwaka huu, saa tano usiku eneo la Majengo na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi akiwa na wahudumu wa nyumba hiyo ya wageni ambayo pia inaendesha baa.

Mama mzazi wa kijana huyo amezungumza na JAMHURI akidai kuwa kabla ya kupelekwa kituo cha polisi mwanaye alipigwa na askari polisi maeneo mbalimbali ya mwili ikiwamo tumboni, kichwani na kusababisha apoteze fahamu.

Amedai pamoja na kumkamata mwanaye na kumpeleka kituo cha polisi kwa tuhuma za wizi wa kompyuta hiyo mpakato, Machi 6, mwaka huu, saa mbili usiku walikuta ameondolewa kituoni hapo na kupelekwa kusikojulikana na hadi sasa hajulikani alipo.

“Tarehe sita asubuhi tulimpelekea chai alikuwepo, mchana tulimpelekea chakula alikuwepo, lakini saa mbili usiku tulipompelekea chakula hatukumkuta na baadhi ya mahabusu wenzake walisema  askari wamemchukua na kuondoka naye,” amedai.

Ameendelea kudai kuwa aliyempelekea chakula aliamua kukiacha chakula hicho kwa mahabusu wenzake ili wampe mwanaye kama atarudishwa kituoni hapo, lakini hadi leo hajaonekana.

Amesema kabla ya mtoto wake kutoweka akiwa mikononi mwa polisi, dada wa mtuhumiwa huyo aliyetajwa kwa jina la Adelina Hans aliwaomba polisi wampe dhamana ndugu yake lakini polisi hao waligoma.

Katika barua yake anadai kuwa polisi walimweleza hawawezi kumpa dhamana kwa kuwa kosa lake ni kubwa na kama ni dhamana ataipata mahakamani, lakini akahoji iweje wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni waachiwe huru ilhali walikamatwa pamoja.

“Hiyo Laptop ilikamatwa kwa dada mmoja aitwaye Naomi, ambaye ni mhudumu wa Baa ya Blue Sky na ilionyeshwa na huyo dada, polisi waliikuta imeviringishiwa sweta na baadaye walimchukua mtoto wangu kijiweni kwake na kumpeleka kituo cha polisi,” amesema.
Kwa mujibu wa barua hiyo, wageni wanaodaiwa kuibiwa kompyuta yao waliomba kuachana na suala hilo na baada ya kukabidhiwa kompyuta yao waliondoka kwenye nyumba hiyo lakini polisi waliendelea kumshikilia mtoto wake.

Hata hivyo mama huyo anapingana na maelezo ya polisi kwamba mtoto wake aliwatoroka polisi wakati akiwapeleka kuwaonyesha ‘TV’, akidai maelezo hayo ni ya uongo na kulitaka Jeshi la Polisi kueleza alipo mtoto wake.

Amesema mtoto wake hakuwa na nguvu za kuwatoroka polisi wenye silaha za moto kutokana na kipigo alichopata kutoka kwa polisi ambacho kilimfanya ashindwe hata kutembea vizuri.

“Tulipompelekea chai hiyo tarehe 5, mwezi Machi alitumia muda mrefu akitembea kwa kujishikiza ukutani hadi kuja kuchukua chai, kwa sababu alikuwa hawezi kutembea vizuri, polisi walimpiga sana na hakupatiwa matibabu yoyote. Iweje leo wanasema aliwakimbia?” amehoji.

Pamoja na kuwasiliana na viongozi wa Jeshi la Polisi Dodoma kutaka kujua alipo mtoto wake kuanzia kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) na hata Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Gilles Muroto, juhudi zake zimegonga mwamba huku akiamini mwanaye mpaka sasa hayupo hai.

Barua kuhusu malalamiko ya mama huyo iliyopelekwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu, imejibiwa na uongozi wa wizara hiyo kwa niaba ya katibu mkuu huyo.

Katika majibu hayo ya katibu mkuu, mama huyo mzazi wa mahabusu huyo ameombwa kuwa na subira wakati suala hilo likifanyiwa kazi ili kubaini ukweli wake na kuahidi kumjulisha mara baada ya uchunguzi utakapokamilika.

JAMHURI limeiona barua hiyo ya Machi 25, mwaka huu, yenye kumbukumbu namba GA 102/349/01‘S’/83 iliyosainiwa na A. A. Kweka, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo inayokiri kupokelewa kwa barua ya mama huyo.

“Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi anakiri kupokea barua yako na kwamba tayari suala lako limekwishaanza kufanyiwa kazi ili kubaini ukweli juu ya jambo hilo na utafahamishwa mara tu baada ya uchunguzi kukamilika,” inaeleza barua hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, amezungumza na JAMHURI na kukiri kuwapo kwa tukio hilo, lakini hakuwa tayari kuelezea kwa undani tuhuma za askari wake kudaiwa kumuua mahabusu huyo zaidi ya kusema kwa kifupi kuwa tukio hilo linachunguzwa.

By Jamhuri