James Kunena aliyeporwa nafasi ya kuzawadiwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa mfanyakazi bora wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) alipigiwa kura na wenzake kwa kuwa alibuni vipuri vilivyotakiwa kuagizwa nje ya nchi.

Hatua yake hiyo iliwashawishi wenzake kumchagua kuwa mfanyakazi bora lakini nafasi hiyo akapachikwa Focus Sahani ambaye hakustahili nafasi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, fukuto limezidi kuibuka miongoni mwa wafanyakazi wa chini kupitia Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU), wakiwapinga baadhi ya viongozi wao wa kitaifa, akiwamo Mwenyekiti Ole Saitabau.

Gazeti la JAMHURI limeona nakala ya barua ya wafanyakazi hao dhidi ya viongozi wao kwenda kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri.

Barua hiyo ya Machi 24, mwaka huu, inamwomba Msajili kutengua nafasi ya Mwenyekiti wa TRAWU – taifa, Ole Saitabau.

“Sisi viongozi  pamoja na wanachama wa TRAWU tawi la makao makuu, Tazara – Dar es  Salaam tunaomba kwa mamlaka uliyonayo kisheria, rejea sheria ya ajira na uhusiano kazini Kifungu cha 53 umuengue ama kutengua nafasi ya Mwenyekiti wa TRAWU – taifa, Ole Saitabau…kwa muda mfupi wa uongozi wake  takriban miaka miwili tumeona wazi ameshindwa mambo kadhaa ya msingi,” imeeleza barua hiyo iliyosainiwa yenye namba ya kumbukumbu TRAWU/TZR/HQ/Vol.1/01.

Taarifa zaidi kutoka kwa wafanyakazi ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini zimeeleza kuwa si kweli kwamba viongozi wa juu wa TRAWU akiwamo Saitabau hawakushiriki kumchagua mfanyakazi bora kama walivyozungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita.

“Walishiriki na ndio wameandika barua kuleta kwa mwajiri TRC ikimtambulisha James Kunena kama mfanyakazi bora na Focus Sahani kama mfanyakazi hodari. Ushahidi wa barua upo.

“Wafanyakazi tunataka mambo mawili yafanyike. Kwanza, kamati kuu ikutane kwa dharura kuwasimamisha kazi wakati taratibu zingine zikifanyika. Pili, wafuatilie kwa Msajili (wa vyama vya wafanyakazi) kwa nini Msajili huyo hataki kuchukua hatua hata pale alipoombwa na viongozi wa matawi saba wanaowakilisha wafanyakazi wapatao 700? Kama angechukua hatua hizi mapema wala udanganyifu huo (kubadili mfanyakazi hodari atwae nafasi ya mfanyakazi bora) usingetokea. Tunapata shaka na ofisi ya Msajili juu ya suala hili. Sheria iko wazi lakini hatua hazichukuliwi,” ameeleza mmoja wa wafanyakazi.

Ilichoripoti JAMHURI

Wiki iliyopita, Gazeti la JAMHURI liliripoti kwamba kashfa imegubika maadhimisho ya kilele cha siku ya wafanyakazi, Mei Mosi, kwa mwaka huu yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya.

Kashfa hiyo imekikumba Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU). Ndani ya chama hicho, baadhi ya viongozi wake wanadaiwa kuwasilisha jina la kigogo asiyestahili kuwa mfanyakazi bora ili apewe mkono na Rais Dk. John Magufuli, kukabidhiwa cheti cha mfanyakazi bora pamoja na zawadi ya hundi.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa katika mchakato wa kumsaka mfanyakazi bora kutoka katika Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania, kinachohusisha pande mbili, wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) na wale wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), mambo yalikwenda vizuri, lakini yaligeuzwa kwa wafanyakazi wa TRL dakika za mwisho wakati shughuli za kilele cha Mei Mosi zikiendelea Uwanja wa Sokoine, mgeni rasmi akiwa Rais Dk. Magufuli.

Katika mchakato wa upigaji kura, JAMHURI limethibitishwa kuwa mfanyakazi wa kada ya chini, James Kunena, ndiye aliyeshinda kwa mujibu wa kura zilizopigwa katika siku husika ya TRAWU, lakini kwa upande mwingine, ulifanyika uchaguzi wa kumpata mfanyakazi hodari, kwa hiyo, kulikuwa na mshindi wa kundi la mfanyakazi bora ambaye ndiye anastahili kuhudhuria sherehe za kitaifa za Mei Mosi na kukabidhiwa zawadi zake husika na mgeni rasmi, mshindi wa kundi la mfanyakazi hodari, kwa kawaida, kwa mujibu wa taratibu za TRAWU huhudhuria sherehe za Mei Mosi kikanda na hukabidhiwa zawadi na mgeni rasmi wa sherehe hizo za kikanda ambazo ni ndogo ukilinganisha na zile za kitaifa.

“Mshindi wa tuzo ya mfanyakazi bora TRAWU kwa mujibu wa kura za wafanyakazi ni James Kunena, na mshindi wa tuzo ya mfanyakazi hodari ni Focus Sahani ambaye ushindi wake ulipatikana baada ya kura kupigwa kwa raundi tatu.

“Wafanyakazi wote tulijua kwamba Kunena ndiye mshindi wetu, na atakuwa katika sherehe za kitaifa Mbeya kukabidhiwa zawadi zake, jambo ambalo lingetupatia hamasa zaidi sisi wafanyakazi wa kawaida, lakini kinyume chake, akatangazwa Focus Sahani ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji TRL,” ameeleza mmoja wa watoa habari wetu aliyeshiriki mchakato wa kusaka mfanyakazi bora.

Ilivyokuwa Uwanja wa Sokoine

Dalili za mipango hiyo ya ‘kupindua’ mshindi zilianza kubainika wakati shughuli ikiendelea. Wakati wa kusoma majina ya washindi wa kipengele cha wafanyakazi bora kwa upande wa TRAWU – TRL akatajwa Focus Sahani badala ya James Kunena.

Sahani akasogea mbele ya Rais Magufuli na kukabidhiwa zawadi, lakini kutokana na hilo, Kunena akawa mkali, akahoji viongozi wake, imekuwaje?

Hili analibainisha mwenyewe Kunena katika mazungumzo yake na JAMHURI. Anasema: “Sikuelewa kilichotokea, nilisafirishwa kwenda Mbeya kwa kuwa ndiye mshindi wa kipengele cha mfanyakazi bora, nikashangaa mfanyakazi hodari ndiye anaitwa badala yangu, huyu mfanyakazi hodari alipaswa kushiriki sherehe za Mei Mosi kikanda ili apewe zawadi yake huko.

“Kutokana na hali hiyo ilibidi nimuulize Katibu Mkuu wa TRAWU (taifa) kuhusu jina langu kuondolewa kinyume cha matakwa ya wafanyakazi walionipigia kura za ushindi. Akaniambia waliwasilisha jina langu, na kwamba nisubiri wafuatilie kilichotokea.

“Focus Sahani alikwenda kushikana mkono na rais na kupewa zawadi ya mfanyakazi bora, baada ya mimi kuhoji Katibu Mkuu akaniletea bahasha ndogo ya kaki yenye hundi mbili. Hundi ya kwanza yenye shilingi milioni mbili, na hundi ya pili ya shilingi laki tano. Nikauliza, vipi kuhusu zawadi ya cheti? Akasema utapatiwa Dar es Salaam.

“Hiyo iliniumiza sana kwa kuwa washindi wote walipewa zawadi na kushikana mkono na mheshimiwa rais. Sikutaka kuhoji sana kwa kuwa viongozi hao ndio walionisafirisha kwenda Mbeya, sikuwa na nauli ya kurudi. Nimerudi Dar es Salaam, wafanyakazi wenzake wananilaumu…nimeingia katika mgogoro na wafanyakazi wenzangu walionipigia kura kuwa mfanyakazi bora kwa mwaka 2019. Wanasema nimehongwa pesa ili niondoe jina langu na kuwekwa jina la bosi wetu, Focus Sahani. Nimekanusha hili kwao lakini hawanielewi, nimewasilisha malalamiko kwa wakubwa zangu wa chama ngazi ya mkoa na kanda, wanasema wanalifanyia kazi suala hili,” amesema James Kunena.

Gazeti hili lilifanya mawasiliano na Focus Sahani ambaye alimweleza mwandishi wetu kuwa yuko katika mkutano na atumiwe ujumbe mfupi wa simu ya mkononi, lakini hadi tunakwenda mitamboni hatua zote hizo hazikuzaa matunda katika kupata maelezo yake ingawa juhudi hizo zinaendelea.

Vigogo walonga

Katika kuzungumzia kadhia hiyo, Katibu Mkuu wa TRAWU – taifa, Nashoni Mariyeri ameliambia JAMHURI kwamba wote wawili – James Kunena na Focus Sahani walistahili kupata zawadi kwa kiwango sawa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Magufuli.

Alifafanua kuwa kutokana na muda kuwa mfupi na matakwa ya kutaka orodha ya wanaotakiwa kupewa zawadi kupunguzwa, James Kunena alikubali mwenzake amwakilishe kupokea zawadi hizo.

“Walikubaliana kwamba mwenzake amwakilishe. Kila mmoja aliandaliwa zawadi ya hundi ya shilingi milioni 2.5 pamoja na cheti,” amesema.

TUCTA wazungumza     

JAMHURI lilifika ofisini kwa Katibu Mkuu wa TUCTA, Dk. Yahya Msigwa, kupata ufafanuzi wa kadhia hiyo. Pamoja na mambo mengine, JAMHURI lilitaka kufahamu, kwanza, barua iliyowasilishwa kwao kutoka TRAWU ilibainisha nani mfanyakazi bora. Pili, hundi iliyoandaliwa na cheti kiliandikwa kwa jina la nani.

“Siioni barua yao. Hawakuleta barua yenye majina hapa ofisini, walikuja Mbeya (kwenye kilele cha Mei Mosi) moja kwa moja, tulipata jina kwenye maadhimisho hayo,” amesema Katibu huyo wa TUCTA, lakini alipoulizwa kufafanua kuhusu utaratibu wa ofisi yake kupata majina ya wafanyakazi bora kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi nchini alijibu: “Mimi (Katibu Mkuu TUCTA) ndiye ninawaandikia barua vyama vyote kuwataka wawasilishe majina ya wafanyakazi bora kwa barua. Nikishapokea barua, ndipo tunaandaa vyeti na zawadi. Orodha hiyo ndiyo inayosomwa katika kilele cha maadhimisho ya Mei Mosi.”

Kuhusu suala hilo la TRAWU,m alisema jina alilopewa katika hatua za mwisho ni Focus Sahani, na kama kuna kasoro nyingine si suala la TUCTA, bali uongozi wa TRAWU.

Sherehe za kitaifa za Mei Mosi mwaka huu zilifanyika Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, mgeni rasmi akiwa Rais Dk. Magufuli.

By Jamhuri