Mwelekeo wa dunia juu ya idadi ya watu, kwa sasa hasa kwa nchi zilizoendelea [Magharibi na Mashariki] zimeachana na sera za kupunguza idadi ya watu wao badala yake zinajitahidi kadri ya uwezo wao kuongeza idadi hiyo. Hii ni baada ya kuathiriwa au kuanza kuathiriwa na madhara ya kupunguza idadi ya watu wao.

Madhara makubwa ya kupunguza idadi ya watu duniani kote, ni upungufu wa nguvukazi [watu umri kati ya 15 – 64], na watoto [umri wa miaka 0 -14] “Taifa la kesho” huku idadi ya wazee [watu wenye umri miaka zaidi ya 65] ikiwa kubwa zaidi ya makundi hayo mawili.

Pamoja na mambo mengine, hali hii ni mwiba kwa maendeleo ya nchi katika nyanja mbalimbali – kiuchumi, kijamii, na kisiasa.

Faida za kuwa na idadi kubwa ya watu ni nyingi kadri maendeleo ya nchi yanavyohusika.

Mfano, idadi kubwa ya watu (hasa watu wenye umri kati ya miaka 15 – 64) ni kwamba ndio nguvukazi katika nyanja mbalimbali kama vile, mashambani, viwandani, katika sekta za afya, elimu, uvumbuzi [sayansi na teknolojia], ulinzi na usalama [jeshi] na kadhalika.

Kuwa na watu wengi ndiyo kuwa na wasomi wengi; wataalamu wa mambo mtambuka wengi; jeshi kubwa na imara katika kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi; ndiyo kuwa na soko la bidhaa [soko la ndani] zizalishwazo mashambani na viwandani; ndiyo uwezo wa nchi kukusanya kodi kwa maendeleo yake yenyewe bila kutegemea misaada ya nje; na mengineyo mengi.

Haimhitaji mtu kuwa amemaliza darasa la saba kuweza kuelewa ni kwanini nchi kama China, yenye idadi kubwa ya watu kuliko nchi nyingine duniani; imeachana na mpango wa kupunguza idadi ya watu wake; sasa inaongeza idadi! Wachina kwa sasa wamesambaa takribani kila kona ya dunia wakifanya shughuli mbalimbali za kila aina kwa maendeleo ya nchi yao. Hawako huko waliko [duniani kote] kwa bahati mbaya; bali mpango maalumu wa nchi yao katika kujiimarisha kiuchumi, kijamii, na kisiasa ili kuendelea na kuwa taifa kubwa na lenye nguvu katika nyanja zote za maisha duniani. Ndio maana ninadiriki kusema kwamba huyu “mtu wa pili” ambaye China imeamua kumwongeza ni kwa ajili ya kuishi nje ya China [kama Tanzania] kwa maslahi ya China.

Historia sasa inatufundisha kwamba kuwa na idadi kubwa ya watu ni ‘dili’ kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa; hasa watu hao wakiendelezwa [kupewa elimu bora] na wakitumiwa vizuri nchi itapaa kimaendeleo. Kwa kweli, karibu nchi zote zenye idadi kubwa ya watu duniani ndizo ziko mbele kimaendeleo ya kila aina.

Hadi Septemba, 2018 idadi ya raia wa China ilikuwa watu 1,415,045,908 (worldometres, takwimu za Umoja wa Mataifa). China ina ukubwa wa eneo takribani kilometa za mraba 9,388,221. Ujazo wa idadi ya watu kwa kila kilometa 1 ya mraba [Population density] ni watu 151. Kiwango cha kuzaliana ni asilimia 1.6. Idadi ya wakaazi wa mjini ni asilimia 58. China, ndiyo nchi ya pili kwa kuwa na uchumi mkubwa duniani baada ya Marekani.

India ambayo ndiyo ya pili kwa wingi wa idadi ya watu duniani (watu 1,354,051,854; ina eneo la kilometa za mraba  2,973,190.

Wastani wa ujazo wa watu kwa kila kilometa 1 ya mraba ni watu 445. Kiwango cha kuzaliana ni Asilimia 2.4; huku asilimia 32 ya watu wake ndio wanaoishi mijini. Pamoja na changamoto za hapa na pale, India imekwishapiga hatua kubwa sana kimaendeleo ukiilinganisha na nchi nyingi zenye idadi ndogo ya watu, kama vile nchi za Afrika.

Marekani ambayo ndiyo ya tatu kwa idadi ya wingi wa watu duniani, kwa sasa ina watu milioni 327. Ina eneo la kilometa za mraba  9,141,420; huku ujazo wa watu kwa kilometa 1 ya mraba ni watu 36. Asilimia 83 ya watu wake wanaishi mijini. Uwezo wa watu wake kuzaa ni 1.9. Hii ndiyo nchi yenye uchumi mkubwa kuliko zote duniani, ikifuatiwa na China, kama tulivyoona.

Vietnam ina ukubwa wa  kilometa za mraba 310,070. Ina idadi ya watu ni takribani milion 96.5 (17/09/2018 worldometres]. Idadi ya watu kwa kila kilometa 1 ya mraba ni  311. Uwezo wa watu wake kuzaa ni 2.0. Vietnam ni  miongoni mwa nchi ambazo zimepiga hatua za haraka sana kiuchumi, na imeendelea mno kiteknolojia.

Ni ukweli ulio wazi kabisa kwamba karibu nchi zote maskini duniani zina idadi ndogo ya watu; hasa ukilinganisha na rasilimali zilizonazo. Mfano, ni nchi nyingi za Afrika kama Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na Sudani  Kusini. Tanzania ina idadi ndogo ya

watu ikilinganisha na ukubwa wa eneo lake la ardhi na wingi wa rasilimali asilia. Ni miongoni mwa nchi maskini duniani, pamoja na kuwa na watu wachache.

Kulingana na takwimu za [National Bureau of Statistics – NBS] Sensa ya Watu na Makaa ya mwaka 2012, Tanzania kwa sasa  ina idadi ya watu inakadiliwa kuwa million 54 lakini takwimu za Umoja wa Mataifa, Tanzania kwa sasa ina idadi ya watu takribani 59,091,392(kufikia 17/09/2018). Idadi ya wingi wa watu kwa kila kilometa 1 ya mraba ni watu 67 tu. Uwezo wa watu wake kuzaliana ni 5.2. Yaani, mwanamke wa Tanzania ana wastani wa kuzaa watoto watano tu katika maisha yake yote. Ni asilimia 31 tu ya watu ndio wanaishi mijini.

Nchi ya DRC ina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 2,267,050. Ina idadi ya watu takribani 84,004,989. Ujazo wa watu katika kila kilometa 1 ni watu 37 tu.

Uwezo/kiwango cha watu wake kuzaa ni 6.4. DRC ni miongoni mwa nchi maskini duniani: hasa ukiilinganisha na utajiri wa raslimali ilionazo.

Sudani Kusini hali ni ile ile; ni miongoni mwa nchi maskini duniani. Ina eneo la takribani kilometa za mraba 610, 952 na idadi ya watu 12,919,053. Ina uwezo wa wastani wa kuzaliana wa 5.2, sawa na Tanzania. Wingi wa watu kwa kila kilometa 1 ya eneo ni watu 21 tu, na ni asilimia 19 pekee ya watu nchini humo wanaoishi mjini.

Kwa ujumla, kama nchi ni vyema sasa tuone umuhimu wa kusisitiza kuzaliana kwa wingi kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu. Kama suala ni kwanini tuongeze idadi ya watu, mifano ya nchi za Magharibi na Mashariki inadhihirisha umuhimu wa kuwa na idadi kubwa ya watu katika nchi. Kuna msemo wa Kiingereza unaosema, “Tarakimu huwa hazidanganyi” . Hapa unajidhihirisha barabara. Kwamba, kwa namna yoyote ile iwayo; kuwa na idadi kubwa ya watu kuna faida nyingi katika nchi husika.

0762380283

Barua pepe: [email protected]

By Jamhuri