Na Mwandishi Wetu, JamuhuriMedia, Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwapatia kiasi kikubwa cha fedha za miradi ya maendeleo ambapo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kiasi cha shilingi bilioni 47.7 kati ya hizo shilingi bilioni 3.2 zililetwa kwa ajiri ya miradi iliyopo chini ya sektetarieti ya Mkoa na shilingi bilioni 44.4 zililetwa kwaajiri ya miradi inayosimamiwa na halmashauri.
Shukrani hizo amezitoa Leo wakati akifungua warsha ya kujadili tathmini ya usimamizi na utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma, iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ruvuma iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Songea.
Brigedia Jenerali Abbas alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa kutenga fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji, miundombinu na kilimo.
“Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuamini na kutupatia shilingi bilioni 47. 7 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Fedha hizi zimechochea maendeleo ya Mkoa wetu na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi,” alisema.
Alibainisha kuwa warsha hiyo inalenga kutathmini kiwango cha usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kubaini changamoto zinazojitokeza pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Pia ameipongeza TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma kwa kuandaa warsha hiyo, akisema ina mchango mkubwa katika kuimarisha uwajibikaji, uwazi na usimamizi bora wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma ,Mary Makondo alisema tathmini ya mara kwa mara ya miradi ya maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha miradi hiyo inakidhi viwango vinavyotakiwa, inaleta tija kwa wananchi na kudumu kwa muda uliokusudiwa.
alisema warsha hiyo imefanyika kwa mujibu wa sheria, ambapo alisisitizwa kuwa miradi ya miundombinu ya barabara, afya, elimu na sekta nyingine za maendeleo inapaswa kujengwa kwa ubora ili wananchi wapate huduma bora na kunufaika na uwekezaji wa Serikali.
Aidha, Makondo alieleza kuwa ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi unapaswa kufanyika kila wakati ili kubaini changamoto mapema na kuchukua hatua stahiki. Washiriki wa kikao hicho walikumbushwa umuhimu wa uwajibikaji katika kusimamia rasilimali za umma na kuhakikisha miradi inatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Warsha hiyo iliwakutanisha viongozi wa Serikali, wakuu wa taasisi, wataalamu wa halmashauri na wasimamizi wa miradi kutoka wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kujadili tathmini ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi kwa manufaa ya wananchi.
Naye Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Ruvuma Hamza Mwenda alisema kuwa mafaniko makubwa wanayoyapata Takukuru katika Mkoa huo yanatokana na ushirikiano mkubwa wanaopata katika kusimamia miradi ya maendeleo.





