BRAZA K… Msanii wa Futuhi mwenye vituko

TABORA

Na Moshy Kiyungi

Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa na waigizaji na wachekeshaji wenye vipaji tofauti vya kuvutia.

Wazee wanawakumbuka watu kama Mzee Jongo, Bwana Kipara, Mzee Jangala, Bi. Hindu, Said Ngamba ‘Mzee Small’, Bi. Chau, Pwagu na Pwaguzi waliotamba kwenye vipindi vya Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) enzi hizo.

Mabadiliko ya kiteknolojia yakaleta runinga na akina King Majuto, Jengua, Mhogo Mchungu, Alwatan Small, kundi la Ze Comedy Original likiwa na Masanja Mkandamizaji, Joti, Mpoki, Wakuvwanga na wengine wakaanza kutamba mubashara na kuvutia wengi.

Miaka ya karibuni akajitokeza Braza K na kujizolea umaarufu katika maigizo na uchekeshaji kwa kutumia lafudhi ya Kiha inayofanya watu waamini kuwa yeye ni Muha kutoka Kigoma.

Lakini jina lake halisi; Andrew Ngonyani, linampambanua wazi kabisa kwamba msanii huyu ni Mngoni kutoka Ruvuma japokuwa ni mzaliwa wa Tabora.

Braza K anasema tangu akiwa shule ya msingi alikuwa kinara wa maigizo na muziki, akitumia muda mwingi kuwachekesha wanafunzi wenzake akishirikiana na rafiki yake anayemtaja kwa jina la Jose.

Wawili hawa walikuwa wakipita madarasani na kuwaburudisha wenzao kwa vituko vya kila aina.

“Wala kipindi hicho sikujua kuwa nina kipaji cha uigizaji na hasa uchekeshaji!” anasema.

Braza K anaamini kuwa kilichosababisha asigundue haraka kipaji hicho ni mapenzi yake kwenye muziki.

“Usanii ulinipa marafiki wengi, nilijichanganya na kila mtu nikishiriki shughuli za vijana nyumbani Tabora na baadaye Kigoma nilikokwenda kutafuta maisha,” anasema.

Kwa sasa ukifika Mwanza na kumtafuta Andrew Ngonyani, utamaliza mwaka bila kumpata. Lakini ukisema unamtafuta Braza K, mara moja utapelekwa ‘Futuhi’; kundi la vichekesho linalorushwa na Star TV.

Wakati awali marafiki zake walikuwa ni wa Tabora, Kigoma na Mwanza, sasa Braza K anajulikana kila kona ya nchi kutokana na umahiri wake wa kuigiza na kuchekesha huku pia akiimba muziki wa R’n’B, Bongo Fleva na dansi.

Wakati wimbo wake uitwao ‘Hadija’ ukijikongoja kwenye anga za muziki nchini, Braza K anazo nyimbo nyingine nne za Bongo Fleva zitakazoingia mitaani wakati wowote.

Braza K alihamia Mwanza kutoka Tabora mwaka 2011 na kujiunga na kundi la Futuhi.

“Kujiunga na Futuhi kulibadili maisha yangu na kuniletea mafanikio kimaisha na kisanii. Sasa ninafahamika ndani na nje ya nchi. Haya kwangu ni maendeleo makubwa ingawa yanaweza kuwa si makubwa sana kulingana na watu wanavyoniona kwenye runinga. Hii ndiyo hali halisi ya sanaa nchini,” anasema.

Braza K anasema kwamba kazi anayofanya inamwezesha kuendesha vema maisha yake na ya familia aliyonayo ya mke na mtoto.

Anakiri kuwa sanaa haiwanufaishi sana wasanii hasa wa mikoani kutokana na watu wanaoshikilia kazi zao kuwa na nguvu na mianya ya kunufaika wao binafsi.

“Nina kila sababu ya kujivunia Futuhi kwa kuwa ndiyo imenifikisha hapa nilipo sasa na kunipatia maendeleo yote niliyonayo,” anasema Braza K.

Anawapongeza wasanii waliotengeneza njia katika sanaa ya vichekesho na kuifanya kukubalika nchini, akiwataja King Majuto, Sharo Milionea na kundi la ‘Ze Comedy’.

Anasema ushindani miongoni mwa makundi ya uchekeshaji na vipindi vinavyorushwa hewani huchochea maendeleo ya tasnia hiyo na kuongeza ubunifu kwa wasanii.

“Ifahamike kwamba kuchekesha si jambo rahisi hata kidogo! Hii ni kazi ngumu sana kuliko uigizaji wa kawaida.

“Inahitaji kufikiri namna nzuri ya kuwachekesha watu na wasikuchoke. Kazi hii inahitaji ubunifu wa hali ya juu. Mimi hukesha nikiwaza namna ya kuwafanya watu wacheke,” anasema.

Vituko vya Braza K, ikiwamo uvaaji wa shati kubwa, ufungaji vifungo ‘ndivyo sivyo’ na wakati mwingine kuonekana na hirizi kubwa ni ubunifu unaowavunja mbavu watu wengi huku ukiwa ndio utambulisho.

Kuhusu hatima ya uigizaji, Braza K anasema hiyo ni sehemu ya maisha yake na atadumu katika fani hiyo.

“Nisipoigiza huwa najiona kama mgonjwa. Yaani ninakosa raha kabisa. Naamini baadaye nitafungua kampuni yangu na kutafuta vijana wenye vipaji na kuwaajiri.

“Hii ndiyo mipango yangu ya baadaye. Hakika tutafanya kazi. Kampuni hiyo itajihusisha na uchekeshaji tu,” anasema akiweka wazi kuwa kwa sasa bado ni muajiriwa wa Futuhi.

Braza K au Tajiri wa Kigoma mbali ya usanii, ni mjasiriamali anayefuga kuku na mmiliki wa bodaboda zinazoendeshwa na vijana aliowaajiri.

Akizungumzia changamoto anazopitia, Braza K anasema: “Ni kubuni vichekesho kila siku. Ni changamoto kubwa ingawa ni ya kikazi. Nyingine ni kukatishwa tamaa na watu. Kuna wakati unakutana na mtu anakwambia eti hauna mvuto wa kuwa mchekeshaji!”

Akiwa mitaani na familia yake, Braza K anasema kuna watu huwa hawaamini kuwa ndiye yule muigizaji wa kwenye Futuhi, kitendo ambacho humfanya aangue kicheko chake maarufu anachokitumia kwenye maigizo.

“Eti kuna watu hushangaa kuona mimi ninamiliki gari. Wanadhani muigizaji ni lazima awe maskini. Hawajui kwamba ni juhudi zangu binafsi ndizo zilizonifikisha hapa,” anasema Braza K.

Anawataja Kitale na Kingwendu kama wasanii wa vichekesho anaotamani siku moja kufanya nao kazi kwa kuwa kila mmoja ana mtindo wake wa uchekeshaji.

Msanii huyu anakemea baadhi ya wasanii wakubwa wanaoigiza filamu akiwataka kuacha kukariri na kuwataka kuendelea kuigiza filamu za kawaida badala ya kuanza kuigiza filamu za vichekesho ambazo hawaziwezi na matokeo yake wanaharibu.

Braza K ameiomba serikali iwasaidie wasanii katika suala la haki zao za msingi ili waweze kujikimu katika maisha, kwa kuwa sanaa ni moja ya sekta zinazotoa ajira kwa vijana wengi nchini.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa simu namba: 078331200, 0713331200, 0736331200 na 0767331200