Katika gazeti hili la JAMHURI toleo lililopita lilikuwa na habari yenye kichwa “Udini wapasua Bunge” kutokana na hali iliyojitokeza katika kikao cha Bunge siku ya Alhamisi iliyopita, ambako mgawanyiko wa kidini miongoni mwa wabunge ulijitokeza.
  Siku hiyo wakati akiahirisha kikao cha asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, alitoa tangazo lenye kuashiria mgawanyiko wa kidini kwa kutangaza kwa kuwapo kwa mkutano wa wabunge wote wa dini ya Kiislamu uliopangwa kufanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa.
Zungu alisoma tangazo hilo wakati wa matangazo ya shughuli za Bunge na kusababisha wabunge kushtushwa na kusababisha wakae katika vikundi vidogo vidogo wakijadili tangazo hilo baada ya kutoka ukumbini.


  Baadhi ya wabunge wamemshutumu Zungu kuruhusu kusomwa kwa tangazo hilo ambalo linachochea mgawanyiko wa kidini ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria na kuleta historia mpya na ya hatari ndani ya Bunge letu.
Akizungumzia tangazo hilo lililoashiria kulea na kuendekeza udini ndani ya Bunge, Mbunge wa Mbeya Vijijini, Mchungaji Lackson Mwanjale, anasema wengi wao walipatwa na mshtuko kuona uhamasishaji huo unafanywa na Kiti cha Spika, jambo ambalo ni hatari kwa nchi.
Anasema kitendo hicho ni mwanzo wa mgawanyiko wa kidini ndani na nje ya Bunge na kwamba ni vizuri Serikali ikaliangalia hilo mapema kwa kukutana na viongozi wote wa dini ili kuweka mambo sawa, kwani nchi inakoelekea si kuzuri.


Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, anasema tangazo hilo limewachefua baadhi ya wabunge kwani baada ya kutolewa alisimama na kuomba mwongozo wa Kiti apate ufafanuzi kuhusiana na kutolewa kwake ndani ya Bunge lakini alinyimwa fursa hiyo.
  Hata hivyo, anasema ni hatari kwa Bunge linalotegemewa kuanza kuonesha mgawanyiko wa waziwazi wakati huu ambao kuna mvutano kuhusu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, huku viongozi wa dini wakitoa matamko ya mara kwa mara.
Wabunge wengi wameongea kuhusu udhaifu huo wa Bunge kuendeshwa sasa kwa misingi ya udini, jambo ambalo litaangamiza Taifa hili na kitendo hicho ni ukiukwaji wa Katiba ya nchi.


Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ilani yake ya mwaka 2005, kilitoa ahadi ya upatikanaji wa Mahakama ya Kadhi wakati huo huku wakijua kuwa Serikali haina dini na lengo lao kupata kura nyingi hata ahadi wanazojua hazitekelezeki.
Mwaka 2007 ukaibuka mzozo mkali wa udini baina ya Waislamu na Wakristo ambao walitaka kuanzishwa kwa Mahakama zao zitakazoendeshwa kwa misingi ya Biblia. Huu ni usaliti mkubwa unaofanywa na wanasiasa wabovu ndani ya nchi yetu.
Wanasiasa hawa wanaowaza manufaa yao binafsi wameishiwa na hoja za msingi na kazi yao sasa ni kuwagawa wananchi kwa misingi ya kidini kwa lengo la kuleta mfarakano na uhasama wa kidini nchini.


  Tunasema wabunge waache unafiki wao uliovuka mipaka, kwani wamekuwa wakitumia hoja za kijingajinga kudai wanapinga udini nje ya Bunge, huku wao bila aibu wakijihusisha na udini ndani ya Bunge.
Hali hii inajitokeza mara kwa mara tunapokaribia katika chaguzi zetu, wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi lakini wamefilisika kwa hoja, wako tayari kutumia udini ili waungwe mkono – iwe kwa njia halali ama haramu – wapate madaraka wayatakayo.
Kitendo alichokifanya Zungu kuonesha udini ndani ya Bunge hakikubaliki kamwe na kimetoa taswira kwamba Bunge limepoteza mwelekeo kwa kuvunja Katiba makusudi.


Tunasema matangazo ya uchochezi wa kidini yanayotolewa ndani ya Bunge si utamaduni mzuri na yanapaswa kukomeshwa mara moja, kwani kazi waliyotumwa wabunge na wananchi si kuwagawa kwa misingi ya udini ama kuhatarisha amani ya nchi hii.

By Jamhuri