SengaMimi Benjamin Thompson Kasenyenda, nafsi yangu inakataa kuwa kweli Joseph Senga eti ametutoka. Lakini kiuhalisia ndiyo hivyo, ndugu yetu Senga ndiyo ameondoka. Kwa kheri mpendwa wetu. Mcheshi na mtu wa watu.

Atakumbukwa na wengi na kwa mengi. Baadhi ni sisi marafiki pale kijiwe cha Mussa cha kusafisha viatu, Mtaa wa Samora, jirani na Idara ya Habari Maelezo, jijini Da es Salaam. Wengine ni Nyaronyo Mwita Kicheere, Issa Muhidin Issa Michuzi, Iman Madega, Saratoga, Isaac Chanzi, Mhando, Albert Thomas Kawogo na wengine wengi wenye kupenda kupita pale japo kwa muda mfupi kila siku kusafisha viatu.

Wengi wao wakifika tu, jambo la kwanza walikuwa wakiuliza vipi Msukuma amepita hapa? Ameacha ng’ombe wangapi? Senga alilipenda sana kabila lake na mwingi wa utani kwa makabila mengine. Senga ni jina maarufu kwenye tasnia ya habari. Jina lake halikuanza kuwika leo.

Aliwika sana miaka ya mwanzoni mwa 1990, pale alipoingia kupiga picha eneo lililokatazwa. Akakamatwa na kufunguliwa kesi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuendeshwa na SSP Mchomba na kuripotiwa sana na gazeti la Mfanyakazi. Lilikuwa ni gazeti maarufu sana wakati huo, hivyo lilisomwa na wengi. Alishinda kesi hiyo na kuendelea na kazi yake ya kupiga picha.

Amefanya kazi magazeti mengi nchini, yakiwemo Mtanzania na Tanzania Daima, linalomilikiwa na familia ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe chini ya Kampuni ya Free Media Limited. Hivyo hii hapa karibuni ilimlazimu kuwa karibu na Freeman Mbowe; na hapa mwishoni Edward Lowassa, ambao alikuwa nao kwenye ziara nyingi za kichama. Akipiga picha vyema ili kuujuza umma kupitia gazeti lake.

Nimeambiwa kuwa ndiye mwanzilishi wa ule mtindo wa kupiga picha inayoonesha Mhutubu pamoja na Umati kwenye picha moja mwaka 2005, kitu ambacho huko nyuma hakikuwepo.

Senga ndiye aliyepiga picha pale Nyololo, Iringa alipouawa mwandishi wa habari Daudi Mwangosi, kwani tukio lile lilitokea kwenye mkutano wa Chadema wilayani Mafinga, Iringa yeye akiwa kwenye msafara huo. Bila picha hiyo, kesi iliyomtia hatiani askari Pacificus Cleophace ingetupiliwa mbali na Mahakama.

Julai 27, 2016 ndipo ilitolewa hukumu ya Mwangosi, ambayo picha aliyopiga Senga ilisaidia utambuzi wa askari Pacificus na hivyo akatiwa hatiani kwa mauaji ya bila kukusudia, Pacificus akahukumiwa kifungo cha miaka 15 jela, juu ya miaka minne aliyokaa mahabusu. Senga ni jina kubwa hilo.

Mara ya mwisho kukutana naye ilikuwa kwenye taasisi ya Moyo ya JK pale Muhimbili mapema mwaka huu. Tulijikuta tunahudumiwa na daktari mmoja. Aliniambia kuwa amekuwa akitibiwa pale kwa zaidi ya mwaka. Akasema anaangalia uwezekano wa kwenda nje ya nchi kwa matibabu.

Nikamwambia mimi ndo kwanza ninaanza matibabu ya moyo. Akanitania: “Ukianza tu kuja kutibiwa hapa, panakunogea, halafu unajikuta unakuja mara kwa mara, hata kama huumwi. Si unaona walivyopanogesha na AC kabisa? Uliona wapi hospitali ya Serikali ina AC kwenye ukumbi wa kusubiri kwenda kwa daktari?” Tukacheka.

Baada ya matibabu, nilimwambia anaweza kunisubiri kidogo nichukue dawa, ili nimsogeze kwake Sinza maeneo ya White Inn. Akasema: “Marufuku kunipa hivyo vilift vyenu siku hizi, vinaua. Ndo maana madokta wamenilazimisha nitembee kwa miguu nusu saa kila siku.” Akaniaga.

Kumbe ndiyo anaondoka hivvyo. Kwakheri ndugu Senga. Mimi nimejifunza mengi kwako, likiwemo la kupunguza matumizi ya vyombo vya usafiri. Safiri salama. Tembea mpaka huko kwa Mola wako. Nasisi tunazidi kutembea.

Tunafanya mazoezi ili kutetea uhai wetu. Lakini siku ikifika tutatembea kukufuateni huko mliko wewe na Mwangosi uliyempiga picha pamoja watu wengine kadhaa. Lala pema peponi Kiongozi.

Senga alifia nchini India ambapo mwili wake ulisafirishwa na kurejeshwa nchini, ambapo baadaye ulilazwa nyumbani kwake Sinza kabla ya Jumapili ya Julai 31, 2016 kufanyiwa ibada ya maziko na kusafirishwa kwenda mkoani Mwanza kwa mazishi.

Jijini Dar es Salaam, ibada hiyo ilihudhuriwa na Waziri Mkuu (mstaafu) na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa, Waziri wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga.

Maziko ya Senga yalitarajiwa kufanyika jana. Senga ameacha watoto saba na mjane.

 

Mwandishi wa makala hii, amejinadi kuwa ni msomaji mzuri wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kupitia Na. 0787 383 067.

1474 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!