fidel-castro1Tawala za kijamaa zilianguka kote duniani, lakini Castro aliendelea kupeperusha bendera nyekundu karibu na maadui wake wakubwa, Marekani.

Kiongozi huyo mwenye utata alisifiwa na wafuasi wake kama kiongozi wa ujamaa, askari mwanasiasa ambaye aliirejesha Cuba mikononi mwa watu.

Lakini alikabiliwa na shutuma kwa kuwazima wapinzani wake kwa njia ya mateso na kwa kuwa na sera ambazo ziliporomosha uchumi wa Cuba.

Fidel Alejandro Castro Ruz alizaliwa Agosti 13, 1926  nje ya ndoa ya familia ya mkulima bwenyenye, Angel María Bautista Castro Argiz, ambaye alihamia Cuba kutoka Uhispania.

Mama yake, Lina Ruz González, alikuwa kijakazi aliyefanya shughuli za shamba ambaye baadaye alikuwa mpenzi wa baba yake, na baada kuzaliwa kwa Fidel, ndiyo wakaoana. 

Castro alisoma katika shule ya Kikatoliki mjini Santiago kabla ya kujiunga na chuo kinachoendeshwa na makasisi wa Jesuit- kilicho El Colegio de Belen jijini Havana.

Hata hivyo, alishindwa kimasomo, na badala yake alipendelea kutumia muda wake mwingi katika shughuli za michezo.

Ilikuwa wakati anasomea sheria katika Chuo Kikuu cha Havana katikati ya miaka ya 1940 ndipo alipokuwa mwanaharakati wa siasa, na kuimarisha ujuzi wake wa kuzungumza hadharani.

Malengo yake yalikuwa ni pamoja serikali ya Cuba, iliyoongozwa na Ramon Grau, ambayo ilikumbwa na shutuma za ufisadi wakati huo. Ghasia za maandamano ya upinzani ziligeuka kuwa maisha ya kila siku na Castro akajitapa akilengwa na polisi.

Pia alikuwa miongoni mwa watu waliopanga njama za mapinduzi ya kumg’oa mamlakani Rafael Trujillo, kiongozi wa mlengo wa kulia wa Jamhuri ya Dominica, lakini jaribio hilo lilishindwa baada ya Marekani kuingilia kati.

Mwaka 1948 Castro alimuoa Mirta Diaz-Balart, mwanae mwanasiasa tajiri nchini Cuba. Mbali na kumtia msukumo wa kujiunga na wasomi wa nchi, aligeuka kuwa na itikadi za  Kimaxist.

Aliamini matatizo ya Cuba ya kiuchumi yalikuwa ni matokeo ya ubepari usioweza kudhibitiwa ambao unaweza kutatuliwa tu kwa mapinduzi.

Baada ya kuhitimu masomo, Castro alizindua shughuli za kisheria lakini zilishindwa kufanikiwa na aliendelea kuingia katika mzozo wa madeni.

Alisalia kuwa mwanaharakati wa kisiasa, akishiriki katika misururu ya maandamano ya mara kwa mara ya ghasia.

Mnamo mwaka 1952, Fulgencio Batista alifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyomg’oa madarakani Rais wa Cuba, Carlos Prío.

Sera ya Batista ya uhusiano wa karibu na Marekani na kukandamiza mashirika ya kijamaa vilikuwa pingamizi kwa kwa imani za kimsingi za siasa za Castro.

Baada ya kushindwa kisheria, Castro alibuni shirika lililoitwa The Movement, lililoendesha shughuli zake kisiri kwa lengo la kuung’oa madarakani utawala wa Batista.

Cuba palikuwa mahala pa watu matajiri kujivinjari, na nchi iliongozwa na kiasi kikubwa na magenge ya wahalifu. Ukahaba, wacheza kamari na walanguzi wa mihadarati vilikithiri.

Julai 1953, Castro alipanga shambulio dhidi ya kituo cha kijeshi cha Moncada akaribu na Santiago ili kupora silaha kwa ajili ya kuzitumia katika harakati za kivita.

Shambulio lilishindwa na wanamageuzi waliuawa ama kukamatwa. Castro alikuwa mmoja wa wafungwa kadhaa waliofikishwa mahakamani Septemba 1953.

Castro alitumia muonekano wake mahakamani kutangaza maasi yaliyotekelezwa na jeshi, jambo ambalo baadaye lilimpatia umaarufu, hususan miongoni mwa waandishi wa habari wa kigeni ambao waliruhusiwa kuhudhuria kesi hiyo.

 Guerrilla warfare (upiganaji vita wa msituni)

Alihukumia kifungo cha miaka 15 jela. Baadaye aliachiliwa huru kufuatia tangazo la huruma la jumla mwezi Mei 1955 baada ya kutumikia kifungo hicho kwa miezi 19 pekee katika mazingira bora kiasi.

Katika kipindi hiki kifupi gerezani alimtaliki mkewe na kujiimarisha zaidi katika sera za Kimaxist.

Kutokana na Batista kuendelea kuwakamata wapinzani wake, Castro alitorokea Mexico kuepuka kutiwa nguvuni. Huko alikutana na mwanamageuzi kijana aliyeitwa Ernesto ‘Che’ Guevara.

Novemba 1956, Castro alirejea Cuba akiambatana na wanajeshi 81 kwenye ndege iliyokuwa na uwezo wa kuwabeba watu 12 pekee.

Makao makuu ya chama yalitafuta hifadhi katika milima ya Sierra Maestra. Kutoka kwenye ngome hii Castro alizindua vita ya msituni dhidi ya utawala wa Havana.

Januari, 1959, Jeshi la waasi likaingia katika mji mkuu wa Cuba, na Batista akatoroka. Mamia ya wafuasi wa zamani wa Batista walinyongwa baada ya kesi ambazo wageni wengi waliziona kuwa hazikuwa za haki.

Castro alijibu kwa kusisitiza kwamba “Haki ya mageuzi haina misingi ya kisheria ya kubadili tabia ama mawazo, bali inazingatia uwajibikaji wa maadili.”

Serikali mpya ya Cuba iliahidi kurejesha ardhi kwa watu na kulinda haki za maskini. Lakini mara moja serikali ilianza kulazimisha mfumo wa chama kimoja cha kisiasa. Mamia ya watu walitupwa jela na kwenye kambi za kutumikishwa kazi za suluba kama wafungwa wa kisiasa.

Maelfu ya Wacuba hususan wenye kipato cha kadri wakalazimika kuikimbia nchi yao. Castro alisisitiza kwamba fikra zake zilikuwa ni bora zinajali kwanza maslahi ya watu wa Cuba.

“Hakuna ujamaa au umaxist , bali uwakilishi wa demokrasia na haki ya kijamii katika mpango bora wa uchumi,” alisema wakati huo.

Mwaka 1960, Fidel Castro aliwapatia uraia Wamarekani wote waliokuwa wanamiliki biashara katika kisiwa hicho.

Kujibu hatua hiyo, utawala wa Washington ulimwekea vikwazo vya kibiashara vilivyotarajiwa kudumu kwa karne ya yote ya 21.

Castro alidai kuwa alilazimishwa kuingia katika mikono ya muungano wa Usovieti na kiongozi wake, Nikita Khrushchev, ingawa baadhi ya wachanganuzi walisema aliingia katika muungano huo USSR kwa utashi wake mwenyewe.

Iwe sababu yoyote ile, taifa la Cuba liligeuka kuwa uwanja wa mapamabano ya vita baridi vya dunia.

Mwezi  Aprili 1961, Marekani ilijaribu kuipindua serikali ya Castro kwa kuwapatia mafunzo wanajeshi binafsi wa Cuba waliokuwa ukimbizini ili kuvamia kisiwa hicho.

Katika mwambao wa Pigs, vikosi vya Cuba vilikabili majeshi ya uvamizi, na kuwaua wengi huku 1,000 wakikamatwa. Fidel Castro alikuwa ameonja madaraka kwa njia ya damu kwa hivyo asingeweza kuwasamehe.

Mwaka mmoja baadaye, ndege za uchunguzi za Marekani ziligundua makombora ya Usovieti wakati zilipokuwa njiani kuelekea maeneo ya Cuba.

Dunia ilishtushwa na uwezekano wa kutokea vita ya nuklia. “Msururu wa maeneo yenye makombora ya masafa marefu ya kivita sasa yanaandaliwa katika kisiwa kilichofungwa. Lengo la ngome hizi za makombora haliwezi kuwa jingine zaidi ya kutoa uwezo wa kufanya mashambulio ya nuklia dhidi ya mataifa ya Magharibi,” alionya Rais John F Kennedy.

Mataifa yenye nguvu duniani yalibaki kushuhudia kinachoendelea lakini ni Rais Khrushchev pekee ambaye aliweza kuchukua hatua kwanza na kuondoa makombora yake nje ya Cuba baada Marekani kukubali kuondoa kisiri silaha zake kutoka Uturuki.

Fidel Castro, hata hivyo, alikuwa tayari ni adui namba moja wa Marekani. Maafisa wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) walijaribu kumuua, katika kisa kilichojulikana kama Operation Mongoose, ambapo mbinu mojawapo ilikuwa apewe sigara iliyokuwa imesheheni vilipuzi.

Mbinu nyingine zilikuwa za kushangaza, ikiwamo mojawapo ya kumfanya ndevu zake zianguke ili kumfanya awe na sura ya kutoheshimika.

Muungano wa Usovieti ulimwaga pesa ndani ya Cuba. Ulinunua mavuno ya sukari yanayozalishwa kisiwani humo na meli zake kurejea zimesheheni na bidhaa nyingine, kama vile chakula kilichokuwa kinahitajika ili kukabiliana na vikwazo vya Marekani vya biashara.

Licha ya utegemezi wa msaada kutoka mataifa ya Usovieti, Castro aliiongoza Cuba kuwa taifa jipya lisilokuwa na mafungamano yoyote.

Hata hivyo, aliegemea hasa Afrika, ambako alituma majeshi kuunga mkono wapiganaji wa msituni waliokuwa na sera za Kimaxist katika nchi za Angola na Msumbiji.

Katikati ya miaka ya 1980, hata hivyo, siasa za dunia za maeneo zilibadili mkondo wake. Ilikuwa ni enzi ya Mikhail Gorbachev, sera za Glasnost na Perestroika, na zilidhihirika wazi kuwa kinyume na mageuzi ya Castro.

Utawala wa Moscow ukakata uhusiano wa kiuchumi mara moja na Cuba kwa kukataa katakata kununua sukari ya Cuba.

Akiwa bado chini ya vikwazo vya Marekani na kukatwa kwa huduma muhimu za mataifa ya Soviet, uhaba wa kudumu wa bidhaa na ukosefu wa akiba ya bidhaa vilidhihirika ndani ya Cuba.

Jazba ilipanda huku misururu ikiendelea kurefuka.

Taifa ambalo Fidel Castro aliita lililoendelea zaidi duniani, hali ya maisha ilikuwa mbaya.

Katika kati ya miaka ya 1990, Wacuba wengi walikuwa wamechoshwa na hali nchini mwao. Maelfu walianza kutoroka kupitia njia ya maji hadi Florida wakiwa na ndoto ya kuishi maisha bora zaidi. Wengi walikufa maji, lakini ilikuwa kura tosha ya kutokuwa na imani na Castro.

Hata hivyo, Cuba ilirekodi baadhi ya mafanikio ya kufurahisha ndani ya nchi. Huduma bora za matibabu zilitolewa bure kwa wote, na viwango vya vifo vya watoto wachanga vililinganishwa na vile vya mataifa tajiri duniani.

Katika miaka iliyofuata, Castro alionekana mtulivu. Mwaka 1998 alitembelewa na Papa John Paul II, jambo ambalo halingeweza hata kufikiriwa miaka mitano ya awali.

Wakati huo Papa aliilaumu Cuba kwa ukiukaji wake wa haki za binadamu, na kumuaibisha Castro mbele ya vyombo vya habari vya dunia.

Fidel Castro alikuwa amebuni utambulisho wake kama mjamaa wa Caribbean ambao kwa miaka kumi iliyopita, alilazimika kuukumbatia, pole pole alianzisha mabadiliko machache ya biashara huria ili kulinda mageuzi yake.

Julai 2006, siku chache tu kabla ya maadhimisho ya mwaka wake wa 80 wa kuzaliwa, Castro alikabidhi mamlaka ya muda kwa Raul baada ya kufanyiwa upasuaji wa dharura wa utumbo.

Afya yake iliendelea kudhoofika. Mapema mwaka 2008, Castro alitangaza kwamba hatakubali nyadhifa za urais na amiri jeshi mkuu katika mkutano mkuu wa kitaifa.

Katika barua iliyochapishwa katika gazeti rasmi la kijamaa, alikaririwa akisema kuwa: “Ni kudanganya nafsi yangu kuchukua majukumu yanayohitaji kutembea na kujitolea, wakati siko katika hali ya kimwili inayoniruhusu kufanya hivyo.”

Alijiondoa kwa kiasi kikubwa katika maisha ya umma, huku akiandika taarifa zilizochapishwa katika vyombo vya habari vya kitaifa chini ya kichwa cha habari…Tathmini ya maisha ya amir Fidel.

Alijitokeza tena Julai 2010, alipoonekana mbele ya umma tangu augue, akiwasalimia wafanyakazi na kuhojiwa na televisheni ambapo alijadili kuhusu hali ya wasiwasi baina ya Marekani na Iran pamoja na Korea Kaskazini.

Mwezi uliofuatia Castro alitoa hotuba yake ya kwanza katika bunge la taifa baada ya miaka minne, akiitaka Marekani kuacha kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran au Korea Kaskazini akionya kutokea kwa maafa ya nyuklia ikiwa uhasama utazidi.

Alipoulizwa ikiwa Castro anaweza kuingia tena katika serikali, waziri wa utamaduni, Abel Prieto, aliiambia BBC: “Nadhani wakati wote amekuwa katika maisha ya siasa za Cuba lakini hayuko serikalini. Wakati wote amekuwa makini kwa hilo. Vita yake kuu ni kuhusu masuala ya kimataifa.”

Tangazo la Rais Obama la Desemba 2014 la mwanzo wa kumalizika kwa vikwazo vya Marekani vya biashara na vinginevyo, lilionekana kama matumaini katika kile kilichokuwa uadui wa nusu karne wa uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Castro aliafiki hatua hiyo aliyoielezea kuwa “hatua nzuri ya kutafuta amani ya kikanda”, lakini hakuiamini serikali ya Marekani.

Wakati Wacuba wengi bila shaka hawakumpenda Castro, wengine walimpenda kwa dhati. Walimuona kama Daudi  ambaye aliweza kukabiliana na Goliath wa Marekani.

 

Imetafsiriwa kutoka BBC

By Jamhuri