Historia hutokea, na watunza kumbukumbu huziandika. Mbunge (sasa marehemu) wa Ulanga Mashariki (CCM), Theodos Kasapila, kila lilipotokea jambo kubwa alikuwa akisema; “Haijapata kutokea”. Hakika ni vyema na haki, nikiazima maneno ya Kapteni Kasapila kusema Fidel Castro, aliyekuwa Rais wa Cuba, ni kisiki cha mpingo aliyewashinda Wamarekani.

Sitanii, haijapata kutokea. Castro ni mwanasiasa wa aina yake. Alizaliwa Agosti 13, mwaka1926 na amefariki dunia Ijumaa, Novemba 26, 2016, ila ameacha hitoria. Marais 11 wa Marekani, kwa nyakati tofauti walifanya mbinu za kumuua Castro, lakini ilishindikana. Ilifika mahala wakamwona kama mtaalam wa ndumba, na alizua mgogoro mkubwa ndani ya vyombo vya ulinzi na Usalama vya Marekani kwa kushutumiana kuwa pengine alikuwa na mawakala wake ndani ya CIA kwani kila walichopanga alikifahamu kabla hakijatekelezwa.

Historia ya Castro ni ndefu, lakini nijitahidi japo kwa ufupi kueleza umaarufu wa Castro duniani ulitokana na nini. Oktoba 10, 1948 Wa-Cuba walimchagua Rais wa Kwanza mzawa, Carlos Prio Socarras. Socarras alianza kujenga Cuba ya kizalendo, Cuba yenye watu wanaojitambua. Alianza kujenga uchumi, akapendwa na watu wake.

Kwa bahati mbaya, Wamarekani hawakumpenda Socarras. Walifanya mbinu kama ilivyokuwa utamaduni wao wa wakati huo, wakamwezesha Fulgencio Batista kumpindua  Socarras, Machi 10, 1952, ikiwa ni miezi mitatu kabla ya uchaguzi unaofuata. Hata hivyo, Wamarekani hawakumuua Socarras, kama kuuma na kupuliza vile, wakampa hifadhi ya kisiasa katika Jimbo la Florida.

Hadi mwaka 1492, wakati Muitaliano, mchunguzi Christopher Columbus alipofika Cuba na kugundua kisiwa hiki, wenyeji walikuwa na vinasaba vya damu na Marekani. Umbali uliopo kati ya Havana (Cuba) na Miami, Marekani ni wastani wa kilomita 350. Hawa walikuwa wakitembeleana na wakati mwingine kuwa na udugu wa damu. Ikumbukwe wote walikuwa katika ukanda wa kulima miwa.

Sitanii, baada ya ugunduzi huu, Hispania ilianza kuitawala Cuba. Cuba iliendelea kutawaliwa na Hispania hadi mwaka 1762, ilipotolewa kwa muda kwa Uingereza, pale Hispania ilipobadilishana na Uingereza koloni la Florida, Marekani. Baadaye Uingereza iliirejesha Cuba kwa Hispania, baada ya Marekani kuwa imejipatia uhuru mwaka 1776 na wakati huo yalikuwa yameanza mapinduzi ya viwanda, huku Uingereza ikiongoza kampeni dhidi ya Ukoloni.

Castro hakuridhishwa na hatua ya Batista kumpindua Socarras. Ndugu wawili, Raul na Fidel Castro, walikimbili uhamishoni Mexico, ambapo wakiwa katika Jiji la Mexico, walikutana na Muagentina, daktari mwanafunzi, Ernesto “Che” Guevara, aliyegeuka mwanamapinduzi wa kweli baada ya kusoma na kuingiwa kwa kina falsafa za Karl Marx.

Baadaye wakiwa Mexico, Castro kwa kusaidiwa na mfanyabiashara ya silaha, anayefahamika kwa jina moja la Antonio, kwa msaada wa fedha alizokusanya Batista kutoka kwa wakazi wa Florida waliopinga kupinduliwa kwa Socarras, waliweza kununua boti yenye uwezo wa kubeba watu 12 kwa gharama ya dola 15,000, inayofahamika kama Granma. Kwa Kiingereza Granma maana yake ni Bibi. Boti hii waliitumia kuwasafirisha Castro, Che Guevara, Raul na wapiganaji wengine ambao jumla yao walikuwa 82. Hadi leo imewekwa kwenye makumbusho na inalindwa.

Katika moja ya vitabu vyake, Che Guevara aliyekuwa mwanamapinduzi mashuhuri duniani aliyeshiriki hadi mapinduzi ya Congo, anasema iliwachukua siku 7 kukatisha Bahari ya Atlantic hadi Havana, katika msitu uliokuwa kando mwa bahari ukiwa umejaa mikoko. Baada ya hapo iliwachukua siku tatu za njaa, kuzimia, kumwagiana maji na kuomba chakula kufikia nchi kavu halisi.

Wanapinduzi hawa wakiongozwa na Castro walinaza vita ya msituni kumwondoa madarakani Batista waliyeamini alikuwa kibaraka wa Marekani. Marekani ilitumia kila mbinu kumlinda Batista, lakini wakati huo Cuba ikisaidiwa na Urusi, iliwazidi nguvu Wamarekani. Ni wakati huu pekee, aliyekuwa Rais wa Marekani, Dwight D. Eisenhower alipoteza umaarufu na kushindwa uchaguzi wa mwaka 1960.

Sitanii, mwaka 1959 Castro alifanikiwa kumpindua Batista. Kwa Wamarekani walijihisi kudhalilishwa. Rais Eisenhower, aliamua kuwapa mafunzo kwa siri askari wanamgambo wa Cuba 1,400 waliokuwa uhamishoni akawasaidia ndege vita na vifaa vya kijeshi kwenda kupambana na Castro mwaka 1961 chini ya uongozi mpya wa Rais wa Marekani, John F. Kennedy.

Kennedy na wafuasi wake walishuhudia cha moto. Hawa askari 1,400 walipoingia Cuba tu, ndani ya siku 1, majeshi ya Cuba yalikwishaua askari 100 wavamizi na kuangusha ndege zote, wakaharibu vifaa vya mawasiliano walivyovitegemea na siku ya pili askari 1,200 wakajisalimisha na kusema ukweli kuwa walitumwa na Marekani. 100 waliosalia inaaminika baadhi walikimbia wakarejea Florida, Marekani, ambako vizazi vyao bado vinaishi hadi leo. Wengine waliliwa pomboo (shark).

Jaribio hili ka kuivamia Cuba Aprili, 1961 lilipata pigo la mwaka. Ingawa Castro alimpindua Batista akiwa na askari 82 tu, alifanikiwa kutokana na ukweli mchungu. Wananchi wa Cuba walikuwa na njaa, maskini wa kutupwa, hawakuwa na elimu, huduma za afya zilikuwa mgogoro, hawakuwa na maji wala heshima yoyote mbele ya jamii ya kimataifa.

Wamarekani waliwapenda Wacuba kwa kuwa kisiwa hiki kilionekana mahala salama kwa utalii na uwekezaji, ambapo kwa watu wa Cuba kutokuwa na elimu, iliwawia rahisi kuwekeza mitaji yao na wakalipa mishahara kidogo. Masilahi ya Marekani ndani ya Cuba yalikuwa ya kibiashara zaidi kuliko huduma za kibinadamu.

Sitanii, Castro alikuwa kiongozi wa kweli aliyediriki kuwambia Wacuba kuwa umaskini wao unatokana na Marekani. Hili hawakulipenda. Wamarekani walijiandaa kufanya kila mbinu kuhakikisha Castro anaondoka madarakani. Aliwahudhi zaidi wa Marekani, pale walipobaini mwaka 1963 kuwa alikuwa ameshirikiana na Rais wa Urusi wa wakati huo, Nikita Khrushchev kupeleka makombora 80 ya nyuklia nchini Cuba.

Rais Khrushchev aliamini kuwa hatua ya kuwa na Castro kama mshirika wa karibu, ingesaidia kuijenga hofu Marekani na kuizuia adhima yake ya kuivamia Cuba. Marekani kwa upande wake kama nilivyotangulia kusema hapo juu, iliamini Castro kwa matendo ya kuwafungua macho aliyokuwa akifanya kwa wananchi wake, angeweza kuwaambukiza tabia hiyo viongozi wengine wa nchi za Amerika ya Kusini wakaanza kutaifisha mashirika na biashara za Marekani zilizopo nchini mwao.

Si hilo tu, Wamarekani walimwona Castro kama mfano mbaya, uliolenga kusambaza siasa ya Ujamaa katika Bara la Amerika, hali ambayo ingedhibiti Ubepari. Mzozo ulizidi kuwa mkubwa na umaarufu wa Castro ulizidi kuongezeka duniani. Mwaka 1962, Marekani ilifanya mazoezi yaliyohusisha askari 40,000 katika visiwa vya Caribbean, bila kutaja ni nchi ipi, ila mazoezi yao yalihusu jinsi ya kumwondoa madarakani Rais wa nchi ambayo ni kisiwa; Castro alijua kuwa mbaya wao ni Cuba pekee.

Mzozo kati ya Urusi na Marekani kupitia Cuba uliendelea kuwa mkubwa. Marekani ilijiandaa kuivamia Cuba, kumuondoa Castro madarakani na hadi Agosti, mwaka 1962 tayari CIA ilikuwa imefanya majaribio nane ya kumuua Castro bila mafanikio. Kwa muda wa miaka 90 aliyoishi duniani, Marekani ilifanya jumla ya majaribio ya kumuua 648 bila mafanikio. Ilipofikia hatua hiyo, mbali na kuiwekea vikwazo vya kiuchumi, Oktoba 22, 1962 Marekani iliweka kizuizi (barrier) majini kuzuia meli zote za Urusi zisiende Cuba.

Sitanii, hatua hii ilimwaga mafuta katika moto uliokuwa unawaka tayari. Oktoba 23, 1963 CIA walimpelekea taarifa Rais Kennedy kuwa meli 27 za Urusi, zilikuwa zinakaribia kwenye kizuizi na maandalizi ya kutumia silaha za nyuklia yalikuwa tayari hivyo wakaomba amri yake kutumia silaha hizo. Kwa muda shughuli zilisimama duniani. Wakakumbuka madhara ya Hiroshima na Nagasaki.

Mawasiliano ya haraka, kuvujisha taarifa za kiinteligensia makusudi kama sehemu ya kitisho, ilikuwa vyote vinakwenda kwa kasi ya mwanga, huku wanadiplomasia wakirejesha kila walichopata kwa Rais wa kila nchi. Dakika chache kabla ya Rais Kennedy kutoa amri ya kutumia silaha za nyuklia, Rais wa Urusi Khrushchev, alipewa taarifa za kiinteligensia zisizotiliwa shaka kuwa Marekani ilidhamiria kuzilipua meli zake 27, na kwa kuwa meli hizo zilikuwa na silaha za nyuklia, Khrushchev akaamuru meli hizo zikate kona na kurejea Urusi.

Askari wa Marekani waliokuwa na jukumu la kubofya kitufe cha nyuklia, jasho lilikuwa linawatoka kila unyoya, kwa kufahamu madhara makubwa kwani dunia ingeangamia siku hiyo ya Oktoba 23, 1962. Wanafahamu fika madhara ya silaha za nyuklia kwani hadi leo maeneo yalikopigwa mabomu ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan.

Takwimu zinaonyesha Hiroshima walikufa watu zaidi ya 150,000 huku Nagasaki wakifariki watu 75,000 katika siku ya kwanza lilipodondoshwa bomu la nyuklia. Ukiacha maelfu ya watu waliokufa, bado hadi leo wanazaliwa watu wenye ulemavu na samaki wa eneo la maji yalipoangukia mabomu wana sumu ukiwala unakufa.

Hatua ya Urusi kurejesha nyuma meli zake, ilitoa fursa kwa Khrushchev na Kennedy kuanza mazungumzo ya haraka. Khrushchev alitoa masharti kwa Marekani kuondoa mabomu yake na vifaa vyote vya kijeshi nchini Uturuki, vilivyokuwa vinatishia usalama wa Urusi, na Marekani ikatii. Kwa upande wake, Marekani ikaitaka Urusi kuondoa mabomu yote ya nyuklia yapatayo 80 nchini Cuba, na Urusi ikatii.

Enzi hizo zilikuwa za vita baridi. Marais wa Marekani na Urusi walikuwa hawazungumzi ana kwa ana, zaidi ya kupeana ujumbe kupitia mabalozi wao. Kuanzia mwaka 1963, wakakubaliana kuwa wanazungumza katika masuala wanayodhani yana masilahi kwa dunia. Tangu wakati huo, Urusi na Marekani wamekuwa na utamaduni wa marais wao kupigiana simu bila masharti na kuzungumza lolote watakalo.

Si hilo tu, Marekani aliingia mkataba wa kutoivamia Cuba milele. Hata hivyo, mshindi wa urais Donald Trump, wakati wa kampeni zake ameahidi kupitia upya mkataba huo na ikibidi ataivamia Cuba. Kabla hajatekeleza ndoto yake Castro amefariki. Castro alikuwa moto wa kuotea mbali. Madhara yake hayakuishia kwake tu.

Kwa upande wa Marekani, ingawa awali walimuona Kennedy kuwa alionyesha ushujaa wa hali ya juu kutotoa amri ya kutumia nyuklia kwa haraka, wapo waliomchukia kuwa amekuwa laini kwa kutekeleza makubaliano na Urusi ya kuondoa majeshi na silaha zake za nyuklia nchini Uturuki, kuahidi kutoivamia tena Cuba na kutia saini makubaliano ya marais wa Marekani na Cuba kuzungumza mara kwa mara, ama ana kwa ana au kwa njia ya simu. Waliona Marekani imedhalilika.

Sitanii, unajua kilichofuatia? Ndiyo maana kichwa cha makala hii nikasema Castro kishiki cha mpingo. Novemba, mwaka 1963 wahafidhina wenye msimamo mkali, wakamuua Rais wa Marekani Kennedy kwa madai yanayotajwa kuwa eti ‘aliliaibisha taifa kubwa’ mwaka 1962 kwa kutoishindiria Urusi mabomu hayo ya nyuklia.

Baadhi walimuona Kennedy kutokana na jinsi alivyoshughulikia mzozo wa Cuba na Castro, kuwa alikuwa anakaribia kukiuka misingi ya Ubepari na kulipeleka taifa hilo katika falsafa ya Ujamaa.

Upande mwingine unatajwa kushiriki mauaji ya ya Kennedy inadaiwa alishutumiwa kuwatesa watu wa Cuba na ndiyo maana Novemba 22, 1963 saa 06:30 mtu aliyefahamika kwa jina la Lee Harvey Oswald, alimpinga risasi katika eneo la Dallas, Texas, Marekani. Kifo cha Kennedy kilitangazwa nusu saa baadaye, kwa maana ya saa 07:00 mchana.

Kwa hofu ilivyokuwa imetawala taifa hilo, aliyekuwa Makamu wa Rais Lyndon Johnson, ilipofika saa 08:39 mchana, aliapishwa kuwa Rais wa 36 wa Marekani. Johnson aliapishwa ndani ya Ndege ya Air Force One katika uwanja wa Dallas Love Field mbale ya mashuhuda 30, akiwamo Jacqueline Kennedy mke wa Kennedy ambaye hadi Johnson anaapishwa nguo zake zilikuwa bado zimetapakaa damu. Kennedy na mke wake, walikuwa kwenye gari la wazi wakiwapungia wananchi mikono, ndipo mumewe aliyekuwa pembeni mwake alipigwa risasi.

Kilichowatisha zaidi Wamarekani, Oswald alipochunguzwa alibainika kuwa Aprili 10, 1962 alinunua pistol aina ya .38 revolver, na badaye akaanzisha Kamati ya Kumtetea Castro, iliyofahamika kama Fair Play for Cuba Committee. Miaka miwili kabla alikuwa akiishi nchini Urusi. Oswald wakati amekamatwa na polisi, alijitokeza mtu mwingine aliyekuwa na pistol kama yake .38 revolver naye akampiga risasi Oswald na kumuua katika mikono ya polisi kwa maelezo kuwa alikuwa amemuua Rais Kennedy. Mtu huyo, Jack Ruby, ambaye awali alifahamika kama Jacob Rubenstein, alifunguliwa mashitaka na kutiwa hatiani kwa mauaji ya kukusudia.

Sitanii, mwangwi wa Castro haukuishia kwa mauaji ya Rais Kennedy pekee. Oktoba 14, 1964, aliyekuwa Rais wa Urusi, Khrushchev naye alipinduliwa nchini mwake kwa chama chake cha Kikomunisti kudai aliliaibisha taifa hilo kubwa kwa kurudisha meli nyuma badala ya kuendelea na mapambano na Kennedy hadi kikaeleweka. Nafasi yake ilichukuliwa na Leonid Brezhnev, aliyetangazwa kuwa mkuu wa nchi na kutakiwa kuendeleza mapambano.

Cuba kwa upande wake, iliendelea na kilimo cha miwa, ikajenga hospitali nyingi, shule za kutosha, ikasomesha watu wake udaktari na hadi leo Tanzania imepata msaada mkubwa wa madaktari kutoka Cuba. Mwalimu Julius Nyerere akawa rafiki mkubwa wa Castro.

Castro, ameendelea kuwa madarakani huku akipambana na marais 11 wa Marekani kuanzia Rais wa 34 hadi wa 45 Barack Obama waliopambana angushwe, lakini wakamshindwa. Obama kwa upande wake ametia saini mkataba wa kuondosha uhasama kati ya Marekani na Cuba, lakini Trump ameahidi kuwa ataufutilia mbali mkataba huo akiingia madarakani.

Mwaka 2006 Castro aliachia madaraka kwa mdogo wake, Raul ambaye ameendelea kuongoza nchi kwa miaka 10 chini ya ushauri wa Karibu wa Fidel. Hata hivyo, naye Raul amekwishatangaza bayana kuwa mwaka 2018 anastaafu urais wa Cuba. Fidel Castro alizaliwa Agosti 13, mwaka1926, katika mji wa Birán, Cuba na amefariki dunia Novemba 26, mwaka 2016 baada ya kukwepa mishale ya kutosha. Je, dunia bado inao wanapinduzi wa kutetea falsafa wanazoziamini hadi kufa kwao? Castro ataendelea kuwa kisiki cha mpingo milele.

 

Je, unaifahamu fika historia ya Castro, usikose nakala ya JAMHURI wiki ijayo.

By Jamhuri