‘Jihadhari na ufumbuzi unaozalisha tatizo jipya’

 

Napenda Rais John Magufuli afanikiwe kisiasa na kiutawala, napenda aandike historia kama alivyoahidi aliposema na wahariri kwenye mkutano wake wa Novemba 4, 2016 pale Ikulu. 

Hata hivyo, kupenda peke yake na kumtakia mema hakumwezeshi mtu kufanikiwa ikiwa hataifuata njia sahihi ya kumfikisha kwenye mafanikio. Makala hii itakuwa ya mwisho kumshauri Rais wetu kuhusiana na hatari zinazoikabili Tanzania huko mbele tuendako.

Inampasa Rais Magufuli kila hatua anayopiga kwenda mbele, ageuke nyuma, atazame kule tulikotoka, kwani kutazama nyuma kutamsaidia kutambua amechukua mwelekeo gani. 

Nabii Musa alipowatoa nduguze utumwani Misri, walitangatanga jangwani kwa miaka mingi, wakiwa wamechoshwa na maisha ya jangwani, Waisraeli walitamani kuingia kwenye nchi mpya waliyoahidiwa. Musa akawasisitizia kwamba siku zote wakumbuke walikotoka kwa kutazama nyuma pia wakumbushane.

Kutokana na huo msisistizo aliuotoa, kitabu chake cha mwisho kati ya vitano alivyoandika kiliitwa ‘Kutazama Nyuma’; wengine walipokitafsiri walikiita ‘Reflection’ kumaanisha mtu anayejiangalia mwenyewe kwenye kioo. Katika Kiswahili kimeitwa ‘Kumbukumbu la Torati.’

Ujumbe mkuu ni huo kwamba Musa anawataka Waisraeli wakiwa jamii huru waishi wakijitazama kama mtu anavyojitazama kwenye kioo, wasiache kutazama nyuma walikotoka, wajikumbushe pia wakumbushane mabaya yaliyopita ili yasijirudie. Musa alitaka kumbukumbu ya mabaya iwasaidie Waisraeli kubaki kwenye lengo la awali ili mazuri au mafanikio yao wanayoyapata yasiwaongoze kwenye upotofu.

Mafanikio yanapotosha mfano hai ni Ulaya na Marekani ambako watu baada ya kuendelea na kujiongezea nguvu wamelewa utajiri, wamesahau kuwa dunia tunayoishi ni ya Mungu, wamefikia kushinikiza viongozi wa nchi maskini waukubali ushoga. Hawaogopi wanataka kuwalazimisha maskini kwa huo umaskini wao wampuuze Mungu aliyekataza machukizo hayo.

Nchini Marekani, kanisa limekuwa butu, limekosa makali, tukiurejea mfano wa Yesu, kanisa la Ulaya na Marekani ndiyo chumvi iliyoharibika isiyofaa kuendelea kutunzwa wala kutumika, inastahili kutupwa jalalani ikanyagwe na watu.

Kanisa lililopoteza madaraka yake kwa Serikali hadi linashindwa kusimamia mambo ya msingi aliyoagiza Mungu, halina faida yoyote kwa mwanadamu lichukuliwe sawa na takataka nyingine zilizoko duniani.

Huku Afrika, makanisa yaliyoletwa na wakoloni yasiwadanganye Waafrika kwamba yatawafanya waendelee kumtumikia Mungu, kwani kutokana na mfumo wao kiutawala na utegemezi wa viongozi wake kwa nchi za Ulaya na Marekani, hatimaye wataukubali ushoga na kufungisha ndoa za jinsia moja kanisani au serikalini. Nchi jirani za Malawi na Msumbiji zimeridhia na kutambua ndoa za jinsia moja.

Musa aliwasisitizia Waisraeli kutosahau uhuru wa taifa lao na kuikumbuka daima siku ile walipopata uhuru, kumbukumbu ya uhuru ilidumishwa kupitia Sikukuu ya Pasaka. Mungu aliagiza kila Muisraeli kumchinja mwanakondoo na kumla kwa haraka haraka wakiwa wamesimama na hiyo nyama iwe ya kubanika ama ya kuchemshwa, haikutakiwa iungwe vionjo vya ziada kama chumvi na vinginevyo, bali ilitakiwa nyama peke yake.

Kila familia ilitakiwa kula kwa pamoja, tukio hilo lingewafanya watoto kudadisi wakiuliza “kwa nini leo tule kwa haraka kama tunafukuzwa?  Kwa nini tule kama kwamba hatuko nyumbani bali tuko safarini? Kwa nini tule kama tunakimbizana na jambo fulani?”

Ndipo baba angepata wasaa wa kuwajulisha wadogo wasiojua kwa kusema “Zamani sisi Waisraeli tulikuwa watumwa nchini Misri, siku kama ya leo ndipo Mungu wetu alipohitimisha kazi ya ukombozi wetu. Mungu alitoa pigo la mwisho kwa Wamisri hadi mtawala wao Farao akawaachilia baba zetu watoke utumwani. Mungu aliwaagiza baba zetu wamchinje kondoo na damu yake waipakaze kwenye miimo ya milango ya nyumba zao ili malaika wa mauti aliyetumwa kuua atakapoiona damu, aivuke nyumba ya Muisraeli asiingie ndani kuua.”

Mungu aliwaagiza Waisraeli kumla mwanakondoo huyo kwa haraka haraka na kummaliza kabla malaika wa mauti hajafika, mabaki yake iwe nyama ama mifupa hayakutakiwa kulala nyumbani bali kuteketezwa motoni.

Kupitia Sikukuu ya Pasaka, dhana ya uhuru kwa Muisraeli ilidumishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, hapa Tanzania mwelekeo ni kwamba kuna kizazi ambacho hakitakuja kuona thamani ya uhuru, kitaibuka kizazi kisichokuwa na kumbukumbu kwamba tuliwahi kutawaliwa na zikafanyika jitihada za kujitawala wenyewe. 

Kwa sababu elimu itolewayo kwa watoto wetu mashuleni siyo elimu ya ukombozi, ni elimu inayowaandaa kuajiriwa na kutumikishwa. Watanzania wa kizazi kipya wanawahusudu Wazungu kupita kiasi, itikadi ya utandawazi imechangia kuwaharibu, sera za mfumo wa soko huria zimeurudisha ‘ukoloni’ kwa mlango wa nyuma. Lililo baya zaidi kizazi kipya ambacho hakikuonja ukoloni kimekuwa na uchu wa kutawaliwa kuzidi wale waliozaliwa na kukulia kwenye ukoloni.

Nikifikia nukta hii ndipo nashawishika kumtahadharisha Magufuli kwamba asije akajikuta anawaongoza Watanzania kwenye safari ya kuwarudisha Misri walikotoka kwenye nyumba ya utumwa. Sisi Misri yetu ni ukoloni ambao kizazi cha akina Kwame Nkrumah (Ghana), Julius Nyerere (Tanzania), Ahmed Sekou Toure (Guinea), Nelson Mandela (Afrika Kusini), Kamuzu Banda (Malawi), Jomo Kenyatta (Kenya), Haile Selassie (Ethiopia), Kenneth Kaunda (Zambia), Gamal Abdel Nasser (Misri), Joshua Nkomo/Robert Mugabe (Zimbabwe), Seretse Khama (Botswana) na Patrice Lumumba (DRC) waliukataa wakajitoa mhanga kwamba ingawaje hawana silaha za kuwapinga Wazungu, lakini ili kuonesha hawaukubali ukoloni wakaupinga kwa midomo na mioyo yao.

Je, ukoloni ni nini? Kwa tafsiri isiyo rasmi yaani isiyokuwa ya kikamusi, ukoloni ni mazingira ya watu kutoka dola yenye nguvu kijeshi, kiuchumi na kiteknolojia kuivamia nchi ya watu wanyonge wasio na nguvu za kijeshi, kiuchumi na kiteknolojia na kuwakalia kinguvu bila ridhaa yao, ili kujinufaisha kwa utajiri asilia wa hiyo nchi inayovamiwa.

Chini ya utandawazi na mfumo wa soko huria, uvamizi dhidi ya nchi nyonge unaendelezwa kwa mtindo tofauti, raia kutoka mataifa yenye nguvu kiuchumi wanakuja na nguvu ya mitaji, wanaikalia nchi yenye watu maskini wasio na mitaji wala teknolojia ya juu, uvamizi wao unawanufaisha kwa kuvuna kirahisi hizo rasilimali za nchi ya maskini.

 

Uvamizi wa karne ya 18 ulihusisha majeshi lakini uvamizi wa kileo unahusisha fedha, wavamizi wa leo wanaitwa na kubembelezwa kwa sababu wamepewa jina jipya zuri wanaitwa ‘wawekezaji.’ Hakuna mwananchi atakayethubutu kuwapinga wawekezaji wanaotoka nje ambao nchi inawahitaji na imewatafuta waje kuwekeza.

Lakini athari za uwekezaji ndizo zitakazothibitisha ukweli kwamba uvamizi wa karne ya 18 unafanana na uvamizi wa kileo, Mtanzania ataendelea kuwa maskini zaidi hata kama wawekezaji wataongezeka Tanzania ikawa na miradi mingi mikubwa itakayowaajiri kwa wingi ama viwanda vingi vitakavyowaongezea ajira nyingi.

Hayo yatakapotokea tutakuwa tumeyarudia mazingira ya awali yaliyowafanya wageni kututawala baada ya kuzimiliki njia kuu za uchumi wetu. Mwingereza alipotawala kuanzia mwaka 1920 hadi 1960, Tanganyika ilikuwa na uchumi mzuri uliotokana na uzalishaji wa juu wa zao la katani. Lakini wafanyakazi wake (manamba) wengi waliendelea kuwa maskini, kwa nini? Kwa sababu ajira peke yake siyo suluhisho la kumwondolea mwananchi umaskini.

Endapo mwenye mtaji atamwajiri Mtanzania lakini akamlipa mshahara kiduchu hali hiyo itamwondoleaje umaskini? Uhalisia wake ni kwamba Mtanzania atakuwa ameondokana na tatizo la kukosa ajira huku akiendelea na tatizo la umaskini, wafanyakazi watakaoangukia hali hiyo, hata wakichapa kazi mara mbili zaidi bado hawatajikwamua na umaskini wao.

Hayo ndiyo mazingira yaliyomfanya Rais wa Kwanza, Mwalimu Nyerere, kuona uhuru walioupata Watanganyika mwaka 1961 hauna maana ikiwa uchumi wao utaendelea kumilikiwa na wageni na kutowanufaisha wenye nchi, ndipo mwaka 1967 alipoibuka na sera za ‘utaifishaji.’

Mwekezaji anayevutwa aje nchini mwetu awekeze kwenye kilimo ama awekeze kwenye ujenzi wa viwanda lazima atamilikishwa ardhi, baada ya miaka kadhaa Watanzania watakaokuwapo watajikuta wakikabiliwa na tatizo la wageni kumiliki ardhi huku wao wakifanya kazi kuwatumikia mashambani na viwandani.

Mgogoro wa ardhi nchini Zimbabwe utufundishe kwamba tunahitaji uwekezaji unaodhibitiwa na dola, mfumo wa soko huria usituzalishie uwekezaji huria. Hilo litakuwa tatizo litakalowalazimisha warithi wetu wamwage damu ili kujikomboa, itakuwa tumewafanyia dhambi isiyosameheka. Kwa sasa mwekezaji anayevutiwa ama anayeombwa awekeze nchini ni rahisi kwake kuiwekea Tanzania masharti ili iyatimize ndipo awekeze kuliko Tanzania kumwekea masharti ili ayatimize ndipo awekeze.

Lipo suala la mavuno ya mwekezaji na pia haki ya kuhamisha faida anayotengeneza na kuipeleka kwenye nchini yake, hapa ndipo unapotakiwa mfumo wa uhakika wa ndani ya nchi. Nyerere alikusudia dola imiliki njia kuu za uchumi, tuukumbuke mfumo ule na tuuangalie upya kuona jinsi tunavyoweza kuuendeleza katika mazingira mapya ya kileo. 

Vinginevyo tutajikuta tumeigeuza Tanzania yetu iwe eneo zuri linalowezesha uzalishaji usiomnufaisha Mtanzania. Tunaweza kuwa na mashamba makubwa ya wawekezaji yatakayofanana na mashamba ya mkonge na pamba na chai yaliyomilikiwa na ‘mabritishi’ na ‘magiriki’ – enzi hizo mkulima kuitwa ‘britishi’ au ‘giriki’ ilikuwa fahari.

Tunaweza kuongoza duniani kuzalishaji gesi kama Tanganyika ilivyokuwa ya kwanza kuzalisha mkonge mwingi ilipotoa asilimia 28 ya mahitaji ya dunia, lakini ‘manamba’ wakiwa maskini sana.

Mkoani Tanga, umeme ulisambazwa hadi barabarani haukuzimika uliwaka usiku wote, lakini kando kando ya barabara kwenye vijumba walivyoishi ‘manamba’ watu walitumia vibatari, hayo ndiyo matokeo ya maendeleo ya kuletewa yasiyopatikana kwa kujiletea wenyewe. Tunaweza kuongoza kwa uzalishaji wa mafuta duniani lakini hali za Watanzania zikifanana na za Waogoni wa Nigeria ambao Ken Saro Wiwa aliwapigania hadi akahukumiwa kunyongwa, hapo wananchi walipomwelewa na kuziambia kampuni za wawekezaji “kiama chenu kimewadia.”

Upo mfano hai wa uwekezaji uliofanywa kwenye madini na migodi yetu ya dhahabu huko Bulyanhulu, Nyamongo, Buzwagi na kwingineko, kwanini kuna kilio badala ya neema? Tatizo siyo wawekezaji au uwekezaji wao, wala siyo wingi wa rasilimali zilizoko bali tatizo ni mfumo. Tanzania ikivutia wawekezaji bila kuwa nchi yenye mfumo wake unaoeleweka ‘uwekezaji huria’ utageuka janga badala ya neema.

Uko mfano hai mwingine wa zao la korosho. Watanzania wengi hasa wakazi wa kusini mikoa ya Lindi na Mtwara wanapenda kula korosho, lakini hawali korosho ingawaje zipo, tatizo likiwa bei. Hapa ndipo kinapoibuka kitendawili kinachochefua; iweje Tanzania izalishe korosho lakini Mtanzania mwenye hamu ya korosho akashindwa kula korosho zinazozalishwa nchini mwake?

Tafadhali Mheshimiwa Magufuli, endelea kukaribisha wajenzi wa viwanda lakini ukumbuke dola haipaswi kupoteza umiliki.

1761 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!