Na Moshy Kiyungi

Tabora

Mwanamuziki mashuhuri wa kimataifa wa Afrika Kusini, Hugh Masekela, amefariki dunia Januari 24, 2018 jijini Johannesburg, Afrika Kusini akiwa na umri wa miaka 78. Chanzo cha kifo chake ni ugonjwa wa tezi dume alioupata miaka kadhaa iliyopita.

Bendi yake ilitoa taarifa ikisema, Masekela amekuwa akiuguza ugonjwa huo tangu mwaka 2008. Machi 2016, Masekela alifanyiwa upasuaji wa jicho baada ya saratani kusambaa, ikabidi afanyiwe upasuaji mwingine Septemba mwaka huo.

Masekela alisifika kwa nyimbo zake na mchango wake katika harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Wasifu wa Masekela unaonesha kuwa alizaliwa Aprili 4, 1939 katika mji wa KwaGuga huko Witbank, Afrika Kusini.

Alikuwa mpulizaji mashuhuri wa tarumbeta wa muziki ya jazz. Alianza kuimba na kupiga piano tangu akiwa mtoto, baada ya kuona filamu ya Young Man with a Horn.

Masekela alifahamika ulimwenguni kwa aina ya kupiga muziki wa jazz la mtindo wa Afri-Jazz na hasa upulizaji wake wa tarumbeta, uongozi wa bendi ya muziki, utunzi na mwandishi mahiri wa mashairi ya muziki.

Masekela alijifunza kupuliza tarumbeta akiwa shuleni, mwalimu wake akiwa ni Padri Trevor Huddleston, ambaye alikuwa ni Mkuu wa Shule ya Huddleston.

Hakuchukua muda, Masekela aliweza kuitawala ala hiyo ya tarumbeta na mwaka 1956 akajiunga na kundi la Jazz la Herbert’s African Jazz Revue.

Akiwa na umri wa miaka 20, Masekela alikuwa akitumbuiza muziki wa aina tofauti hasa ya jazz, bebop, funk na Afrobeat wakati huo akiwa na kundi la Jazz Epistles. Kundi hilo lilikuwa na wasanii maarufu kama mpiga kinanda mahiri, Abdillah Ibrahim.

Mwaka 1960, Masekela alikwenda London, Uingereza ambako alijiunga na shule ya muziki ya Guildhall na baadaye alikwenda New York, Marekani ambako alisoma katika mji wa Manhattan.

Mwaka 1962 alitoa albamu yake ya kwanza iitwayo Trumpet Africa. Miaka miwili baadaye alitoa nyingine iitwayo The Americanization of Ooga Booga ambayo ilitamba mpaka kushika chati, hasa baada ya kupigwa na kituo kimoja cha radio cha mjini California.

Mpaka kufikia Agosti 2000, Masekela alikuwa ameuza nakala milioni 50 na kumfanya apate tuzo ya Platinum.

Hugh ameshirikiana na wasanii kama Miriam Makeba wa Afrika Kusini na Paul Simon wa Marekani kwenye albamu ya Graceland.

Tarumbeta yake imesikika zaidi kwenye nyimbo za Gumboots na Diamonds on the soles of her shoes.

Enzi za uhai wake, Masekela aliwahi kusema kwamba alitumia muziki kama silaha ya kusambaza mageuzi ya kisiasa enzi hizo za ubaguzi wa rangi, na alifanikiwa.

Imeelezwa kwamba Masekela alikuwa ni baba wa muziki wa jazz nchini Afrika Kusini kwa mchango wake mkubwa uliobakia ndani ya mioyo na kumbukumbu za mamilioni ya watu.

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, amemsifia Masekela kama msanii wa muziki wa  jazz, mpiga tarumbeta maarufu, mwanaharakati wa utamaduni na mtu aliyekuwa katika harakati za ukombozi.

Aliuweka hai mwanga wa uhuru duniani kote katika harakati zake za kupinga ubaguzi wa rangi kupitia muziki wake, na kushinikiza uungwaji mkono wa kimataifa, fani ya muziki na nchi kwa ujumla tumempoteza mtu muhimu sana,” amesema Rais Zuma.

Mwimbaji wa Afrika Kusini, Johnny Clegg, amemuelezea Masekela kama mwanamuziki bora na siku zote akiishi kwa mitazamo ya asili yake ya Afrika Kusini.

Aliondoka nchini Afrika Kusini wakati ilipoongozwa na watu weupe mwaka wa 1960, hakurejea hadi pale Nelson Mandela alipoachiwa huru mwaka wa 1990.

Muda wote alikuwa uhamishoni jijini London, Uingereza.  Baadaye alihamia jijini New York, Marekani na kukutana na msanii mwenzake wa Afrika Kusini, Miriam Makeba, Dizzy Gillespie na Harry Belafonte. Masekela na Makeba waliishi maisha ya ndoa ya muda mfupi.

Miongoni mwa nyimbo zake zilizovuma na zilizopendwa ni ule wa Bring Him Back Home, aliposhinikiza Nelson Mandela aachiwe huru.

Masekela alitumbuiza katika hafla ya ufunguzi wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010, zilizofanyika nchini Afrika Kusini ikiwa ni mara ya kwanza fainali hizo kufanyika barani Afrika.

Kwa upande wake, Waziri wa Sanaa wa Afrika Kusini, Nathi Mthethwa, amesema taifa hilo limempoteza mwanamuziki wa haiba ya kipekee aliyeburudisha nyoyo za watu wa taifa hilo kupitia muziki yake.

Wakati wa enzi za nguli huyo, alikuwa mwanaharakati akipigania haki na kupambana dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.

Moja ya kazi zake ni Soweto Blues, muziki ambao ulitumiwa na makundi ya kupambana na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini. Nyingine ni pamoja na Tagi, Mandela, Apartheid, Afrika Kusini, Hugh Masekela.

Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.

Mwandishi  wa makala hii anapatikana kwa namba 0784 3312000767 331200 na 0713 331200.

By Jamhuri