Home Kurasa za Ndani BARABARA YA VUMBI MGODI WA NGAKA INAVYOATHIRI UCHUMI NA MAZINGIRA

BARABARA YA VUMBI MGODI WA NGAKA INAVYOATHIRI UCHUMI NA MAZINGIRA

by Jamhuri

Na Albano Midelo

WAKAZI wa vijiji vya Kata ya Ruanda vilivyopo barabarani kutoka mgodi wa makaa ya mawe Ngaka Wilaya Mbinga Mkoa wa Ruvuma wanapata athari za kimazingira zinazosababishwa na uchimbaji wa madini hayo.

Kwa mujibu wa sensa ya makazi ya mwaka 2012 Vijiji vinavyounda Kata ya Ruanda vina jumla ya wakazi 7374 ambao wanatoka katika vijiji vya Ukombozi, Ntunduwaro, Paradiso na Ruanda.

Diwani wa Kata ya Ruanda Edimund Nditi anasema Wakazi wa vijiji hivyo  wanapata athari ya vumbi kutoka kwenye magari yanayobeba makaa wa mawe hadi bandari ya nchi kavu ya Kitai hasa katika kipindi cha kiangazi.

Hata hivyo Kampuni binafsi ya TANCOAL ambayo inajishughulisha na uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe kwenye mgodi wa Ngaka,imekuwa inamwagia maji kwa kutumia magari ya kubeba maji(boza) katika baadhi  ya maeneo ya makazi ili kupunguza vumbi zito ambalo linawaathiri wananchi.

Kuhusu barabara ya vumbi toka mgodini hadi bandari ya nchi kavu ya Kitai inavyoathiri wananchi wanaoishi kandokando mwa barabara,Kaimu Meneja wa Mgodi wa Ngaka anasema barabara hiyo ipo chini ya Wakala wa Barabara mkoa wa Ruvuma(TANROADS) na kwamba Kampuni ya TANCOAL wanatumia barabara hiyo kusafirisha makaa ya mawe hadi Kitai tangu mwaka 2011.

Magari makubwa zaidi ya 70 kila siku yanabeba makaa ya mawe,wakati wa kiangazi magari yanatimua vumbi jingi ambalo linakwenda kwa wananchi,hatua ambazo tunazichukua ni kumwagilia maji katika barabara hiyo kwenye makazi ya watu ili kupunguza vumbi ambalo linaathiri wananchi’’,anasema Mwanga.

Hata hivyo anasema barabara hiyo inatakiwa ipitike muda wote na kwamba kila barabara inapoharibika mgodi unakuwa wa kwanza kutoa vifaa vya ujenzi na kufanya matengenezo,hata hivyo TANROADS imeanza kufanya matengenezo barabara hiyo toka Kitai hadi mgodi wa Ngaka ambapo hivi sasa Mkandarasi yupo katika kijiji cha Paradiso.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Dk.Patrick Banzi anasema barabara hiyo wakati wa masika inachafuka na kusababisha gari kupungua kwa kuwa barabara ya kutoka mgodini hadi Kitai ni ya tope hali ambayo inaathiri mapato ya Halmashauri.

Hata hivyo Dk.Banzi anasisitiza kuwa barabara hiyo muhimu katika uchumi wa wilaya ya Mbinga, ikijengwa lami uzalishaji wa makaa ya mawe utaongeza,magari yatakuwa mengi na Halmashauri ya wilaya ya Mbinga itapata mapato mengi.

Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Ruvuma (TANROAD)Mhandisi Lazack Alinanuswe anasema kuwa kuna mpango wa kuweka lami katika barabara hiyo ambayo inaanzia Kitai kupitia Ruanda hadi Lituhi ili kumaliza tatizo la ubovu wa barabara hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Ruvuma.

Mhandisi Alinanuswe anasema upembuzi yakinifu,usanifu wa kina na matayarisho ya nyaraka za zabuni za ujenzi wa barabara ya lami toka Kitai hadi Lituhi yenye urefu wa kilometa 84.5 umefanyika na kwamba mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 667 unatekelezwa na Mhandisi Mshauri Crown Tech Consult Ltd.

Kazi ambazo anazifanya Mhandisi Mshauri huyo ni upembuzi yakinifu na usanifu wa kina,kazi hii ipo katika hatua za mwisho na hadi kufikia Septemba 30,2017 zaidi ya shilingi milioni 590 sawa na asilimia 88.50 zilitumika kumlipa Mhandisi Mshauri’’,anasema Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma.

Kuhusu milipuko inayotokea wakati wa uchimbaji wa madini hayo,kaimu Meneja wa Mgodi wa Ngaka Edward Mwanga anasema  madini ya makaa ya mawe  katika eneo la Ngaka yanapatikana umbali wa kuanzia mita 20 toka juu ya ardhi na kwamba kabla ya kuyafikia kuna  miamba mikubwa ya mawe ambayo haiwezi kuondolewa bila kulipua baruti.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ntunduwaro Joseph Ngahy anasema kijiji hicho licha ya kuwa na neema ya madini ya makaa wa mawe,hakina huduma muhimu za kijamii.

Anazitaja huduma ambazo hazipatikani kwa uhakika ni barabara ya lami, maji safi na salama,umeme na huduma ya afya ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa hali inayosababisha wakazi wa Kijiji hicho kwenda Songea na Mbinga kufuata matibabu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ntunduwaro John Nyimbo anasema ulipuaji wa baruti migodini umesababisha majengo ya shule ya msingi Ntunduwaro kuweka nyufa na kupasuka na kwamba baadhi ya nyumba zimeanguka na nyingine zina nyufa kubwa kuanzia  juu hadi chini jambo ambalo ni hatari kwa wanafunzi na wananchi wengine.

Magari yaliobeba makaa ya mawe yanapita katika Kijiji cha Ntunduwaro na kuathiri wananchi waliopo kando kando mwa Barabara na kwamba vumbi hilo pia linasambaa na kuleta kero kubwa wakati wa kiangazi’’,anasema Nyimbo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Paradiso Steven Challe anasema wananchi wake wamekuwa wanapata kero kubwa wakati wa kiangazi kutokana na vumbi ambalo magari yanayosafirisha makaa ya mawe yamekuwa yanatimua na kuingia katika nyumba za watu waliojenga kando kando mwa barabara hiyo.

Wakati wa kiangazi kero inakuwa kubwa kwa kuwa wenye magari wakishapakia makaa ya mawe wakati mwingine huwa hawafuniki vizuri hivyo vumbi la makaa linakwenda kwenye nyumba za watu,pia makaa yakimwagika,huwa hawazoi inapofika kipindi cha mvua kama sasa makaa yanashuka moja kwa moja kwenye vyanzo vya maji ambavyo vinatumiwa na wananchi’’,anasema Challe.

Anatoa rai kwa serikali kuwajengea haraka barabara ya lami ili kumaliza kero hiyo ambayo inasababisha wananchi kuugua magonjwa ya njia ya hewa kawa mafua na kikohozi.

Anasema maji ambayo yanamwagwa na Kampuni ya TANCOAL ili kupunguza vumbi katika barabara hiyo bado yanasaidia kwa kiwango kidogo kwa sababu wananchi wanaendelea kuathirika kutokana na magari mazito yanayopita wakati wote hivyo anashauri ujenzi wa barabara ya lami ndiyo suluhisho la kudumu.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ruanda Deo Haule anasema barabara ya vumbi toka mgodini ambayo inapita katika kijiji chake inaleta changamoto kubwa wa wananchi licha ya Kampuni hiyo kujitahidi kumwagiliaji maji,bado hali ni mbaya hasa majira ya kiangazi.

Dk.Winfrid Mgaya wa Kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza katika Hospitali ya Rufaa Peramiho, anasema hewa chafu ya ukaa yenye gesi ya madini ya makaa ya mawe inaposambaa hewani si tu inawaathiri watu wa eneo la kuzunguka mgodi bali pia inasambaa na kuenea sehemu mbalimbali angani na kuchangia ongezeko la joto duniani.

Dk.Mgaya anasisitiza kuwepo kwa athari za makaa ya mawe kimazingira kuanzia uchimbaji, upasuaji, usagaji, usafirishaji, uhifadhi na kutupa mabaki ya makaa ya madini hayo kama  uchafu kwenye vyanzo vya maji.

Uchunguzi umebaini kuwa madhara ya madini ya makaa ya mawe yanaweza kuwaathiri viumbehai kwa njia ya hewa,maji na nchi kavu,ambapo katika mkoa wa Ruvuma wilaya ambazo zinaguswa moja kwa moja ni wilaya ya Mbinga,Nyasa na Songea.

Katika barabara ya kutoka bandari ya nchi kavu ya Kitai kupitia Songea pembeni mwa barabara mawe ya madini ya makaa ya mawe yameanguka lakini pia vumbi hilo linaweza kusambaa hewani kwa kuwa magari yanayobeba yamefunikwa na turubai hivyo vumbi ambalo haliwezi kuonekana kwa macho linaweza kusambaa na kuleta athari.

 Mwandishi ni mchangiaji wa gazeti hili mawasiliano yake ni albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917

 

 

You may also like