NA ANGALIENI MPENDU

Binadamu anapokuwa na tabia ya kuaminika, anapenda haki na anafuata utaratibu mzuri wa kufanya kazi, anajijengea sifa ya uaminifu, uadilifu na nidhamu. Huyu ndiye binadamu ninayemfahamu na ninayemkubali kwa Tanzania niitakayo.

Binadamu mwenye upungufu wa sifa hizi, hutambuliwa na kuonekana hayawani na mpenda kufanya mambo ya dhuluma na ufisadi, hiana na choyo, uwongo na utovu wa nidhamu. Huyu ndiye anayefisidi uchumi na rasilimali za Taifa. Simkubali kamwe.

Hapa Tanzania tunao watu wenye sifa ya ubinadamu (utu) na tunao pia wenye sifa ya uhayawani (unyama). Haya ni makundi tofauti kidesturi, kimtazamo na kimsimamo katika kufanya kazi. Kundi la utu linajenga Taifa; na kundi la unyama linabomoa Taifa.

Tangu nchi yangu ipate uhuru miaka mingi iliyopita, imebebwa katika mikono ya makundi haya na kulelewa kwa theluthi mbili ya amani na utulivu, na kwa theluthi moja ya rushwa, ufisadi na umaskini. Na hapa ndipo ninapodiriki kutamka Tanzania ninayoitaka na Tanzania nisiyoitaka. Leo nazungumzia ninayoitaka.

Kuna mambo mengi muhimu ingawa yanaonekana ni madogo kwa thamani ya nchi. Lakini ndiyo yenye kubeba vitu vitatu, mahitaji ya Watanzania katika kujenga na kudumisha Taifa letu. Vitu hivyo ni Uhuru, Haki na Demokrasia.

Watanzania tukiamua kwa nia moja ni wazi tutafika Tanzania ninayoitaka kwa mambo haya yanayoonekana ni madogo. Tunapopendana, tunapojali haki zetu na tunapoweka matumaini yetu katika kauli na matendo yetu, tutafika kwenye mafanikio.

Mafanikio yanapopatikana yanakuwa ni chachu katika akili zetu na kutoa hisia anuwai kama vile: kazi za sanaa, uchoraji wa ramani za majengo, utundu wa kubuni kutengeneza vifaa na mitambo, na njia za mawasiliano na za usafirishaji mazao na watu.

Sekta ya elimu hupata wasomi na wataalamu, tiba hujaliwa kupokea mabingwa wa uganga, kilimo huzoa wakulima stadi na maji huwa safi na salama kutokana na wahandisi wanaokamilisha msemo “maji ni uhai.” Bila ya maji ni shida kwa Taifa.

Mambo yote haya na mengineyo yanahitaji uelewano na ushirikiano kuanzia katika familia hadi taifani. Kati ya baba na mama, watoto wa wazazi, walimu na wanafunzi, wakulima na wafanyakazi, wanasiasa na jamii, serikali na raia (wananchi).

Zaidi ya upendo, ubunifu na matumaini tunapata ushindi ambao daima huondoa unyonge na kupoteza hasira. Watu huwa furahani na kusahau machungu yaliyowapata au kuwafika. Yote niliyoyagusa yanakamilishwa na imani ya kumcha Mwenyezi Mungu.

Watanzania tuna dhima kubwa ya kumcha Mwenyezi Mungu. Viongozi wa dini muwe wamoja katika kuweka imani ya roho na nidhamu ya waumini kwa Mwenyezi Mungu, ili wapate shufaa wanapoomba toba baada ya kukiri makosa yao ya kila siku.

Mambo yote haya msingi wake ni vitu vitatu: uhuru, haki na demokrasia. Uhuru wa kuishi, kutoa mawazo, kutoa na kupokea habari, kustawisha jamii, kufanya kazi kwa upendo na amani, uhuru bila shuruti na kuondoa unyonge na umaskini.

Kila Mtanzania kupata haki ya jasho lake, kuishi katika nchi yake, kushirikiana na wenzake kugawana mali ya Taifa. Kufuata demokrasia ya nchi yetu inayolinda Katiba na sheria tunazojiwekea kwa mujibu wa makubaliano yetu. Hii ndiyo Tanzania ninayoitaka.

Itaendelea

By Jamhuri