Butiama inahitaji Zimamoto

Mwaka 2008 Serikali ya Awamu ya Nne ya Mzee Jakaya Kikwete, ilipitisha uamuzi wa kuanzishwa kwa wilaya mpya ya Butiama. Baadhi, na siyo wengi, hatukuunga mkono uamuzi huo. Waliyo wengi walifurahia uamuzi huo.

Ambao hatukuunga mkono tulitaja uhaba wa ardhi kwenye eneo la Kijiji cha Butiama, tukiwa tumesikia kuwa mahitaji ya ardhi ya makao ya wilaya ni makubwa sana, na tukitambua kuwa Kijiji cha Butiama kina maeneo mengi ambayo ni milima na ambayo hayafai kutumika kwa shughuli za kilimo.

Katika moja ya makala nilizoandika wakati huo juu ya mada hii, nilipendekeza kuwa, ili kuepuka kuwapunguzia wana Butiama ardhi ambayo tayari ni kidogo, Serikali ingetumia maeneo ya milima kujenga makao mapya.

Hoja nyingine ilikuwa uwezekano wa wengi kubadilisha mila na desturi za wachache. Mila na desturi za kabila dogo la Wazanaki zimedhoofishwa na ukweli kuwa, kwanza, Wazanaki ni kabila dogo mno, na muingiliano na makabila mengine kwa uhusiano mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuoleana, kumesambaratisha mila na desturi hizo.

Hapa silengi juu ya kukumbatia ukabila kama nyenzo ya kujikingia manufaa kwa Wazanaki, ila nazungumzia umuhimu wa kutunza urithi wa utamaduni kama nyenzo muhimu ya kuendeleza utalii wa utamaduni, kazi ambayo nimekuwa naifanya kwa karibia miaka minane. 

Kwangu mimi, wilaya inaambatana na athari za miji na majiji, na athari hizo mara nyingi hufifisha mila na desturi za jamii za vijijini.

Lakini pamoja na athari tunazoziona, ongezeko la watumishi wa Serikali na wa Halmashauri kwenye wilaya huleta ongezeko la kipato kwa wakazi wa eneo husika, kupitia huduma mbalimbali ambazo watatoa kwa wageni, ikiwa ni pamoja na malazi, na chakula. Kwa ujumla wazalishaji watapata soko kubwa zaidi na wataweza kuongeza uzalishaji na kipato chao. Wenye nyumba na vyumba vya kupangisha nao wataona faida ya moja kwa moja ya eneo kuwa wilaya kwa ongezeko la mahitaji ya nyumba.

Tayari zinaonekana dalili kijijini Butiama kuwa kuna ongezeko la kiwango fulani la ujenzi wa nyumba kwa madhumuni ya kukidhi ongezeko hili la wafanyakazi. Potelea mbali kuwa bado wafanyakazi wengi wa wilaya wanaishi nje ya Butiama na wanasafiri kila siku kuja Butiama na kuondoka kulala Musoma, Kiabakari, na maeneo mengine ya jirani.

Lakini hatimaye, idadi hii kubwa itahamia Butiama na kuongeza ile hatua ya kubadilisha kijiji tulichokifahamu kuwa mji ambao utakuwa mgeni kwetu na ambao hatuna uhakika kama utatuletea neema au majanga

Kama ipo ishara kuwa yatatokea majanga, basi ishara nzuri ilikuwa moto uliolipuka hivi karibuni kwenye eneo lililo karibu na makazi ya Mwalimu Nyerere; tukio ambalo limeibua maswali kuhusu ukamilifu wa Wilaya ya Butiama kuitwa wilaya bila kigugumizi.

Tunatambua kuwa Serikali haina uwezo wakati wote kuanzisha wilaya ikiwa imekamilika kwa vigezo vyote, na ni hivyo kwa Wilaya ya Butiama. Kwa mfano, ni mwezi uliopita tu ndiyo huduma za Benki ya National Microfinance Bank (NMB) zimezinduliwa Butiama, lakini kama ambavyo tukio la moto limebainisha, bado ziko huduma muhimu ambazo hazijakamilika.

Moto ulianza ukiwa mdogo tu, na haukuwa tishio kabisa kwa mali wala maisha ya watu. Moto ulipochachamaa, ikawa patashika ambayo sijawahi kushuhudia. Ipo kawaida ya watu kuchoma moto maeneo ya mashamba kwa madhumuni ya kusafisha eneo kwa haraka na kwa gharama ndogo, ingawa tunafamu pia kuwa wapo wanaoanzisha moto kwa makusudi tu.

Moto huo ulisambaa haraka, ukavuka barabara na kuanza kuunguza sehemu ya msitu wa miti aliyopanda Mwalimu Nyerere na ukaendelea kushika kasi mpaka kukaribia eneo yalipo Makumbusho ya Mwalimu Nyerere. Wakazi wa eneo hilo waliungana kudhibiti moto kwa zana ambazo hazikuwa na uwezo wa kutosha wa kudhibiti moto. Kilichosaidia ni kuwa upepo haukuwa mkali.

Baadhi yetu tulichukua jukumu la kuomba msaada wa gari la Idara ya Zimamoto kutoka Musoma na gari hilo lilifika baada ya saa moja, ambao ndiyo mwendo wa kawaida kati ya Butiama na Musoma. Wataalamu hao wa kudhibiti moto, pamoja na vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa kutoka Kikosi cha Rwamkoma, pamoja na wanakijiji waliyokusanyika, walishiriki kudhibiti moto na kuweza kuzuia usivuke na kukaribia jengo la Makumbusho. Msaada mwingine ulitolewa na gari la maji la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutoka kikosi cha Makoko, Musoma.

Ule moto ungevuka njia na kuunguza Makumbusho, basi jengo lililo karibu na makumbusho ambalo tuna hakika lingeshika moto ni nyumba ya Mwalimu Nyerere aliyojengewa na JWTZ, na Serikali ya Tanzania, baada ya Vita ya Kagera. Saa hizi tungekuwa tunazungumzia majipu kadhaa ya kutumbuliwa.

Tunaposhukuru kuwa hayo hayakutokea na tunapobaini kuwa hakuna majipu Butiama, tunatafakari pia kwamba upo umuhimu wa kuanzishwa kwa huduma za zimamoto katika Wilaya ya Butiama, si kwa ajili ya kulinda tu urithi wa historia inayomhusu Mwalimu Nyerere, lakini pia kwa kuwaongezea wakazi wa Butiama ulinzi wa maeneo yao dhidi ya matukio ya moto ambayo sina shaka yataendelea kutokea.

Wakati mwingine tukio baya ni mwanzo wa uamuzi wenye manufaa. Tukio baya tumeliona. Sasa tunasubiri uamuzi wenye manufaa.