Balozi wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Michael Bloomberg, akigagua namna bwawa la Theewaterskloof linaloathirika kwa kukauka kunakochangiwa na mabadiliko ya tabianchi.
Baada ya mamlaka za Cape Town kudhibiti matumizi ya maji Februari mwaka huu, kufikia galoni 13 kwa siku kwa mtu mmoja, wakazi wa jiji hilo wanatumia muda mrefu kusimama kwenye foleni kusubiri maji. (Picha kwa hisani ya AP)

Cape Town iliyopo Afrika Kusini ni miongoni mwa majiji machache yenye vivutio vya utalii vinavyochangia pato la taifa hilo lenye nguvu kubwa ya uchumi barani Afrika, hivi sasa linakabiliwa na upungufu wa maji ulio kero kwa wenyeji na wageni.

Meya wa jiji hilo, Patricia De Lille amesema upungu wa maji uliopo umesababisha matumizi ya maji jijini humo kushuka kufikia lita milioni 500 kwa siku, ikilinganishwa na lita bilioni 1.1 za mwaka 2016.

Takwimu hizo zinazotolewa na Meya De Lille ni kielelezo cha namna mamlaka za Cape Town zilivyojipanga kukabiliana na changamoto zinazotokana na upungufu wa maji.

Wenyewe na wageni wanaoingia jijini Cape Town wamekuwa wakitahadharishwa kuhusu matumizi ya maji yasiyofaa, lengo ni kuwezesha kiasi kidogo cha maji yaliyopo kukidhi mahitaji ya kibinadamu.

Wajumbe wa Mkutano wa 17 wa Dunia wa Kudhibiti Tumbaku (WCTCOH 2018) uliofanyika jijini humo kuanzia Machi 7 hadi 9, mwaka huu na wengine wakiwasili mwanzoni mwa mwezi huo, ni miongoni mwa waliotahadharishwa kuhusu ‘kubana’ matumizi ya maji.

Matamko kadhaa yakatolewa na sekretarieti ya WCTCOH2018 kupitia kwa Mwenyekiti wa kamati iliyoandaa mkutano huo, Profesa Harry Lando, Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Aaron Motsoaledi na Meya wa jiji hilo, Patricia De Lille.

Washiriki wa mkutano huo wakahamasishwa kuunga mkono jitihada za kudhibiti matumizi ya maji yasiyofaa, ili kukabiliana na upungufu wa rasilimali hiyo.

Ingawa tahadhari hiyo ilitolewa, mamlaka za utawala jijini Cape Town zimesema kuna maji ya kunywa ya  uhakika kwa wakazi wake na wageni wakiwamo waliokuwa washiriki wa mkutano huo kutoka takribani mataifa 100 duniani.

Lakini jambo la msingi likabaki kuwa juu ya watu `kujenga’ fikra kuhusu upungufu uliopo na hivyo kuchukua hatua za udhibiti wa matumizi ya maji.

Kwa upande wa utawala wa jiji hilo, ikaamriwa kwamba mtu mmoja anapaswa kutumia kutumia chini ya lita 50 za maji kwa siku, kutumia ‘bomba la kuogea’ ndani ya muda usiozidi dakika mbili na kupigwa marufuku kuoga kwenye sink hususani hotelini.

Pia ikaazimiwa kwamba matukio yote yanayofanyika jijini humo yanapaswa kutohusisha matumizi yasiyofaa ya maji ama kuwa katika kiwango cha chini kabisa.

Jitihada za kudhibiti hali hiyo zikifanyika, ikiwemo kuweka matenki ya uvunaji maji ya mvua na kusambazwa vimiminika vya kusafisha mikono ikiwamo kwa matumizi ya msalani.

Kwenye hoteli, migahawa na baa palikuwa na karatasi zinazotahadharisha  matumizi yasiyofaa ya maji.

Hali hiyo ipo pia kwenye baadhi ya hoteli na mabwawa ya kuogelea yamefungwa, mengine yakawekewa maji ya baharini ‘yaliyochakatuliwa’, lengo likiwa ni kupunguza matumizi ya maji yasiyo ya lazima.

Meya wa Cape Town, De Lille amesema ukame na ukosefu wa maji uliojitokeza umekumbusha namna uwiano uliopo kati ya maisha na kifo.

Jiji hilo limepanga kuyafunga mabomba kwa watu wanaofikia milioni nne, likibaki kuwa moja ya majiji duniani yanayoendelea huku likikabiliwa na upungufu wa maji.

Hali hiyo itasababisha watu hao kupanga mistari kwenye foleni, wakilindwa na askari wenye silaha wakati wakipokea msaada wa maji ya kunywa.

Ongezeko la watu na ukame, ukichochewa na mabadiliko ya tabia nchi vinatajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vinavyosababisha maeneo ya miji kukabiliwa na uhaba wa maji.

Kina cha maji kwenye mabwawa yanayosambaza maji kwenye jiji hilo lenye kiwango kikubwa cha utalii, kimeshuka kufikia asilimia 10  ikilinganishwa na asilimia 20 ya mwaka jana.

Mbali na ukosefu wa mvua unaochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi, Cape Town inakabiliwa na mahitaji ya maji yanayoongezeka kwa viwango tofauti.

Idadi ya watu jijini Cape Town imeongezeka kufikia watu milioni 3.74 (kwa mujibu wa sense ya mwaka 2011). Kwa hali hiyo, idadi hiyo itakuwa imeongezeka zaidi kwa mwaka huu.

Muasisi asasi ya Bloomberg ambaye pia aliwahi kuwa Meya wa Jiji la New York kwa mihula mitatu,  Michael Bloomberg, amesema  “ukame uliopo hapa Cape Town unapaswa kuwaamsha wote wanaodhani kwamba mabadiliko ya tabia nchi ni tishio lililo mbali.”

Bloomberg ambaye ni mmoja wa `matajiri bilionea’ wa Marekani ni Balozi wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

“Tayari mabadiliko ya tabia nchi yapo hapa, yamesababisha ukame na tunahitajika kuchukua hatua ili kuepuka madhara zaidi,” amesema Bloomberg.

Bloomberg amesema, “mamlaka za jiji na jumuiya ya wafanyabiashara wanasaidia katika kutoa misaada, lakini ngazi zote katika jamii, mataifa na mabara  wanapaswa kuchukua hatua pana zaidi.”

Balozi huyo wa mabadiliko ya tabia nchi akatembelea bwawa la Theewaterskloof ambalo ni kubwa kuliko yote, likisambaza maji ukanda wa magharibi mwa Afrika Kusini.

Katika ziara hiyo, Bloomberg akafuatana na wanamazingira mahiri na wataalamu wa masuala ya maji, akapata maelezo fasaha kuhusu ukame na wakajadili namna bora ya kukabiliana na hali iliyopo.

Wanamazingira na wataalamu wa maji waliokuwapo ni pamoja na Christine Colvin, Meneja Mwandamizi wa Majibaridi wa Shirika la Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) nchini Afrika Kusini.

Mkurugenzi wa Majisafi na Majitaka wa jiji hilo, Peter Flower, Mkurugenzi Mtendaji wa Makazi Yasiyorasimishwa, Maji na Taka wa jiji hilo,  Dk. Gisela Kaiser na Dk. Kevin Winter wa Taasisi ya Utafiti wa Maji ya Chuo Kikuu cha Cape Town.

Christine Colvin wa Shirika la Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) nchini Afrika Kusini, amesema upungufu wa maji jijini humo una madhara sit u kwa upatikanaji wake, lakini pia katika uhusiano wa mtu na rasilimali hiyo.

“Ghafla maji yamekuwa suala linalomgusa kila mtu kama familia na sekta binafsi wanahangaika kutafuta mbadala..” amesema.

Kwa hali ilivyo sasa, inahitajika kuwapo vyanzo vingine vya maji na kuitathmini miundombinu iliyopo sasa. Maeneo yenye vyanzo vya maji ambavyo ni sehemu ya miundombinu hiyo ni muhimu vikahifadhiwa vizuri.

Vinahitaji uangalizi wa karibu na uwekezaji vikiwa ni sehemu ya maendeleo ya uchumi wa jiji hilo kwa miaka ijayo.

By Jamhuri