Na Charles Ndagulla, Moshi

WAKULIMA wa zao la kahawa nchini hawana budi kufurahia mabadiliko ya taratibu mpya  za usimamizi wa sekta ndogo ya kahawa baada ya kupitishwa kwa uamuzi mgumu ambao utachangia kuleta ufanisi katika uzalishaji wa zao hilo.

Miongoni mwa uamuzi huo magumu ni pamoja na wanunuzi binafsi kupigwa marufuku kwenda vijijini kunuua kahawa ya wakulima ambako sasa jukumu hilo linaachwa kwa vyama vya msingi ya ushrika na vyama vikuu vya ushirika.

Kabla ya uamuzi huo, kampuni za watu binafsi zilikuwa zikinunua kahawa kwa wakulima na hivyo kuwafanya baadhi ya wakulima kuuza kahawa yao ikiwa mbichi kwa lengo la kupata fedha za chapchap hatua ambayo inachangia kuwapo kwa kahawa chafu na isiyokuwa na ubora.

Uamuzi huo ulitangazwa hivi  karibuni mjini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Dk.Charles Tzeba katika mkutano wa tisa wa wadau wa kahawa  ulioandaliwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wawakirishi wa vyama vya ushirika nchini, wawakirishi wa halmashauri za wilaya zinazolima kahawa, wadau wa kahawa na wawakirishi kutoka taasisi za fedha, Benki ya ushirika (KCBL) na Bodi ya stakabadhi ghalani.

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, vyama vya msingi vya ushirika vitakuwa na jukumu la kukusanya kahawa kutoka kwa wakulima, kuipeleka kwenye viwanda kwa ajili ya kukoboa na baadaye kuipeleka mnadani.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo amesema kuanzia sasa wanunuzi wote wa kahawa sharti wawe na cheti cha ulipaji kodi.

Amesema bei atayolipwa mkulima itapatikana pale kahawa itakapouzwa mnadani na kwamba vyama vya ushirika vitalipwa ili navyo viwalipe wakulima fedha zao kulingana na kahawa waliyokusanya.

Katika mabadiliko hayo ya uendeshaji mpya wa minada, kwa sasa wauzaji wa kahawa mnadani hawataruhusiwa kupeleka bei ya akiba na badala yake jukumu hilo litaachwa kwa dalali atakayekuwa na wajibu wa kuandaa bei ya akiba kulingana na bei ya  soko la kahawa.

Vyama vikuu vya ushirika navyo vimeonywa kutokupeleka kahawa mnadani ikiwa imechanganywa na ya vyama vingine lengo ni kulinda ubora wa kahawa na bei ya vyama vitakavyoweka juhudi katika kuzingatia ubora wa kahawa na kahawa ya kila chama cha msingi itaonekana kwenye katalogi.

“Bodi ya kahawa itatoa bei elekezi ya kahawa kwa vyama vya msingi vya ushirika na vyama vikuu vya ushirika zitakazofaa kulipwa kama malipo ya awali,” amesema Kimaryo.

Kuhusu wenye mashamba makubwa ya kahawa, Kaimu Mkurugenzi huyo amesema kuwa nao watatakiwa kwenda kuuza kahawa yao mnadani tofauti na zamani ambako walikuwa wakiuza kahawa yao moja kwa moja nje ya nchi.

Hata hivyo, amesema wale ambao wana mikataba ya mauzo ya muda mrefu na wateja wao wa nje, Bodi ya kahawa itaandaa utaratibu kupitia minada kutoathiri mikataba yao.

Akizungumzia ugharamiaji wa mikakati, Kimaryo amesema shughuli zote ambazo awali zilikuwa chini ya Mfuko wa Wakfu wa Kahawa (TCDF) ambao ulivunjwa na Waziri Mkuu hivi karibuni, zitafanywa na Bodi ya Kahawa.

Shughuli hizo ni pamoja na kuhamasisha uzalishaji wa miche bora ya kahawa, kugharamia mikutano ya wadau wa kahawa na kuwezesha upatikanaji wa pembejeo za kilimo.

Katika hatua nyingine, Mkoa wa Kagera bado umeendelea kuwa kinara wa uzalishaji ambako katika msimu wa 2017/18 umezalisha tani 12,131 ukifuatiwa na Ruvuma iliyozalisha tani 11,914.

Mkoa wa Songwe unashika nafasi ya tatu ukizalisha tani 8,690, huku Mkoa wa Kilimanjaro ukikamata nafasi ya nne kwa kuzalisha tani 2,968 na Arusha ikifunga tano bora ya mikoa inayoongoza kwa uzalishaji baada ya kuzalisha tani 2,312.

Katika uzalishaji wa kahawa duniani, Uganda na Ethiopia bado zimeng’ang’ania kwenye kumi bora ya nchi zinazozalisha kahawa kwa wingi dunia ambako Ethiopia ipo nafsi ya tano na Uganda ikiwa nafasi ya tisa.

Brazil inakamata nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Vietnam wakati Colombia iko nafasi ya tatu na nafasi ya nne ipo Indonesia, Honduras nafasi ya sita na India nafasi ya saba, Peru nafasi ya nane na Guatemala ikishika nafasi ya 10 nyuma ya Uganda.

Nchi hizo 10 ndizo zilizoshikilia roho ya kahawa duniani kwani zinazalisha aslimia 88 ya kahawa yote inayozalishwa duniani na aslimia 12 inaachwa kwa nchi nyingine ikiwamo Tanzania.

Kuhusu hali ya bei ya kahawa nchini, Kaimu Mkurugenzi huyo wa Bodi ya Kahawa, anasema katika msimu wa 2016/2017 wakulima waliouza kahawa yao wakati bei ikiwa nzuri sokoni walipata wastani wa Sh 5,000 kwa kilo ya Arabika.

Amesema wastani wa bei kwa msimu ni Sh 4,000 kwa kilo ya kahawa ya Arabika, huku wakulima wanaozalisha kahawa aina ya Robusta walilipwa wastani wa Sh 1,200 hadi 1,400 kwa kilo ya maganda.

“Msimu huu 2017/2018 bei ya kahawa imeshuka kutokana na kushuka kwa bei ya kahawa katika soko la dunia. Bei ya mkulima imekuwa ni ya wastani kutokana na ushindani unaotokana na kiwango kidogo cha uzalishaji,” amesema.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa katika misimu saba iliyopita uzalishaji wa zao la kahawa nchini umekuwa ukipanda na kushuka huku baadhi ya wakulima wakidaiwa kulipa kisogo zao hilo na kugeukia mazao mseto kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na bei ndogo.

Katika msimu wa 2010/2011 uzalishaji wa kahawa ulikuwa tani 56,790.0, lakini msimu uliofuata wa 2011/2012 uzalishaji ulishuka kwa kasi ya kutisha na kufikia tani 33,086.7 na ulipanda tena msimu wa 2012/2013 na kufikia tani 71,319.1.

Msimu wa 2013/2014 tani 48,761.9 zilizalishwa na tani hizo zilishuka tena msimu wa 2014/2015 na kufikia 42,768.0 na kupanda tena katika msimu wa 2015/2016 hadi tani 60,188.0 kabla ya kuporomoka msimu wa 2016/2017 hadi tani 46,963.0.

Amesema changamoto nyingine inayochangia kushuka kwa uzalishaji ni pamoja uwekezaji kidogo kwenye uzalishaji kutoka taasisi za fedha na wakulima wengi kutotumia kikamilifu mashine za kati (CPU) za kumenyea kahawa.

Kuhusu soko la nje amesema Italia imezipiku nchini za Japan, Ujerumani, Marekani na Ubeligiji kutokana na kuongoza kununua kahawa ya Tanzania kwa aslimia 25.18 ikifuatiwa na Japan (16.89%), Ujeruman (11.32%), Marekani(10.86%), huku Ubeligiji ikishika nafasi ya tano kwa aslimia 9.41.

By Jamhuri