Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema ukaguzi na udhibiti wa ndani ya chama hicho kwa sasa ni zaidi ya kile kilichobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Kwa mujibu wa Dk. Bashiru, Kamati ya Kuhakiki Mali za CCM aliyoiongoza kwa takriban miezi mitatu ilibaini mengi zaidi ya kinachobainishwa na CAG, na anatumaini kuwa ripoti ijayo ya ukaguzi wa CAG itakuwa na mambo mengi mazuri kuhusu CCM.

Katika mahojiano yake kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa na Gazeti la JAMHURI mwishoni mwa wiki iliyopita nyumbani kwake Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Dk. Bashiru amesema ukaguzi wa CAG miaka iliyopita ulikuwa hauhusu baadhi ya mali za CCM zilizokuwa ‘zimeporwa’ kinyemela na baadhi ya wanachama, na kwamba kwa sasa daftari la orodha ya mali za chama hicho limesheheni.

 “CCM imejikagua na kujihakiki kwa ukamilifu. Tumefanya kazi kubwa kiasi hata cha kumsaidia CAG kufanya kazi yake vizuri ya ukaguzi, tumerejesha mali ambazo mwanzoni hakuwa anaweza kuzikagua kwa kuwa hazikuwamo kwenye orodha ya CCM ingawa zinamilikiwa na chama hicho,” amesema Bashiru.

Akifafanua zaidi upana wa sekta ya udhibiti, Dk. Bashiru amesema Tanzania imepiga hatua katika udhibiti wa sekta kadhaa kupitia vyombo vya udhibiti kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika masuala ya sekta ya fedha na uchumi, udhibiti wa nishati na maji kupitia EWURA na hata kazi inayofanywa na CAG lakini anasema kuna haja ya kutazama suala la udhibiti katika mtazamo wa kidunia, kwa kuwa wale aliowaita ‘wakubwa’ wamekuwa ndio wadhibiti wa wadhibiti katika mwelekeo wa kupoteza maana hasa ya udhibiti.

Katika hilo, Dk. Bashiru amehoji: “Nani hasa mdhibiti wa wadhibiti? Ni muhimu kuwa na udhibiti wa ndani ya nchi, CAG anafanya kazi ambayo nasi kwenye CCM tunamuunga mkono na kimsingi, CCM tumejikagua hasa na kujidhibiti kwa viwango vikubwa mno baada ya kazi ya Kamati ya Uhakiki wa Mali za Chama.

 “Lakini katika ngazi ya dunia, tunaona Shirika la Fedha Duniani (IMF) likidhibiti mifumo ya sera za uchumi na masuala ya fedha pamoja na Benki ya Dunia, mifumo ya kibiashara inadhibitiwa na Shirika la Biashara la Dunia (WTO), nani anadhibiti viwanda vya silaha na biashara ya silaha kwa masilahi ya dunia?

“Kwa hiyo, mjadala wa udhibiti hapa nchini unapaswa kutazamwa kwa mapana zaidi ya suala la CAG. Nasema ni muhimu udhibiti wa ndani, lakini nchi za dunia ya tatu, na hasa Afrika lazima itazame ngoma hizi zinazopigwa na wakubwa. Tusicheze ngoma hizo bila kutafakari,” amesema Dk. Bashiru.

CAG na udhibiti

Dk. Bashiru alizungumzia suala la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika picha pana zaidi, akitafakari kwa kuhoji  maswali yanayoweza kuibua mjadala si tu wa kitaifa, bali hata nchi za kusini mwa Afrika na dunia ya tatu kwa ujumla.

“Tujiulize, nani mdhibiti wa wadhibiti? Ni wananchi? Kazi ya udhibiti isiwe kazi ya kipolisi. Udhibiti si dhana ya kipolisi, ni dhana ya kisiasa kwamba wenye nguvu ni wananchi, kwa hiyo madaraka yote ya mwisho kuhusu udhibiti yawe kwa wananchi.

Mimi ni Katibu Mkuu wa CCM lakini nimekuwa kiongozi wa kamati ya kuhakiki mali za chama, haya aliyoyaona CAG ni madogo, kimsingi, ukaguzi wake wa hesabu za chama katika miaka iliyopita haukuwa unahusisha mali zote za chama, kwa nini? Kwa sababu hapakuwa na orodha ya mali zote.

“Sasa chama kimefanya kazi yake vizuri, kimejikagua kwanza kikamilifu kupitia kamati ya uhakiki wa mali zake, zote sasa zimo kwenye orodha ya mali za chama, mkaguzi ataweza kuzikagua na mimi nina uhakika ripoti ijayayo ya CAG itakuwa nzuri mno kwa chama chetu.

Kuhusu ripoti ya sasa ya CAG, wadhamini wa chama wamo wao ndio wataelekeza cha  kufanya na sisi kama watendaji wakuu ambao tumekwishafany akazi kubwa ya kuweka sawa mali za chama ikiwa ni pamoja na kuzihakiki, tutatekeleza maelekezo yao.

“Nilikuwapo mwenyewe kwenye ‘exit meeting’ ya CAG (mkutano wa mashauriano ya mwisho kuhusu ukaguzi) tulijieleza na tumepata hati safi, najua mwakani katika taarifa yake hali itakuwa nzuri zaidi kwa kuwa kwanza, tunalo daftari timilifu la orodha ya mali za chama, pili, tumeweka mfumo imara zaidi wa kudhibiti mapato.

“Lazima tujue kuwa kazi ya CAG pekee haitoshi, chama au vyama vya siasa ni lazima vijenge mifumo yao ya udhibiti na ukaguzi, sisi tumekwisha kufanya hivyo.

“Lakini tukiachana na hilo la CAG ambalo ni jambo jema kujikagua wenyewe, tupanue fikra zetu zaidi kama taifa. Tutambue kuwa wakati CAG anaendelea kufanya kazi yake katika miaka ya nyuma, watumishi hewa walikuwapo na matatizo mengine mengi, sasa utaona kazi ya CAG pekee haitoshi, kikubwa ni kuweka mifumo rasmi thabiti ya udhibiti.

“CAG hatungi sera, serikali ndiyo yenye jukumu hilo na vyombo vingine, CAG kazi yake ni sehemu tu ya udhibiti, hapa nchini kuna mamlaka nyingine nyingi za udhibiti, tumeona Benki Kuu (BoT) inavyodhibiti maduka holela ya fedha kigeni.

“Hebu tujitazame kitaifa na kimataifa hasa Afrika. Kama kweli tunataka kujiweka vizuri katika udhibiti na ukaguzi, tujiulize, nani anadhibiti wadhibiti? Kuna IMF katika utawala ama mifumo ya fedha, anavyo vigezo vyake, kuna WTO wanavyo vigezo vyao katika eneo la biashara, kuna Benki ya Dunia anavyo vigezo vyake katika sera za uchumi na mikopo. Hivi ni vyombo vya udhibiti na ukaguzi pia. Je, nani anavidhibiti? Ni Bunge la Tanzania? Ni Umoja wa Afrika (AU)? Vipi kuhusu udhibiti wa viwanda vya silaha, kwa hiyo, ni kweli udhibiti na ukaguzi wa ndani ni jambo muhimu lakini katika eneo hilo hilo tuitazame dunia katika jicho pana, sekta ya udhibiti na ukaguzi nchi za Afrika inabidi iitazame kwa upana sana, tutazame mifumo ya kidunia.

Matokeo ya udhibiti

Katika mahojiano yake na Gazeti la JAMHURI, Dk. Bashiru amesema kuna mafanikio makubwa katika ukaguzi na udhibiti ndani ya CCM bila hata nguvu ya CAG.

 “CCM tumefanikiwa sana kujidhibiti. Kwa mfano, Mwanza akaunti inasoma salio la milioni hadi 400, hii ni matokeo ya udhibiti wa mapato. Awali, kwa sehemu kubwa mapato yalikuwa yanapotelea mifukoni mwa watu wachache, hasa viongozi.

“Pale Amana (jijini Dar es Salaam) chama kinamiliki eneo la mita za mraba 1,500, eneo hili lilikasimiwa kwa mtu binafsi, alipewa hati ya eneo na akaishikilia kwa zaidi ya miaka 20 kama ndiye mmiliki.

 “Utaratibu unataka hati hizi zitunzwe makao makuu ya chama, lakini hati hii haikuwapo CCM makao makuu. Maana yake ni kwamba haikuwamo kwenye orodha ya mali za chama. Sasa tumeirejesha hati hii kwenye mikono ya chama.

“Sasa hapa kuna mambo mawili. Kwanza, kurejesha mali za chama mikononi mwa chama. Pili, namna ya kuzisimamia na kudhibiti mapato. Katika mfano huu wa eneo la Amana, baada ya kuirejesha hati, wanachama na viongozi waliendelea na mchakato wa kutafuta upya wapangaji na bahati mbaya, baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Ilala wanadaiwa kuomba rushwa ili kufanikisha wapangaji wapate eneo, hili suala lipo mahakamani.

Kujipunguzia posho

Dk. Bashiru amezungumzia mtazamo wake kuhusu nafasi aliyonayo kwenye chama hicho kikongwe.

 Katika hilo, amediriki hata kujifutia baadhi ya stahili zake kwa nafasi aliyonayo lakini hatua hiyo haijamridhisha kwa kuwa haijaleta mageuzi anayoyalenga katika kuboresha masilahi ya watumishi wa chama hicho.

Dk. Bashiru amejiondoa sehemu ya posho ya kikanuni inayoitwa ‘posho ya huduma kwa kiongozi’.

“Hata hivyo unapojipunguzia wewe haina maana kwamba tatizo limekwisha. Bado tatizo halijakwisha, unapojipunguzia ama kujikata fedha wakati hatua hiyo haiongezei kipato chochote wenzako moja kwa moja kunazalisha swali jingine muhimu sasa, tunajenga mfumo gani imara wa kuimarisha masilahi ya watumishi? Hili bado tunalifanyia kazi na wenzangu,” amesema.

Kulinda mabadiliko

Amesema moja ya changamoto iliyopo CCM kwa sasa ni kuyalinda mabadiliko makubwa yenye manufaa kwa chama hicho, na kwamba, namna ya kuyalinda kwa uhakika ni kuanzisha mafunzo ya uongozi na itikadi ili hatimaye kujenga taasisi imara.

 “Ujenzi wa taasisi imara za kisiasa hauwezi kutokea tu kwa matamko ama kwa ubunifu wa muda mfupi wa viongozi.  Kwa hiyo katika kujenga taasisi ni lazima pia kuwalenga vijana.

 “Kinachotusumbua mimi (Katibu Mkuu – CCM) na Mwenyekiti wa chama (Rais John Magufuli) kwanza; ni kukigeuza chama kiwe chama cha wanachama, chama kinachoendeshwa kwa vikao vya wanachama, mafunzo na semina, na hivi ndivyo Mwalimu Julius Nyerere alivyojenga chama, na alipong’atuka aliendesha programu ya kuimarisha chama. Na kwa sasa tunaendelea na hilo, tumefufua vyuo vyetu vya mafunzo, kule Tunguu – Zanzibar, kule Naibu Katibu Mkuu wa chama anafanya kazi kubwa, lakini tunacho chuo chetu Ihemi, Iringa ambacho si tu kinatoa mafunzo ya itikadi bali hata mafunzo ya ujasiriamali.

“Kuna miradi ya chama inafanyika Ihemi kwa  njia ya mafunzo, kwa mfano utengenezaji wa fulana, kofia na bendera za chama,” amesema.

 Alipoulizwa hali itakuwaje wale wanaopata mafunzo kuhama chama, kisha kujiunga na upande shindani wa kisiasa dhidi ya CCM katika mazingira ya siasa za vyama vingi, Bashiru alijibu: “Haya ni mafunzo ya kujenga imani ya kisiasa na kifikra. Mtu anayejitoa kwenye chama baada ya kupata mafunzo haya anaweza kuwa na sababu zenye mashiko labda.

 “Lakini katika hali ya kawaida, inatarajiwa mtu aliyeiva kwa mafunzo hawezi kuhama chama bali atashiriki kukiimarisha zaidi. Imani yetu ni kwamba hatua hii ya mafunzo itasaidia mno chama na taifa kwa ujumla,” amesema.

Jambo la pili alilosema linawasumbua yeye na mwenyekiti wake ni kukifanya chama (CCM) kusimamiwa kwa dhati katika misingi ya kifalsafa, kiitikadi na kisera kama ilivyoanishwa na waasisi wa chama hicho.

 Anasema ufanisi pekee katika hilo ni kuhakikisha wakati wote CCM inasimamia haki na usawa. Kujenga jami yenye haki na usawa halisi.

“Changamoto iliyopo ni kwamba bado kuna mifumo inayoendekeza ama iliyojengwa katika misingi ya ubinafsi. Kwamba usawa unakuwa si usawa wa binadamu wote, bali unakuwa usawa wa watu wachache wanaotumia vichochoro vya fursa mbalimbali zikiwamo za kisheria kukandamiza wengine.

“Kwa sehemu kubwa nchi yetu imekuwa na vijana wengi na hii ni fursa ya kuibadilisha jamii hiyo iwe na mtazamo chanya zaidi kwa taifa. Vijana ninaowazungumzia hapa ni wale waliozaliwa baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka mwaka 1985, vijana wenye umri wa miaka 34 kushuka chini, wengi wao hawa hawajui kiasi cha kutosha kuhusu misingi hiyo miwili, haki na usawa iliyotumika kujenga chama hiki. Miongoni mwao wanajua tu kwamba unapodai haki basi ni kuhusu mtu binafsi, haki binafsi, hawaitazami haki na usawa kwa upana wake.

 “Kama jamii nzima haijajengwa katika misingi ya kulinda haki za wote, kwamba iachwe tu kuna wenye haki zaidi ya wengine, ni dhahiri tutaangamiza taifa hili, tutapata shida zaidi.

 “Tumeona kuna shida katika baadhi ya nchi za wenzetu ambao wamepuuza mambo haya ya haki na usawa katika upana wake. Tazama Afrika Kusini ya leo, Ethiopia na kwingine Afrika, utaona kuwa Afrika imepasuka, kuna matabaka miongoni mwa raia, kuna pengo kubwa kati ya walionacho na wasionacho na kwa hiyo utakuwa unajenga jamii yenye hasira, ndicho kinachotokea Afrika Kusini kwa wenzetu. Mtazamo wa namna hii ndilo jambo linalotutesa mimi na mwenyekiti, tunawezaje kukibadilisha chama kiwe taasisi imara katika kulinda usawa na haki kwa mapana yake, wakati wote, lakini tunashukuru kuna hatua tumeanza kupiga kurejea kule kwenye misingi ya chama iliyoasisiwa na waasisi wetu.

 “Tunakiri kuwa vijana hawakuandaliwa vizuri katika hilo, kwa hiyo ni lazima juhudi za kutosha zifanyike kwa kuwa wao ndio watakaoendeleza taifa hili kama ambavyo wengine wamepokea kutoka kwa waasisi,” ameeleza.

Ukali hautoshi

Dk. Bashiru amesema haitoshi kuwa wakali dhidi ya vitendo vya ufisadi.

“Ukali dhidi ya ufisadi ni jambo muhimu sana lakini haitoshi. Jambo jingine kubwa zaidi katika mazingira hayo ni kujenga uelewa wa wananchi dhidi ya mfumo unaozalisha mafisadi.

 “Matumizi ya nguvu dhidi ya ufisadi, unyonyaji hayana nafasi sana, labda iwe ni matumizi ya nguvu za hoja, na hili unalifanikisha kupitia mafunzo.

2071 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!