Nina kila sababu na nia ya kutoa pongezi na kongole kwa Watanzania kumudu kuendesha kampeni ya uchaguzi na kuwachagua madiwani, wabunge na rais kwa njia ya utulivu na amani.

Oktoba 25, 2015 imepita, ikiwaacha Watanzania hao katika sura mbili tofauti – ya huzuni na furaha. Baadhi yao wamejaa huzuni na masikitiko kutokana na kushindwa kupata viongozi wawatakao kuongoza nchi. Na wengine wamefurahi na kujisifu kuwapata viongozi waliowakusudia kuwa viongozi wa kuongoza nchi hii.

Mchakato huo wa kupata viongozi uliendeshwa na kusimamiwa na vyama vya siasa, kila kimoja kikiwa na nia ya kutaka kushika dola. Mvutano mkubwa ulikuwa kati ya vyama vya upinzani kwa upande mmoja na upande wa pili chama kinachotawala kiking’ang’ania kuendelea kushika dola.

Kati ya vyama 22 vya siasa tulivyonavyo nchini, ni vyama vinane ndivyo vilivyotia nchi katika mshikemshike viliposimamisha wagombea wa udiwani, ubunge na urais. Vyama saba kambi ya upinzani vikiwamo ACT-Wazalendo, ADC, CHAUMA, NRA, TLP, UPDP na CHADEMA (na UKAWA wake) upande wa pili ni chama tawala-CCM.

Mvutano wa kambi mbili hizo ulitia hobelahobela kila eneo la nchi na kuwatumbukiza Watanzania katika upenzi, ushabiki na uitikadi uliozaa milipuko ya kisiasa hata kutupiana vijembe na kejeli; ilimradi mambo yalikuwa mshikemshike.

Yote hayo yamepita. Kambi ya Upinzani kura hazikutosha; na hivyo  hawakuweza kushika dola. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kura zimetosha na hivyo kuendelea kushika dola. Hapa nawajibika kutoa pole na pongezi kwa Kambi ya Upinzani na kutoa heko na kongole kwa chama tawala.

Napenda kusema Watanzania wana kiu kubwa ya mabadiliko. Wanahitaji mabadiliko ya kweli. Chama Cha Mapinduzi sasa hakina hiyari katika kuleta maendeleo ya watu, haki na usawa miongoni mwa Watanzania. CCM inalazimika kwa udi na uvumba kuleta mabadiliko ya kweli nchini, Tanzania.

Blaa blaa zimeisha na zimepitwa na wakati kama anavyosema Rais wetu kutoka CCM, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli; “Hapa Ni Kazi Tu”  Mbiu hii ni tafsiri na mwendelezo wa mbiu isemayo UHURU NA KAZI  na UHURU NI KAZI ya chama mama (TANU). Kila mtu lazima afanye kazi. Kwa mtu aliye na uwezo wa kufanya kazi afanye kazi.

Unapofanya kazi unaua uzembe. Rais Magufuli hataki, hataki uzembe. Hawapendi wazembe kwani ni maadui wa maendeleo ya watu na Taifa. Unapofanya kazi ukweli unajenga utu na heshima yako na ni kipimo cha utu. Watanzania tukizingatia mbiu hiyo kwa kauli na vitendo tutajenga Tanzania Mpya.

Tukifanya kazi wanaume kwa wanawake mashambani, maofisini, viwandani na sokoni kwa dhati hatutatoa  mwanya wa rushwa na ufisadi. Hii ina maana ya kuwa mtu mkweli katika kauli na vitendo tunapotakiwa kutoa huduma kwa umma; kuwa muumini wa dini kwa kumuweka mbele Mwenyezi Mungu katika kumtii kwa kila  tendo jema.

Watanzania tumeipa kura za kutosha  CCM kwa imani kubwa ya kauli na ahadi za mgombea wake Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuieleza, kuichambua na kuitetea Ilani ya CCM katika nia yake ya kuendelea kupambana na changamoto kubwa nne zilizomo ndani ya Taifa hili la Watanzania.

Changamoto hizo kupambana na umaskini. Ingawa yapo mafanikio  ya kukua kwa uchumi na ongezeko la huduma za kijamii yaliyopatikana; bado takwimu zinaonesha kwamba asilimia 28.2 ya Watanzania ni maskini, wengi wapo vijijini kwa asilimia 75 wakitegemea kilimo na wa mijini wakiendesha biashara ndogo ndogo zisizo rasmi.

Pili, ni ajira kwa vijana. Lau kama tatizo la ajira lipo kwa dunia nzima, hapa nchini linazidi kukua kutokana na shule za sekondari na vyuo vyetu kutoa vijana wengi wahitimu na wasio na kazi. Mkazo ni kuanzisha viwanda vikubwa, vya kati na vidogo vidogo bila kuacha sekta za utengenezaji bidhaa mbalimbali nchini.

Changamoto ya tatu ni vita dhidi ya rushwa. Katika jitihada za kuinua uchumi na kuongeza huduma za jamii, adui rushwa hana budi adhibitiwe na kuondolewa ili Watanzania wasiendelee kuwa maskini. Vyombo vya kupambana na rushwa na ufisadi vitaimarishwa kupambana na maadui hao ikiwamo  na kuanzishwa Mahakama maalum kwa ajili ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.

Na nne, ni changamoto ya kudumisha ulinzi na usalama. Tangu tupate uhuru mwaka 1961 na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 Watanzania tumeishi kwa amani na mataifa jirani kukimbilia kwetu kwa hifadhi yanapotokea machafuko katika nchi zao. Jitihada zitafanywa kuimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa gharama yoyote.

Kauli na ahadi hizo hazina budi kutekelezwa kwa vitendo siyo kwa maneno matupu tena. Kazi ianze kwa kuondoa mfumo uliojenga uzembe, mahaba na ufisadi. Hapo Tanzania itawekwa ndani ya mabadiliko ya kweli. Vinginevyo mwaka 2020 CCM “bye bye”. 

 TUSEME INAWEZEKANA TUTIMIZE WAJIBU WETU.

1047 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!