Matokeo ya urais somo kwa CCM

Uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umehitimishwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo, na Dk. John Pombe Joseph Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiye rais wetu mpaka uchaguzi mwingine utakapofanyika.

Kwa mara ya kwanza ya historia yake na kwa historia ya chama cha Tanganyika African National Union (TANU), CCM kwa upande wa Bara imeshinda kwa kiasi kidogo kuliko wakati wa uchaguzi wote uliopita. Kama yupo aliyetarajia CCM kushinda sidhani kama alitarajia ushindi huo ungekuwa wa kiasi kikubwa kuliko ilivyotokea.

Na labda hali ingeweza kuwa mbaya zaidi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wamechagua mgombea urais ambaye alikuwa na tuhuma nzito za ufisadi ambazo wao wenyewe wamekuwa wakizitangaza kwa miaka mingi kwa Watanzania.

Kwa kufanya hivyo walijipokonya nguvu kubwa ya kukemea ufisadi wakati wa kampeni; jambo ambalo pengine limewapunguzia kura. Swali ambalo bila shaka litaulizwa kwenye tathmini za uchaguzi huu ni: mambo yangekuwaje iwapo CHADEMA wangeweka mgombea ambaye hana tuhuma kama hizo?

Lakini bado hili halibadilishi ukweli kuwa sababu kubwa ya matokeo haya ni nguvu na uungwaji mkono mkubwa ambao Edward Lowassa alihamishia kutoka CCM na kuupeleka CHADEMA na UKAWA. Alipohama baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM walihama naye na kura nyingi nazo zilimfuata huko huko.

Wengi waliopiga kura kuunga mkono upinzani ni wale mbao walipiga kura dhidi ya CCM na wagombea wake. Hazikuwa kura za upinzani, zilikuwa kura dhidi ya CCM. Na ndiyo maana kauli mbiu ya kampeni ya UKAWA ilikuwa “Tunataka Mabadiliko.” Ya aina gani, hatujui, lakini lililowekwa wazi ni kuwa yalihitajika mabadiliko. Na wapigakura wengi waliitikia mwito huo.

Suala hili, pamoja na ushindi mwembamba wa CCM ingekuwa ni somo jadidi kwa CCM na ingekuwa chachu ya kukaa chini na kutafakari nini kimesababisha kufikia hali hii. Bila shaka hili litafanyika.

Yapo masuala mengi yanayoweza kupunguza kura za CCM. Nitataja machache tu. Kwanza ni kuzidi kupungua kwa wale wanaokumbuka ahadi za TANU. Au tuseme ni kuzeeka kwa wale wanaofahamu chimbuko la CCM. Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wapigakura kwenye uchaguzi ulioisha wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 walifikia asilimia 57. Mtu ambaye alikuwa hajazaliwa mwaka 1977, kilipoasisiwa Chama Cha Mapinduzi, hana mzizi madhubuti unaomuunganisha na chama hicho. Idadi hii itazidi kuongezeka kadiri miaka inavyopita.

Hawa ni wapigakura ambao wameanza kupata uelewa wa kutambua masuala tofauti, lakini si ile historia kuwa chama kinachoongoza kilikuwa mstari wa mbele kupigania uhuru, haki, usawa, na utu wa mwanadamu nchini na kwenye Bara lote la Afrika. Hawa wanaifahamu CCM kwa mujibu wa maelezo ya CHADEMA na vyama vingine vya upinzani vikikosoa CCM kwa matatizo mengi tu; kubwa lilikuwa kuwapo kwa msururu wa kashfa za ufisadi. Kuvumilia tuhuma hizi ni vigumu kwa hawa kuliko wale wanaotafakari historia na kuota kuwa labda kuna siku historia itajirudia ya chama kile cha awali.

CCM wangepaswa kuweka mikakati ya kulinda kura za kundi hili kwa kuonekana inachukua hatua madhubuti dhidi ya shutuma za aina hii, na shutuma nyingine ambazo ni kero kwa wapigakura.

Kosa kubwa la CCM ni kuacha kuchukua hatua za kisiasa dhidi ya watuhumiwa na badala yake kuwapima kwa vigezo vya kimahakama. Kwa taarifa, hata nyoka anahitaji kujiparuza kwenye mwamba, jiwe, au sehemu ngumu kubandua gamba lake. Tunatarajiaje binadamu ambaye amejikita ndani ya mfumo unaompa faida kupamia majabali ili ajivue gamba yeye mwenyewe?

Mfumo wa sasa wa uongozi wa umma unampa faida kubwa mno aliyemo ndani yake. Turejee tena kwenye ahadi za TANU. Ya tano ilisema hivi: Cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.”

Sasa hivi watu wengi wanashawishika kugombea nafasi za uongozi kwa sababu tu wameona kuwa cheo kinaweza kuleta manufaa binafsi makubwa sana na kwa muda mfupi. Haya manufaa yangekuwa yanapatikana bila kuhusishwa na vitendo ambavyo vinakiuka maadili ya uongozi sidhani kama wapigakura wangelalamika sana.

Tatizo ni pale inapoonekana kuwa wapo viongozi wanafaidika isivyo halali na nafasi za uongozi. Hili nalo linaweza kuwa chanzo cha kupunguza kura za CCM mwaka huu.

Kupungua kwa mianya ya kumpa faida kiongozi wa umma kutokana na nafasi yake kunaweza kuwa sababu kubwa ambayo itapunguza msururu wa wasaka fursa ambao kutokana na matendo yao, badala ya kujenga imani kwa chama na serikali yake, wanabomoa imani hiyo na kuongeza kundi la watu ambalo liko tayari kutoa adhabu kali siku ya uchaguzi.

Chama Cha Mapinduzi kinapata fursa ya kupima matokeo haya na kutafakari hatua za kuchukua kupunguza kura dhidi yake katika uchaguzi mkuu ujao. Sina shaka kuwa uongozi wa CCM unafahamu vizuri tu vikwazo vya kushughulikia. Matunda ya uongozi mzuri kwenye chama chochote cha siasa ambacho pia kinaongoza serikali hayaishii kwa wanachama wake tu. Yataleta faida kwa nchi nzima.

Makosa ya uongozi na utendaji ndani ya CCM yapo mengi. Hata Dk. Magufuli amekiri hivyo. Ubishi unaweza kuwa makosa ni ya kiwango gani na yanaweza kuleta athari gani kwa CCM kama chama tawala.

Matokeo ya uchaguzi huu ni somo zuri sana kwa Chama Cha Mapinduzi. Wapigakura wengi walitaka kuiondoa tu CCM madarakani na walikaribia kufanikiwa kufanya hivyo. Ingekuwa muda mzuri sasa wa kurekebisha hizo kasoro zilizopo. Iwapo CCM hawajifunzi sasa ni dhahiri kuwa hawatajifunza tena.