simbaChama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Upanga Magharibi kiko hatarini kupoteza kiti cha udiwani baada ya kada aliyeteuliwa kuwania nafasi hiyo kudaiwa kuingia kwa figisufigisu mbali ya kuwa na tuhuma za kufungwa jela kwa makosa mbalimbali ya jinai.

Na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimetega uamuzi wa uongozi wa chama hicho wakitaka kutumia kete ya kisheria kuiengua CCM kwenye ushindani kabla ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Kwa upande wa CCM aliyepitishwa na uongozi wa CCM Wilaya ya Ilala ni Adnan Kondo ambaye inaelezwa kuwa alipigiwa kura na matawi mawili ya Minazini na Upanga siku ya Agosti mosi, mwaka huu badala ya manne kwa kuyatosa yale ya Upanga na Chuo Kikuu cha Muhimbili.

Mbali ya mizengwe, inaelezwa kuwa mteuliwa huyo, Adnan alikatiwa rufaa na wagombea wenzake akiwamo Godwin Mmbaga aliyeandika barua Julai 20, mwaka huu yenye kichwa cha habari ‘Kukiukwa kwa sheria na katiba ya CCM’ akilalamikia mambo matano likiwamo la mpinzani wake kukingiwa kifua na mama yake kwa kutumia madaraka aliyonayo.

Barua hiyo ilikwenda kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala na nakala kupelekwa ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Mwenyekiti wa CCM mkoa, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala pamoja na kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa wilaya ya Ilala, lakini hata hivyo haijafanyiwa kazi.

Sehemu ya baria hiyo inasema inamlalamkia Kondo kutumia cheo cha mama yake ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Sophia Simba; “Ndugu, ikumbukwe kuwa mwaka jana ofisi yako iliagiza kuanzishwa kwa tawi ambalo lilianzishwa ili kupata namna ya kumtwika mtoto wa Sophia Simba  Adnan K. Kondo nafasi mbalimbali za uongozi ili kumpa sifa punde atakapogombea nafasi ya Udiwani.

“Pia ilitambulika na taarifa kutolewa kwako na uongozi wa Kata ukikutaadharisha tawi hilo pamoja na kulenga kumjenga mtoto wa kiongozi aliyetajwa pia liliandaliwa kutumika kupachika wanachama ‘mamluki’ kutoka maeneo mengine ya mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa ilikwishafahamika mtoto  huyo wa kiongozi hawezi kupata kura za wakazi zikatosha.

“Hivi sasa yote uliyotaadharishwa, licha ya kudhihirisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kusababisha vurugu kubwa iliyokaribia kuangusha CCM kwenye mtaa wa Charambe, hivi sasa yote yamedhihirika kwa ukamilifu na iwapo ofisi yako haitochukua hatua sahihi na mapema, Uchaguzi Mkuu huu utakuwa na vurugu kubwa na kukiweka Chama cha Mapinduzi matatani,” anasema.

Mmbaga ametaja mambo yanayoendelea kutendeka ndani ya kata hiyo yakidaiwa kufanywa na kondo kuwa ni uongozi wa tawi la Tambaza na Jangwani Minazini kurundika wanachama ‘hewa’ kwenye leja zao kinyume na katiba ya CCM.

Wanachama hao wanadaiwa kukusanywa kutoka maeneo mbalimbali mkoani, kwenye viwanja vya mpira na kuwapiga picha kisha kuwapa kadi za CCM, pia kuwakusanya wagonjwa wanaopata tiba za dawa za kulevya kupitia mradi wa Methadone kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha tiba za akili na kupatiwa kadi za CCM kisha kulipwa sh 5,000 kwa ahadi ya kumpigia kura Adnan.

Mmbaga amedai kwamba viongozi wa matawi wa Tambaza na Jangwani Minazini wamegoma kuwasilisha orodha ya wanachama kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Kata na wamekutwa kwenye msikiti wa Budha uliopo makutano ya mtaa wa Mindu na Maliki wakiwa wanaongeza wanachama ilhali hawana sifa za uanachama kwenye matawi husika.

Pamoja na Kondo, kudaiwa kuitaka nafasi hiyo sheria za nchi hazimruhusu kuipata kwani kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari ameshawahi kutenda makosa ya kihalifu na kuhukumiwa miaka kadhaa makosa- ambayo anadaiwa kuyafanya nje ya nchi hasa Marekani.

Mwaka 2000 Kondo anadaiwa kufungwa miezi sita jela kwa kosa la wizi benki kwa kutumia kadi za kughushi, mwaka 2001 mwaka mmoja jela kwa kosa la hilo hilo, mwaka 2007 kifungo cha miaka mitano jela kwa makosa matatu; ambayo ni kujifanya mfanyakazi wa serikali, kujifanya askari polisi pamoja na kosa la wizi benki kwa kadi ya kughushi.

“Huu ni mpango wa kutaka kuvuruga uchaguzi Upanga Magharibi pamoja na mwenendo mzima wa uandikishaji wa wapigakura kwa mfumo wa BVR, sisi wana Upanga Magharibi tunalaani vikali kitendo cha kada huyu kutumia madaraka aliyonayo kuvuruga uchaguzi wa madiwani, ubunge na urais kata ya Upanga Magharibi,” anasema Beatrice Makani ambaye ni mwenyekiti wa CCM, Kata ya Upanga Magharibi.

Beatrice anamtuhumu Sophia Simba ambaye ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto na mlezi wa matawi ya Tambaza na Minazini, kuratibu wanachama wa CCM kutoka kata za Manzese, Mbagala na Mwananyamala kupiga kura kata ya Upanga kwa lengo la kumpa ushindi mgombea huyo kinyume na taratibu za chama.

Anasema kwamba uchaguzi huo ulizuiwa kufanyika, lakini taarifa zinasema kwamba baadaye Agosti mosi, mwaka huu kata za Minazini na Tambaza zilifanya uchaguzi chini ya Katibu mpya wa kata Abdul Malilima na kumtangaza Kondo kuwa ni mshindi kwa kura 1500.

Uchaguzi huo umelalamikiwa kuwa ulikuwa batili kutokana na kufanyika kwake njia za ujanja ujanja bila mwenyekiti kufahamu kinachoendelea sambamba na uteuzi wa katibu mpya wa kata aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi na kwamba hizo ni mbinu chafu kuhakikisha Kondo anakuwa diwani wa kata hiyo licha ya kutokubalika wanachama karibu wote.

Beatrice Makani akielezea uchaguzi huo wa kura za maoni katika kata hiyo anasema haukufanyika kutokana kushindwa kwa kuhakikiwa kwa majina ya wanachama katika leja katika vitabu vyote sambamba na mizengwe ya kila namna iliyojitokeza waliandamana kutoka ofisi za kata hadi ofisi za chama hicho Wilaya ya Ilala wakipinga uchaguzi huo. Anasema kutokana na kitendo hicho cha wanachama kuchukizwa na Simba, kutumia nafasi zake za Uwaziri na UWT kuvuruga uchaguzi huo kwa makusudi huku akifahamu kwamba mtoto wake anayeshinikiza awe diwani wa kata hiyo hana sifa zinazoweza kumpa ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu dhidi ya mgombea wa CHADEMA kupitia ukawa Juliana Ngodo, aliyekuwa meneja wa kampeni wa Kondo. Juliana alihama Julai 29, mwaka huu kujiunga Chadema.

Hata hivyo anasema Julai 29, mwaka huu, siku mbili kabla ya kura za maoni uongozi wa CCM Mkoa, ulimpeleka barua ya kusimamishwa ukatibu wa Kata ya Upanga, Joaviness Kimaro. Kata hiyo ina matawi manne ya Tambaza, Minazini, Chuo Kikuu cha Muhimbili na Upanga Magharibi kuhakikisha shughuli ya upigaji kura zinafanyika maeneo hayo licha kuonekana kwa matukio yenye viashiria vya kutotendeka kwa haki kwa wagombea wote.

Beatrice anasema aliongoza kikao cha kuhakiki majina ya wanachama katika matawi hayo manne na kugundua kuweko kwa dalili za kuvuruga upigaji kura na hivyo kazi hiyo ikaamishiwa wilayani ambako Mwenezi wa Kata, Kundya alihoji kuhorodheshwa majina ya marehemu na watu wasiofahamika kuwa ni wanaCCM ndani ya kata hiyo. 

“Julai 31, mwaka huu, baada ya kuhoji idadi hiyo ya wanachama ambao baadhi yao ni marehemu na wengine kutofahamika ndani ya kata hiyo wanaofikia zaidi ya 970 ikiwa ni kubwa ikitiliwa shaka na kila mmoja ambaye hakuwa sehemu ya mchezo huo mchafu, Katibu Mwenezi bwana Kundya alishambuliwa na wanachama waliokerwa na hoja yake kuhusu majina hayo, hadi sasa bado anatibiwa majeraha aliyoyapata katika Hospitali ya Mwananyamala,” anasema mwenyekiti huyo.

Pamoja na kufanyika uchaguzi uliompa idadi kubwa ya kura Kondo katika maeneo ya Tambaza na Minazini kwa uchaguzi batili ulioshinikizwa na Sophia Simba, Agosti 1, mwaka huu, Kamati ya Siasa ya Wilaya iliitisha kikao Agosti 4, mwaka huu na kuagiza uchaguzi huo ulikuwa batili hivyo urudiwe.

Hata hivyo kwa mashinikizo kutoka kwa Simba hakuna dalili za kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa kuwashirikisha wanachama wa kata hiyo, na kata mbili zilizosalia za haziwezi kufikiwa idadi ya kura alizozipata kondo dhidi ya wagombea wenzake Godwin Mmbaga anayetetea nafasi ya udiwani na Chikota.

Kutokana na tuhuma hizo JAMHURI ilimtafuta Kondo kutaka kupata ukweli wa tuhuma zinazoelekezwa kwake, akajibu: “Huo ni uzushi na mbinu za kutaka kufuta ndoto zangu za kuwa diwani. “Najua aliyeleta habari hizi ni mpinzani wangu, mimi nasema sioni sababu za chama kuniengua. Na kama kuna tuhuma CCM ina taratibu zake za vikao. Nadhani apeleke tuhuma zake huko, sio magazetini,” anasema Adnan.

JAMHURI ilimtafuta Sophia Simba – mama mzazi wa Adnan na muda wote simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno pia hakujibu. Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Abillahi Mihewa alisema yuko mkoani Dodoma kikazi na kuelekezwa atafutwe Katibu Mwenezi wa Mkoa, Juma Simba Gadaffi.

Licha kutaka Mwenezi atafutwe kwa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo, Mihewa ameandika barua akiagiza uchaguzi huo ufanyike kwa matawi mawili ya Upanga Magharibi na Chuo Kikuu cha Muhimbili ambayo hayakufanya uchaguzi na kusisitiza kwamba Tambaza na Minazini wao walifanya uchaguzi wao hivyo matokeo yake yanapaswa kutambuliwa.

“Nakutumia maagizo ya haraka kwamba uchaguzi huo ufanyike matawi mawili, Upanga Magharibi na Muhimbili University,” inaeleza sehemu ya barua ya Katibu Mkuu wa CCM Mkoa ya Agosti 4, mwaka huu kwenda kwa katibu wa CCM, wilaya ya Ilala, Ernest Chale. 

Katibu Mwenezi wa Mkoa, Gadaffi amesema chama hakina taarifa zozote kuhusu Kondo kwamba aliwahi kushitakiwa kwa makosa ya jinai nje na ndani ya nchi na kuongeza kuwa malalamiko yakifikishwa ndani ya chama kwa ushahidi unaokubalika yatashughulikiwa kwa vikao vya halali.

“Mtu anayeshinikiza uteuzi ufanyike kwa upande mmoja, huyo sio kiongozi, lakini hili la kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya jinai ndio nalisikia leo hii kutoka kwako mwandishi, ofisi haina ushahidi wowote unaoonesha Adnan kuwa aliwahi kufungwa nje ya nchi kwa kosa la wizi,” anasema samba.

Wakati Mwenezi huyo akizungumza hayo, Godfrey Lutego mwanasheria kutoka kampuni ya uwakili ya Haki Kwanza amelieleza JAMHURI kwamba sheria hairuhusu kwa mtu yeyote aliyetumikia adhabu ya kifungo cha miezi sita au zaidi kuwania nafasi yoyote ya uongozi wa kisiasa.

“Sheria haimpi sifa mtu aliyetumikia kifungo kutokana na makosa ya jinai iwe ndani au nje ya nchi na kama mtu akiwania nafasi ya uongozi na ikathibitika hivyo anapoteza nafasi yake,” anasema wakili Lutego.

Kutokana na tuhuma ambazo zimetolewa kwa Adnan inaelezwa kwamba Kata ya Upanga Magharibi itakuwa mikononi mwa CHADEMA, kupitia ukawa hata kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu. Kwa kuzuia kurudiwa kwa uchaguzi huo kumewanyima baadhi ya makada wa chama hicho kumchagua kiongozi wanaomtaka akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema ambao ni wakazi wa kata hiyo.

1855 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!