Ni ukweli usiopingika kwamba kauli zilizotolewa na viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita kwamba chama hicho hakiwezi kukabidhi nchi kwa njia ya makaratasi (kura) zimethibitisha kuwa utawala wa kidemokrasia Tanzania hauna nafasi.

Kauli hizo za viongozi wa CCM zimechangiwa kwa kiasi kikubwa na hofu ya kukataliwa na Watanzania waliokichoka chama hicho kinachojiendesha kwa mtindo uleule waliokuwanao wakoloni weupe. Wao kwa ujeuri tu wakajigeuza “wakoloni weusi” waliojiwekea uhalali wa kuwatawala ndugu zao kwa njia halali au haramu.

Kutokana na yale yanayoendelea huko Zanzibar na CCM wanaelewa kwamba wameshindwa vibaya, wanachotafuta sasa ni kuingiza ubabe na kuwalazimisha wananchi kuongozwa na chama hicho hata kama wamekataliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Niliwahi kueleza katika makala zilizopita kuhusu ubabe na udikteta unavyochukua nafasi kubwa kwa vyama vya siasa ambavyo vimekataliwa na wananchi kwa njia ya kura, kutokana na kujisahau kwa viongozi wake ama kushindwa kuwatumikia wananchi.

Kwa mfano CCM ilianza kupoteza umaarufu wake kwa Watanzania baada ya mwasisi wake, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuachia nafasi yake ya uenyekiti kwa Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi mwaka 1987. Hapa ndipo matajiri walianza kujiingiza kwa wingi ndani chama na kuteka mamlaka yote.

Wananchi wengi waliokosa ukwasi hawakutambuliwa na chama wala kuthaminiwa kama ilivyokuwa wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere.

Baada ya matajiri kukiteka chama hicho, ikasukwa mikakati mizito ya kulizika Azimio la Arusha kwa kuasisi lile la Zanzibar kwa lengo la kuua miiko yote iliyokuwa dira ya maisha ya viongozi wa umma.

Chama kikashindwa kuisimamia Serikali na matajiri waliojiingiza kama makada maarufu wakakielekeza katika kujilimbikizia mali, ikiwa ni pamoja viwanja vya michezo na baadhi ya majengo yanayodaiwa kumilikiwa na CCM.

Ufisadi ukashika kasi, kodi hazikukusanywa. Serikali ya awamu ya tatu ikasifika kwa kukusanya kodi, kuuza mashirika ya umma kwa makada wa CCM walioitwa wawekezaji ambao wengi wao wakavigeuza viwanda hivyo kuwa mazizi ya kufugia mifugo.

Wengine wakauziwa mashamba ya umma na vijiji vilivyokuwa jirani na mashamba hayo na hivyo kuongeza chuki kwa wananchi dhidi ya chama hicho cha siasa.

Umaarufu wa CCM umeporomoka zaidi kwa serikali ya awamu ya nne iliyozidisha pengo kati ya matajiri wachache na wananchi wengi maskini ndani ya nchi yao. Kutokana na madudu yaliyofanywa na CCM wananchi kwa nia moja waliamua kumwadhibu adui yao kwa njia ya kidemokrasia kwa kukikataa chama hicho kila kona.

CCM bila aibu na kuendekeza siasa za kihuni kila eneo kilipokataliwa na Watanzania waliokusudia kipumzike na kujifunza kuongoza kikiwa nje ya madaraka kimezuia haki ya Wazanzibar kwa kuzuia kutangazwa matokeo ya urais na kutaka uchaguzi urudiwe.

Sababu zao hazina mashiko! Kisa mgombea urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif amepata ushindi na kumbwaga Dk. Shein wa CCM.

Inaeleweka wazi kuwa Jecha alishinikizwa na viongozi wa CCM ayafute matokeo baada ya kuyapata matokeo yote na kugundua kuwa Maalim Seif ameongoza na hivyo kuendeleza mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

Kwao CCM wanaamini wanaposhinda iwe kwa hila ama kwa njia halali ndio demokrasia. Wanapokuwa wamebanwa hata kwa mambo yaliyowazi kama uchaguzi wa mameya wa Jiji la Tanga, Kinondoni na Ilala wanatafuta kuongoza kwa njia za kibabe. Hiyo ndio demokrasia inayoimbwa na CCM.

Profesa Ibrahim Lipumba aliwalinganisha CCM na Intarahamwe. Wako tayari waendelee kukaa madarakani hata kama damu itamwagika.

Kwa upande wa Umeya CCM walipobaini kuwa idadi ya madiwani walionao katika Halmashauri za Kinondoni na Ilala haziwezi kuwabeba, na kwa kuwa mshipa wa aibu ulikatika kwa viongozi wa chama hicho wakaamua kuwaingiza wabunge kutoka Zanzibar ili waje Bara kuwa mamluki na kupata Umeya. Uhuni wa namna hii unafanywa na vyama vya siasa vilivyokataliwa na wananchi kama CCM.

Kwa upande wa Jijini Tanga, msimamizi wa uchaguzi aliamua kufanya anayojua kwa kutangaza matokeo kwa kuyapindua. Baada kuhesabiwa kura, mgombea wa CUF alimepata kura 20 na mgombea wa CCM kura 17.

Msimamizi wa uchaguzi huo Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Daudi Mayeji anayedaiwa kuwa ni kada wa CCM akatangaza kuwa mgombea wa CCM amepata kura 19 dhidi ya kura 18 za mgombea wa CUF.

Utaratibu huu haukubaliki, ni wazi kwamba CCM imekusudia kulazimisha kupendwa na wananchi wakati haikubaliki. Utulivu wa Watanzania sio nafasi ya kufanya lolote watakalo. Sasa kama CCM ni chama cha kibabe na udikteta kitangaze wazi kwani haina maana kuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa katika hali hii.

1784 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!