Rais Magufuli, matumizi ya mkaa ni janga la kitaifa (2)

MAGUFULIMkaa unatumika sana mijini kwa shughuli za kibiashara mfano, mama lishe, mighahawa na hoteli mbalimbali. Kusema kweli mkaa ni janga kubwa kwa misitu ya asili na ni mamilioni mengi ya miti inayokatwa kutengeneza mkaa. Inakadiriwa kuwa karibu hekta 300,000 hadi 400,000 za misitu ya asili huharibiwa kila mwaka kutokana na utengenezaji mkaa.

Isitoshe, teknolojia inayotumika kutengeneza mkaa (matanuru ya udongo), inasababisha kupatikana mkaa kidogo wakati miti mingi imetumika. Kwa mfano, mtegeneza mkaa kwa kutumia tanuru la udongo hupata tani moja ya mkaa kwa kutumia tani 10 hadi 12 za miti iliyokatwa.

Kuna umuhimu sana kwa Serikali kutafuja njia mbadala ya kupikia kwa kutumia gesi kama LPG (liquefied petroleum gas) au hata gesi asilia (natural gas) pamoja na vyanzo vingine kama kutumia umeme na pengine kutumia mafuta ya taa. Kusema kweli imekuwa vigumu kwa Watanzania wengi kutumia vyanzo hivyo vya nishati kutokana na gharama zake kuwa kubwa.

Hivyo imekuwa rahisi kutumia mkaa kutokana na kupatikana kirahisi katika maeneo tunayoishi, lakini pia hata kama mtumiaji akiwa na fedha kidogo mfukoni anaweza kukunua mkaa kidogo akapikia chakula chake. Inawezekana kiuhalisia mtumia mkaa akawa anatumia fedha nyingi kwa mwezi ukilinganisha na anayetumia gesi.

Motisha kwa mtumia mkaa ni kwamba anatumia fedha kidogo kidogo kila siku (ana bajeti matumizi ya kila siku) kuliko kutakiwa kununua mtungi wa gesi kwa fedha nyingi mathalani, Sh 50,000 kwa mara moja (kwa mtungi wa kg 15). Majiko ya gesi nayo yanauzwa bei ghali.

Ipo haja kwa Serikali kupitia Wizara inayohusika na masuala ya nishati kuweka sera itakayodhibiti matumizi makubwa na biashara ya mkaa. Kwa sasa inakadiriwa kuwa biashara ya mkaa nchini ni kubwa na inawanufaisha watu zaidi ya 300,000 kuanzia mtengeneza mkaa hadi muuzaji wa rejareja kwa kutumia makopo ya ujazo wa kilo moja au zaidi.

Makadirio yaliyofanywa na wataalam nchini na wengine kutoka taasisisi za kimataifa yanaonyesha kuwa biashara ya mkaa nchini Tanzania, thamani yake inakaribia Sh trilioni mbili kwa mwaka.

Hiki ni kiasi kikubwa cha fedha, lakini kwa kupitia biashara hii ya mkaa miti mingi kutoka katika misitu ya asili inaangamia kila kukicha. Nikiwa njiani kutoka Mpanda Desemba 21-22 mwaka jana kurejea Daes Salaam nimeshuhudia magunia mengi ya mkaa yamerundikwa kandokando ya barabara kuu. Hali inatisha unapofika katika Milima ya Ukwiva hadi Mikumi; kuna magunia mengi ya mkaa.

Vilevile, ukimaliza eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kunzia eneo la Doma hadi maeneo ya Melela mpaka Melela Mlandizi ni magunia mengi ya mkaa. Ukitoka eneo la Segera mkoani Tanga mpaka Chalinze (Bagamoyo) pia kutoka Morogoro–Chalinze– hadi Ruvu ni magunia ya mkaa yasiyohesabika. Nenda mikoa ya Tabora, Geita, Kagera, Kigoma, Katavi, Lindi, Pwani, Mtwara, Rukwa, Ruvuma na Tanga hali ni hiyo hiyo. Je, tutaiacha hali hii iendelee hadi lini?

Kama kuna Sera ya Gesi na Mafuta ni vizuri pia kukawapo Sera ya Biashara ya Mkaa. Sekta binafsi ihamasishwe kupanda miti na kuanzisha mashamba makubwa ya kuzalisha kuni na mkaa.

Kupitia sera husika biashara ya mkaa idhibitiwe na Serikali iweze kukukusanya ushuru kwa faida ya Watanzania. Kisiwe ni kitu kinachowanufaisha watu wachache tu huku tukiacha mazingira yakiendelea kuharibika. Mazingira yanapoharibika athari zake ni kwa viumbe hao wote.

Mkaa ni sehemu ya nishati hivyo Wizara husika idhibiti na kuchukua hatua ipasavyo kuleta uwiano mzuri kati ya vyanzo vingine vya nishati zinazotumika nchini mfano, umeme kwa viwanda na shughuli nyingine; mafuta kwa shughuli za usafirishaji na kuendesha mitambo ya gesi asilia kwa kuzalisha umeme na sasa jitihada makusudi zifanyike kuingiza suala la mkaa kama nishati muhimu ya kupikia chakula na matumizi mengineyo.

Mkaa kiwe chanzo rasmi kwa matumizi halisia ya nyumbani na katika shughuli za kibiashara. Kwa sasa mkaa unatumia kwa wingi, lakini haumo katika mfumo rasmi (formal sector) bali ni katika sekta isiyo rasmi (informal sector) kitu ambacho ni upungufu katika sera za nishati nchini.

Kama kuna Kamishna wa Mafuta na Gesi, basi awepo pia Kamishna wa Mkaa na kuwepo na bajeti ya kuendeleza mkaa kama ilivyo kwa vyanzo vingine vya nishati. Watanzania wanahitaji nishati ya kupikia hivyo wizara husika iwatafutie nishati ya kupikia kama inavyotafuta nishati nyingine kwa matumizi mengine nchini.

Misitu ya asili isiendelee kutegemewa kama chanzo kikuu cha kupata mkaa, bali kutafutwe vyanzo vingine mbadala. Wataalam wa misitu kupitia Idara ya Misitu na Nyuki na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS jukumu lao kubwa ni kuhifadhi misitu ya asili na pia kuanzisha na kuendeleza mashamba ya miti.

TFS inaweza ikawa na mashamba ya miti ili kutoa nishati ya kuni na mkaa, lakini katika kutekeleza hilo waongozwe na Sera ya Nishati ambayo itaweka mambo bayana hadi kwa sekta binafsi na kwa wawekezaji wengine ili waanzishe mashamba ya miti ya nishati. Tanzania inahitaji sana misitu ya asili kuendelea kupata huduma za kiikolojia kwa misingi iliyo endelevu kwa ajili ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.

Kwa mfano, misitu inasaidia sana kuondoa gesi ukaa (Carbon dioxide-CO2) ambayo ni hatari sana kwa mabadiliko ya tabianchi. Misitu inaondoa gesi hiyo kutoka katika mfumo wa hali ya hewa duniani na kuihifadhi, na badala yake huweza kutoa gesi aina ya Oksijeni (O2) ambayo hutumiwa na binadamu pamoja na wanyama. Misitu inahifadhi vyanzo vya maji lakini pia inachangia upatikanaji mvua. Misitu inasaidia sana kuhifadhi na kurutubisha udongo ndiyo maana wakulima maeneo yao yakiishiwa rutuba wanavamia maeneo yenye misitu wakijua kuwa udongo una rutuba nyingi.

Vilevile, misitu ya asili ni maeneo mazuri kwa makazi ya wanyamapori na upatikanaji wa chakula chao. Wanyamapori wakipata makazi mazuri, wakapata maji na chakula cha kuwatosha, watalii wataweza kuja Tanzania kwa wingi na nchi itanufaika kimapato.

Lakini sana matumizi ya misitu ya asili yasiyo endelevu ikiwamo kilimo cha kuhamahama na ufugaji usiokuwa na tija pamoja na uchomaji mkaa vinasababisha mito kama Katuma unaopita katikati ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi kukauka kila mwaka wakati wa kiangazi hivyo kusababisha wanyamapori kupata shida kubwa.

Hali kama hiyo kwa miaka mingi inatokea katika Hifadhi ya Taifa Ruaha kutokana na Mto Ruaha Mkuu (Great Ruaha) kukauka maji kutokana na kuharibika kwa vyanzo vyake na umwagiliaji uliokithiri kwa kutumia maji mengi kupita kiasi.

Isitoshe, kutokana na misitu tunapata dawa za asili (miti shamba) na hata sehemu kubwa (asilimia 75) ya dawa za hospitali vyanzo vyake ni misitu na mimea mbalimbali. Kuna faida nyingi zinazotokana na misitu ya asili ambazo sijazitaja hapa kama vyakula vya asili na mbogamboga.

Nimalizie kwa kusema kuwa kila jitihada zifanyike ili kuinusuru misitu ya asili isiendelee kuangamia kwa mahitaji makubwa ya mkaa. Wataalaam wa misitu na nyuki tujivunie kuihifadhi misitu na isiwe kinyume cha hapo. Kama ni matumizi kwa mantiki ya kupata bidhaa zinazotokana na misitu, bidhaa hizo ukiwamo mkaa zitokane na usimamizi ulio thabiti na kwa matumizi endelevu.

Ni sharti kutumia mpango wa usimamizi uliyoidhinishwa ili kuruhusu uvunaji au matumizi mengineyo. Kinyume cha hapo tutakuwa hatuitendei haki misitu ya asili pamoja na sekta nzima ya misitu na nyuki. Taratibu, Kanuni na Sheria vifuatwe. Tafadhali Rais Magufuli, nakuomba sana uokoe misitu. Mkaa ni janga la kitaifa.

Mwandishi wa makala hii, Dk. Felician Kilahama ni Mkurugenzi Mstaafu, Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii.