Kama Watanzania wataulizwa leo nini walichokuwa wakikitarajia kwa nchi yao ya uhuru na kazi, basi jibu ni moja tu kwamba tulikuwa tunataka mabadiliko ya kuachana na mabepari wachache waliohodhi mali zetu ambazo tulizipata kutokana na jasho la siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, mali hizi awali tuliona ni zetu na zilikuwa zinatusaidia kama Watanzania na kutuletea maendeleo.

Kama Watanzania wataulizwa leo juu ya viongozi wa Serikali yao walikuwa wakitarajia nini, napo jibu linaweza kuwa ni kwamba walitarajia kuwa na viongozi wa kuwatumikia kutokana na kodi zao na siyo viongozi miungu-watu ambao waligeuka kuwa kero katika maisha yao na nyadhifa hizo waligeuza kuwa za urithi na uchifu.

Watanzania sasa wanaona kama matarajio yao yako mbioni kukamilika kutokana na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kurekebisha mfumo wa Serikali na kuondoa uchifu ambao ulikuwa unawakera sana wananchi wengi waliokuwa wamewapa dhamana ya madaraka ya kuongoza idara na taasisi mbalimbali.

Katika siku za hivi karibuni, kuna matukio ambayo yanajulikana kwa jina la kutumbua majipu, majipu hayo yanaonekana kuwafurahisha wananchi kwa sababu wanaona baadhi ya viongozi wakiwajibika kwa wananchi ipasavyo na baadhi wakienguliwa kwa kushindwa kuwasimamia walio chini yao, au kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kila siku kama wakuu wa sehemu husika.

Watanzania walifika mahali walikosa imani, uzalendo, utu, uamuzi, mapenzi baina yao, Watanzania walikosa uhuru wa kujidai mbele ya walio utumwani, Watanzania walikuwa watumwa kwa Watanzania wenzao, Watanzania walikosa imani na viongozi wao, Watanzania walikosa utu wa mtu wa Kitanzania na uzalendo wa kulipenda Taifa lao, Watanzania waliuana kwa kukosa mapenzi na kuamini ushirikina, Watanzania walikosa uwezo wa kutoa uamuzi sahihi kwa wakati sahihi.

Yote haya yalifanyika kwa kutokuwa na imani kwa baadhi ya viongozi ambao tuliwapa dhamana. Watanzania wameanza kuwa na imani baada ya kuanza kubaini mianya na matendo maovu ya baadhi ya viongozi ambao tayari wamechukuliwa hatua na wengine wakichukuliwa hatua.

Watanzania wameanza kuwa na imani kwa Serikali yao baada ya kuona usawa na haki vinakaribia kupatikana katika mfumo wa utawala uliopo, Watanzania wameanza kuona kuwa hii ni nchi yao na wana haki ya kumiliki mali zilizopo hapa nchini, huu ndiyo uliokuwa mpango mkakati wa enzi zile za siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Watanzania wanaona wanatoka katika minyororo ya utumwa wa kulishwa wasichotaka, kupewa wasichopenda, kupelekwa wasikojua, Watanzania wanaanza kuona matunda ya uhuru kwa kuelezwa haki zao, wanaona utawala bora uko mbioni kupatikana, wanaona usawa katika sheria na haki za kimahakama.

Watanzania wanatarajia kuona mali zao zikirudishwa na waliopora wakipelekwa mahakamani, Watanzania wanashuhudia waliokuwa viongozi wakihaha na kutafuta suluhu na watu waliokuwa wakionekana watumwa kwao, Watanzania wanaiona nuru ya nchi wakiwa mbali.

Watanzania wanaona fursa ya kufaidika na rasilimali za Taifa lao, wanawaona watu wachache ambao waligeuza rasilimali kuwa mali yao binafsi wakihangaika kujijumuisha katika ushiriki wa kuturejeshea mali zetu, wanawaona wakiomba msamaha na kujifanya ni watu miongoni mwetu na wanataka suluhu.

‘Hapa kazi tu’ ni kaulimbiu ambayo sasa ipo midomoni mwa masikini wote wa nchi hii, masikini ambao kwa namna moja ama nyingine wapo nyuma ya uongozi wa awamu ya tano kuhakikisha unatekeleza azma ya kuwaletea maisha bora ambayo wameyakosa kwa kipindi kirefu.

Rai yangu kwa uongozi wa awamu ya tano ni kuhakikisha kuwa malengo waliyojiwekea na ahadi walizozitoa zinatekelezeka, na kwa kuwa Watanzania sasa wameanza kuwa na uzalendo, ni dhahiri kuwa watatoa ushirikiano wa hali na mali kama ilivyokuwa zamani wakati wa ulinzi wa kila mwananchi.

Watanzania sasa wana matumaini makubwa sana, wana ari ya ajabu baada ya kuona majipu makubwa yakianza kutumbuliwa ili kuirejesha Tanzania yetu, wanaamini katika umoja na ulinzi wa pamoja kufikia malengo, Watanzania wa sasa ni wale waliokuwa wamekata tamaa ya maisha na sasa wanaona nuru ya matumaini.

Tunawatakia kila la heri viongozi wetu mlioapa kututumikia na kutuletea mabadiliko tuliyokuwa tukiyatarajia kwa muda mrefu. Hali kadhalika, heri ya Mwaka Mpya wasomaji wetu wote, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika na mapambano yaendelee dhidi ya mafisadi waliotutawala kwa muda mrefu. 

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo.   

By Jamhuri