Wakati  mwingine  kujilinda  waweza  kukuita  kujitetea, kujiokoa au kujikinga.  Ni hali ambayo  mtu hufanya jitihada za kujinasua katika  tendo ovu linalotekelezwa na  mtu  mwingine  dhidi  yake.   Mfano  wake  ni  kama  kuvamiwa  na  majambazi, kutekwa, kufanyiwa  fujo  ya  aina  yoyote, kupigwa au  kujaribu  kupigwa n.k. Matukio ya  namna  hii  au  yanayofanana  na  haya ni  sehemu  yetu  ya  maisha.  Yumkini yanapotutokea huwa tunachukua hatua. Na moja ya hatua    za awali kabisa  tunazochukua huwa ni kujaribu kujitetea au kujikinga  nayo.

Umevamiwa  nyumbani   na  majambazi,  umefanyiwa  fujo  njiani  kwa sabasbu  yoyote ile  na  wewe  unaamua  kujitetea  ili  usidhurike,  na  katika  kujitetea  huko unasababisha  kifo  cha  mtu – awe  yule aliyetaka kufanya  fujo au mwingine mpita  njia, sheria inasemaje kuhusu mkasa  wa  aina  hii?  Makala itaeleza  japo  mambo  ya  msingi  kuhusu  hali hii. 

 

1. HAKI YA KUJILINDA

Haki  ya  kujilinda  ni  haki  ya  kisheria. Ni  haki  ambayo  ipo  kwa  kila  mtu.  Mbali  na  kuwa  haki hii  ni ya  kisheria  pia  haki hii ni  ya  kuzaliwa. Kuna  tofauti  kati  ya  haki  kuwa  kisheria  na  kuwa  ya  kuzaliwa. 

 Haki  za  kisheria  ni  zile  haki  zote  ambazo  zimeelezwa  ndani  ya  sheria.  Zimekuwapo  baada  ya sheria  kutungwa na  hivyo  kabla  ya  sheria  kutungwa  hazikuwapo. Haki  ya  kuzaliwa  ni  haki  ambayo  imekuwapo  tangu  mwanadamu  wa  kwanza  alipoumbwa. Ni haki ambayo  mtu  anazaliwa  nayo. 

Haki  hii  haihitaji  kuwa  ndani  ya  sheria ili  mtu  awe  nayo  isipokuwa  tu  anapozaliwa  huzaliwa nayo, hukua nayo  na  hufa  nayo. Kujilinda  au  kujitetea  pale  mtu  anapotaka  kukudhuru hakuhitaji kuwa ndani  ya  sheria ili ndiyo umzuie asikudhuru, isipokuwa ni  jambo ambalo  hutokea  lenyewe (automatic). Lipo tu hata sheria isiliseme.    Kwa hiyo, pamoja na kuwa haki  ya  kujilinda usidhurike ni  haki ya  kisheria, lakini  kubwa  zaidi  ni kuwa haki  hii  ni  haki  ya  kuzaliwa.  

Haki nyingine  za  kuzaliwa  ni  kama  haki  ya  kuishi. Ukishazaliwa haki ya  kuishi  inakuwapo siyo  mpaka  iwe  kwenye  sheria, haki  ya  kuzungumza, ikiwa  umezaliwa  unazungumza  basi  hiyo  ni  haki  ambayo  husubiri  sheria  iitoe, haki  ya  kutembea n.k. Haki  ambazo  si  za  kuzaliwa  ni  kama  hizo  za kuchagua au  kuchaguliwa,  kupiga kura, haki  elimu n.k.

 

2.   UNAPOSABABISHA KIFO UKIJARIBU KUJILINDA/KUJITETEA

Kifungu  cha  18 cha  Kanuni za Adhabu, sura  ya  16 kinasema  kuwa mtu  hawezi  kuwajibika  kijinai  kwa  kitendo alichokifanya wakati wa kutimiza  haki  yake  ya  kujitetea, kumtetea  mtu  mwingine,  au  kutetea  mali. 

Kifungu  hiki  kinasomwa  na  kifungu  cha  18c kinachosema  kuwa  haki  ya  kujilinda, kumlinda  mtu  mwingine au  mali itatumika  kwa  mtu  yeyote  ambaye  katika  kutumia  haki hiyo  atasababisha kifo  au  dhara  kubwa  kwa  mtu  mwingine. 

Maana  ya  vifungu  hivi  ni  kuwa  haki  ya kujilinda  itatumika  kama  kinga  kukuondolea hatia  ya  jinai  iwapo umesababisha  kifo. Lakini  ili ikubalike  kama  kinga  na  usitiwe  hatiani  kwa  kosa  la  kuua,  vifungu  hivi  vimetoa  masharti  yafuatayo:

( a ) Kwanza  wewe  uliyesababisha  kifo  uwe  umesababisha  kifo  hicho  kwa  nia  njema  kwa  maana  ya  kuwa  ulikuwa  kweli  kabisa  ukijilinda  usidhurike. Isije  kuwa  unatumia  nafasi  ya  kujilinda  kumuua  au  kumdhuru  mtu  mwingine   kwa  makusudi  ukijifanya  ulikuwa  ukijilinda. Swali la ‘ulifanya makusudi au  kwa  nia  njema ya  kujilinda’ litathibitishwa  kitaalamu  na  mazingira ya tukio husika.

( b ) Kitendo ulichofanyiwa  kiwe  ni  kitendo  ambacho  kiukweli  ulitakiwa  kutumia  nguvu  kiasi  cha  kusababisha  kifo. Isiwe mnatupiana maneno mawili matatu halafu unasababisha kifo kwa  kisingizio  kuwa ulikuwa ukijilinda usidhurike. Kuwe  na  mazingira  ambayo hata  ukiyatizama  yafanane  na  hatua  ya  kujikinga  hadi  kusababisha  kifo.

( c )  Pia  ikiwa  kitendo  kinahusu  kubaka  au kufanya  kinyume  na  maumbile,  kinga  ya  kujikinga  hadi  kusababisha  kifo inaswihi.

( d ) Pia  kujikinga/kujitetea hadi kusababisha  kifo kunakubalika  ikiwa tendo linahusisha  kuteka  nyara  au  kutorosha.

( e ) Pia  matendo  kama  kuvunja  na  kuingia, unyang’anyi, kuchoma moto, nayo yanakubalika   katika  kujikinga  hadi  kusababisha  kifo. 

Kwa kumalizia,  zingatieni  kuwa  ikiwa  upo  katika  mazingira unayoweza kujikinga/kujitetea  bila  kusababisha  kifo  au  madhara  makubwa,  basi  ni  vema  kufanya  hivyo. Kujikinga hadi  kuua liwe chaguo  la mwisho  pale  unapokuwa huna  namna  nyingine  yoyote  isipokuwa  kufanya  hivyo. 

 

Kuhusu sheria  za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea  SHERIA  YAKUB BLOG.

By Jamhuri