Chameleon atwaa tuzo ya mwanamuziki bora Uganda

Msanii maarufu wa muziki nchini Uganda, Joseph Mayanja, maarufu kama, Jose Chameleon, hivi karibuni alitwaa tuzo ya msanii bora wa kiume wa kimataifa nchini humo. Chameleon ametwaa tuzo hiyo baada ya kuibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha Msanii Bora wa Kiume wa mwaka katika tuzo za Africa Entertainment Awards, zilizofanyika jijini Kampala, hivi karibuni.

Ushindi wa tuzo hiyo unazidi kumpa nafasi mwanamuziki huyo kuendelea kung’ara katika tasnia ya muziki ndani na nje ya Uganda, na hata katika ukanda wa nchi za Afrika.

 

Baada ya kupokea tuzo hiyo, Chameleon aliwashukuru mashabiki wake akisema kuwa bila wao yeye asingeweza kutwaa tuzo hiyo, ambayo alisema kuwa kwake anaiona kama kitu muhimu zaidi kinachodhihirisha maendeleo yake kimuziki.

 

Lengo la tuzo za African Entertainment Awards ni kuonesha thamani ya muziki na urithi wa utamaduni kwa wanamuziki wa Afrika.

 

Kadhalika, lengo la tuzo hizo ni kuwatia moyo wasanii ambao wametumia sanaa na utamaduni wa Mwafrika katika kuonesha utaalamu wao kubuni mitindo mbalimbali katika taaluma ya burudani.

 

Mbali ya utoaji wa tuzo, tamasha hilo lilitawaliwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wa nchini Uganda. Mwaka 2002 Chameleon alipata mwaliko wa kutumbuiza katika michuano ya Olimpiki katika Jiji la London, Uingereza.

 

Kadhalika, msanii huyo amekuwa katika maelewano mazuri na kampuni ya AS Entertainment ya Afrika Kusini, ambayo pia ilimpa mchongo wa kufanya maonesho wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.

 

Hivi karibuni, ametoa wimbo mpya wenye jina la Badilisha ambao tayari umekubalika katika soko la Afrika Mashariki. Kutokana na umahiri wake katika kushambulia jukwaa, wapenzi wake wamembatiza jina kwa kumuita Dokta wa Muziki.